Thursday, September 22, 2011

Askofu Kilaini aonya ushoga katika Katiba

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini ameonya Taifa kutokukubali kuingiza suala la ushoga katika Katiba mpya kwa kuwa kufanya hivyo ni kuliingiza taifa katika laana ya Sodoma na Gomora.

Amesema huo ni ugonjwa unaohitaji tiba na si kuubeba kama kitu cha kawaida kwa kuwa bila kuutibu, Watanzania wengi wataugua na kumalizika kabisa hasa watoto na vijana.

Askofu Kilaini aliyewahi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam alipotakiwa kuzungumza kwa nafasi ya kiongozi wa dini na waandishi wa habari nje ya Kongamano la Maaskofu la siku mbili linalojadili masuala ya Katiba na Utawala Bora.

Kongamano hilo limeandaliwa na Kikundi cha Mazungumzo cha Umoja wa Makanisa (TEDG) ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kushirikiana na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC).

“Katika hilo hakuna kukwepa kuwa huo ni ugonjwa na ugonjwa unatafutiwa dawa si kuubeba, ushoga si maumbile ya kawaida ya binadamu, bali ni ugonjwa, Taifa lazima liwe macho katika hili, tuliweke taifa katika laana ya Sodoma na Gomora (miji iliyoangamizwa na Mungu kutokana na kukithiri kwa matendo maovu), “ alisema Askofu Kilaini.

Alisema ikiwa watatambulika na kutokea kupewa kulea yatima watakapofunga ndoa, mtoto atamuita nani baba au mama kati yao, hivyo tatizo litakuwa kubwa zaidi kuliko inavyofikiriwa jambo analoamini ni nguvu ya mataifa tajiri kuharibu vizazi vya Watanzania.

Alisema jambo hili si la kawaida kama linavyotaka kufanywa, bali linatakiwa kutafutiwa dawa ili liishe na si kulilea kwa kuwa ni ugonjwa unaoambukiza.

“Hili si suala la dini tu bali ni suala la ubinadamu, waliokwisha kuingia wanapaswa kusaidiwa kutoka, si rahisi kurejea hali ya kawaida lakini wanaweza kuwa wanaume wazuri pia,” alisema askofu huyo maarufu.

Alipendekeza wasizuiwe kutoa maoni wakati wa mchakato wa Katiba mpya kwa kuwa ni Watanzania, lakini si kuingizwa na kutambuliwa na Katiba na kushauri elimu na ushauri iwe njia ya kuwasaidia huku wazazi wakihakikisha wanakuwa wazi kuzungumza na watoto wao kuhusu ubaya wa suala hilo.

Hivi karibuni katika Tamasha la 10 la Jinsia, mashoga zaidi ya 20 kutoka Zanzibar na Dar es Salaam walihudhuria na katika kuchangia mada, walitaka waruhusiwe kutoa maoni wakati wa mchakato wa Katiba mpya na iwatambue ili wapate ulinzi wa kikatiba.

No comments: