Monday, September 5, 2011

Kamati ya kumchimba Jairo kuanza kazi leo

Mwenyekiti wa Kamati Teule ya kuchunguza tuhuma za Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, kuingilia Haki na Madaraka ya Bunge ya kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Ramo Makani, amesema leo kamati yake itakutana kwa mara ya kwanza na kupitia hadidu za rejea ili waanze kazi hiyo.

Makani ambaye ni mbunge wa (Tunduru Kaskazini-CCM), anawaongoza wabunge wengine ambao ni, Gosbert Blandes (Karagwe-CCM), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF), Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).

Akizung na gazeti hili jana, Makani alisema watakutana leo asubuhi na kuongeza kuwa mbali na kupitia hadibu za rejea, watapanga ratiba ya kufanya kazi hiyo.

Julai 26, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, liliunda kamati hiyo yenye wajumbe watano itakayokuwa na kazi ya kuchunguza sakata zima la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Kamati hiyo iliundwa kabla ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge, baada ya wabunge kuridhia ufanyika uchunguzi huo.

Spika Makinda pia alizitaja hadidu rejea za kamati hiyo kuwa ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilisha uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.

Nyingine ni kamati hiyo kuangalia uhalali wa utaratibu huo kisheria ama kikanuni, iwapo fedha hizo kama zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na kuangalia matumizi halisi ya fedha husika.

Pia kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kukamilisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara hiyo bungeni.

Vilevile, kuchunguza mfumo wa serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na utaratibu wa kuliarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.

Nyingine ni kuangalia nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na kuangalia mambo mengine yoyote yanayohusiana na masuala hayo.

Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda usiozidi wiki nane na itawasilisha taarifa yake wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge, utakaoanza Novemba 8, mwaka huu.

No comments: