Friday, October 3, 2008

Wabunge wa Afrika Mashariki wapigiwe kura na Wananchi wote– Wabunge

Wabunge wa Tanzania wametaka ubunge wa Afrika Mashariki uwe ni wa kupigiwa kura na wananchi wote ili kuongeza kasi ya uwajibikaji ya wabunge hao badala ya utaratibu wa sasa kuwa wabunge ndio wanaowapigia kura.

Maoni hayo ya Wabunge wa Tanzania yametolewa na Mwenyekiti wa Bunge la Tanzania Mhe. Zuberi Ali Maulid alipokuwa akitoa salamu za Tanzania katika mkutano wa mahusiano ya Mabunge ya Afrika Mashariki unaofanyika mjini hapa.

‘’Katika kipindi hiki ambacho Bunge la Afrika Mashariki limekuwa likitunga sheria zenye kuathiri Wananchi kwa ujumla na kwa kuwa Wabunge wa Jamhuri hawana fursa ya kujadili maamuzi ya Bunge hilo, ni vyema wabunge hawa wa Afrika Mashariki wakawa wanachaguliwa moja kwa moja na wananchi’’ alisema Mhe. Maulid.

Mheshimiwa Maulid aliongeza kuwa ni muhimu pia kwa Mkataba wa Afrika Mashariki na Sheria za Tanzania kurekebishwa ili kuruhusu Wabunge wa Bunge la Tanzania kujadili na kupitisha maamuzi ya Bunge la Afrika Mashariki, ‘’ Maamuzi wanayoyatoa yana athari kubwa kwa watanzania wote, hivyo ni vyema maamuzi yao kabla ya kutekelezwa yapate baraka za Bunge la Tanzania kwa kujadiliwa’’ aliongeza Mheshimiwa Maulid.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambae pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa akifungua mkutano huo alisema kuwa bado kuna vikwazo vidogo vidogo katika kufikia ushirikiano wa pamoja kutokana na hofu zisizokuwa na msingi.

‘’Katika kipindi ambacho mazungumzo ya kuwa pamoja zaidi yanasuasua ni vyama wananchi wakaelewa kuwa kwenye ushirikiano huwa siku zote kuna hasara za muda mfupi lakini faida zake ni za kudumu", alisema.

Katika mkutano huo, Tanzania inawakilishwa na Mheshimiwa Zuberi Maulid ambae ndio kiongozi wa msafara na wapo pia Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mheshimiwa Zitto Kabwe pamoja na Waheshimiwa Godfrey Zambi, Masolwa Cosmas, Beatrice Shelukindo, Ruth Msafiri na Hassan Kigwalilo.

3 comments:

Anonymous said...

Naungana na wabunge kwa hilo, ni utaratibu wa kizamani unaotumika, ni vema tukawachagua kulingana na sifa na uwezo wao.

Kutuwakilisha nje ya nchi tena huko wanakutana na wakenya na waganda ambao kila siku tunawahofia na huku sisi tunapeleka vilaza na kuteuana bila vigezo vya msingi imepitwa na wakati na wataenda kusinzia tu kwenye bunge hilo. Tena hata wabunge hao wa Afrika mashariki wasichaguliwe kutoka miongoni mwa wabunge wa Bunge letu, wagombee watu tofauti na wabunge wa Bunge la Jamhuri kwa vigezo vinavyotakiwa.

Andrew Makune

Anonymous said...

Naungana nawewe Andrew, huwa wanateuana bila vigezo muhimu!!!

Ni vema tukawachagua nje ya Bunge la jamhuri tena wawe wasomi hasa wenye kuleta ushindani.

Joel

Anonymous said...

Wana GDSS tunataka mada hii iletwe tuijadili jumatano kabla haija-expire. Tafadhali TGNP!!!!

Mkereketwa wa GDSS