Thursday, October 23, 2008

Mwalimu Nyerere: Mwanaharakati mchochezi wa maasi matakatifu

Wiki jana Oktoba 14, Watanzania waliadhimisha miaka tisa ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, Mjini London, Uingereza kwa ugonjwa wa kansa ya damu.

Ni kwa yapi Mwalimu anapaswa kukumbukwa? Ni kwa yapi anastahili kuigwa na jamii ya Kitanzania na Jumuiya ya kimataifa kwa ujumla?

Ukiachilia mbali ushupavu wake na heshima aliyojipatia kwa kupigania na kuleta Uhuru, Mwalimu ni mtu wa ngano na simulizi nyingi, kuanzia staili ya maisha yake, tabia na fikra zake.

Hakuna mazingira wala hali yoyote ya kuonyesha kwamba Mwalimu alijilimibikizia utajiri kihalali au vinginevyo wakati na baada ya utumishi wake, aliporejea na kuishi kijijini kama raia wa kawaida, mwaka 1985.


JK Nyerere
Mwalimu J.K. Nyerere

Nyumba yake ndogo imejengwa sehemu ile ile ilipokuwa nyumba ya baba yake, Chifu Nyerere Burito, imetuama juu ya miamba ya kilima cha asili cha Mwitongo, kijijini Butiama. Ni ndogo mno kutostahili hadhi ya mtu aliyekuwa kiongozi wa kimataifa.

Baada ya kuona kwamba kijumba hicho kidogo hakikustahili hadhi ya rais mstaafu kama Mwalimu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) lilijitoleaa kuipanua, kama alivyopata kusema yeye mwenyewe: “Vijana waliona vyema Amiri Jeshi wao Mkuu anastahili nyumba ya wageni, lakini ni masikini, hana fedha”, akimwambia mwandishi wa makala haya, alipomtembelea nyumbani kwake Butiama, Februari 1999, miezi kadhaa kabla ya kwenda London kwa matibabu.

Kuna kipindi kufuatia kupinduliwa kwa Rais Kwame Nkurmah wa Ghana, mwaka 1966, Dar es Salaam ilionekana kuchukua nafasi ya Accra kama “Makkah” ya Afrika kwa wanaharakati Weusi; na kwa kufuta mwangwi wa hotuba za nguvu na za kiimahiri za Nkurumah, Tanzania, chini ya Rais Nyerere, ilishika hatamu za fikra za kimapinduzi kwa ladha ya ukurasa wa Afrika ya kale.

Mwalimu hakupenda makuu, kujikuza au urasimu mwingi, alichukia utajiri: “Kimsingi mimi ni mkulima (mdogo) na Mjamaa. Hakuna mtu anayeweza kutajirika kwa kazi yake. Milionea hawi milionea kwa jasho lake; lazima atakuwa amewanyonga wengine; mpe mtu huyo kisiwa chake uone kama atatajirika”, alipata kusema.

Kuhusu wanasiasa wanaojikweza majukwani na kutoa misaada ya mamilionoi ya pesa kwa wengine, Mwalimu, katika kitabu “Binadamu na Maendeleo” , akimnukuu Mtakatifu Ambrose, anasema, “ Humpi masikini sadaka ya mali yako, unampa kilicho chake, maana wewe umenyakua na kukifanya chako peke yako. Kile kilichopo kitumiwe na watu wote”.

Anaendelea: “Hakuna yeyote mwenye haki ya kutumia mali (rasilimali za taifa) hiyo anavyotaka. Hakuna yeyote mwenye haki ya kulimbikiza mali, au kitu asichokihitaji akitumie peke yake, wakati wengine hawapati hata mahitaji ya lazima….”

Mwalimu aliwahi kutamka wazi kuwa hakuhitaji utajiri, alisema:
“Nihitaji utajiri kwa ajili gani? Nilikuja duniani uchi na nitarudi uchi; sioni sababu kwa nini nijihangaishe na mambo ya utajiri; natimikia watu wangu, utajiri kwangu wa nini?”

Mwalimu alikufa fukara, lakini kwa utumishi uliotukuka. Katika enzi hizi za ufisadi, mafisadi wangapi wanao ujasiri wa kuwaza au kusikiliza ujumbe wa Mwalimu? Na wameadhimishaje siku hiyo?.

Mwalimu alianza kufikiria juu ya “Ujamaa” alipokuwa Chuo Kikuu Nchini Uingereza, lakini hakuwa muumini wa sera za Ki-Karl Marx kwa sababu, anasema, Karl Marx alitawaliwa na nadharia za kibaguzi za ki – Darwin, zilizomwona Mwafrika kama binadamu wa daraja la pili.

Hakutaka kuigiza Ujamaa wa Ki – Ulaya kwa sababu ulijikita zaidi katika dhana ya migongano ya kitabaka, wakati huo Afrika haikuwa na matabaka, anasema, “Ujamaa wa ki – Ulaya (Socialism) ni matokeo ya upepari uliokomaa… (lakini) lengo letu lilikuwa ni kuleta maendeleo wakati huo huo tukibakiza moyo wa jumuiya asilia”.

Baadhi ya watu walihoji ni vipi Mwalimu aliweza kuchanganya harakati za kisiasa, dhana za Karl Marx, ibada na hata dhana ya kuwapo Mungu bila kuathiri kimojawapo.

Kwa hili Mwalimu alipata kusema: “Kama ningeziogopa harakati kwa kisingizio cha kulinda imani yangu ya dini, nisingeweza kuongoza mapambano ya Uhuru wa nchi hii; ingekuwa ni sawa na kudhalilisha Ukristo wangu na Kristo, ambaye yeye mwenyewe alikuwa mwanaharakati na mwanamapinduzi”

Msimamo huu wa Mwalimu umewekwa wazi katika kitabu chake “Binadamu na Maendeleo”, kwamba: “Kanisa likubali kuwa maendeleo ya watu maana yake ni maasi… watu hufikia hatua ya kuyakataa mambo yanayowabana katika Uhuru wao kama binadamu”

Mwaliimu aliasa, “Ikiwa hatutashiriki kwa vitendo katika mapambano ya kuondoa utaratibu wa maisha na wa uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonge, basi Kanisa litakuwa halina uhusiano na maisha ya binadamu, na dini itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za ushirikina zinazokubaliwa na wenye hofu tu”.

Mwalimu aliamini kuwa maendeleo lazima yamaanishe maasi matakatifu, kwa sababu ya kuleta mabadiliko, alisema: “Tunasema kwamba, binadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Mimi nakataa kumfikiria Mungu aliyefukara, mjinga, mshirikina, mwoga, dhalili, ambayo ndiyo hali ya walio wengi kati ya wale aliowaumba kwa mfano wake mwenyewe”.

Mwalimu aliamini pia kwamba yote hayo yanasababishwa na binadamu kwa binadamu mwenzake, alisema: “ Lakini tulivyo hivi sasa tu viumbe, tena si viumbe wa Mungu, bali wa binadamu wenzetu… Kanisa lazima lishambulie wazi wazi mtu au kikundi chochote kinachosaida kudumisha unyonge huo wa mwili na roho, bila ya kujali misukosuko inayoweza kutokea kwa kanisa au kwa wafuasi wake.”

Mwalimu alichukia tabia ya kuiga kila kitu bila kuhoji sera, mifumo ya maendeleo na demokrasia ya kigeni kwa kutozingatia mazingira na hali halisi ya nchi yetu: “Angalia wanavyoishi kule Marekani; ni fujo na uhuni mtupu. Kama wanakuvutia kwa gharama ya watu wetu, fungasha mizigo uende ukaishi huko kama wao. Hapa lazima jicho lako liwe kijijini kwa wanavijiji; usiangalie hizo gari mbili na majokofu na vitu vyote katika nchi za kibepari, bado wanaendelea kutunyonya. Sisi tunataka kujenga jamii yenye usawa, jamii iliyostaarabika, tukipewa muda”, alisema.

Juu ya demokrasia na Maendeleo, Mwalimu aliona kuna mambo mawili muhimu: la kwanza, ni uongozi wa kueleza, na la pili, ni demokrasia katika kuamua mambo: “Maana uongozi si kukemea watu; maana yake si kuwatukana watu au kikundi cha watu usiokubaliana nao; wala maana yake si kuamuru watu kutenda lile wala hili. Uongozi maana yake ni kuzungumza na kushauriana na watu ukawaeleza na kuwashawishi. Maana yake ni kuwa mmoja wao na kutambua kwamba wao ni sawa na wewe”

Mwalimu aliamini kwamba uongozi hauwezi kuchukuwa nafasi ya demokrasia; uongozi lazima uwe sehemu ya demokrasia. Alihuzunika baada ya kustaafu kubaini kwamba rushwa serikalini ilianza kuchukua umbo la kulitaifisha Taifa.

Ni wakati huo pia alipong’amua kwamba chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM), kilikuwa kimekoma kuwa chama cha wanachama na kuwa chama cha viongozi. Na kwa sababu hiyo alianzisha mjadala juu ya mfumo wa vyama vingi nchini.

Mwalimu alinukuliwa akisema: “ Kiitikadi, mimi ni mtu wa Chama kimoja. Lakini nimeanzisha mjadala huu kwa sababu ile dhana kwamba ni mwiko kuhoji Katiba yetu si ya kidemokrasia…. Siwezi kukubali; nasema, kama hawa jamaa (watu) wanataka mfumo wa vyama vingi, waache waanzishe….”

Mwalimu alikwisha kututoka. Ni kweli alikuja mtupu duniani na amerudi mtupu, lakini fikra zake zinaishi. Hata hivyo, tumejionea jinsi fikra hizo zinavyopigwa vita na vikosi vya nyang’au wa uchumi na siasa ili washike hatamu za nyanja hizo kwa maangamizi ya uchumi, Taifa na watu wake.

Ilivyo sasa uzalendo unatoweka haraka, maadili yanayoyoma. Uongozi umenyakuliwa na wasomi wachache wanaojifanya kuyaelewa matatizo yetu, wakati ni kinyume chake. Wameunda mtandao na mabwana wa ubepari wa kimataifa; viongozi wamepungukiwa hisia za kitaifa zinazozaa uzalendo, ushujaa, kujitoa mhanga kwa nchi. Wamekuwa kama watu wanaojiaandaa kustaafu na kuishi ughaibuni.

Kwa tabaka hili dogo, lakini lenye nguvu, demokrasia sasa maana yake ni kukamata mawazo ya watu wasio na elimu ya demokrasia kwa kuwanunua kwa nguvu ya pesa na kunyakua madaraka ya kisiasa.

Viongozi wamebweteka na kubugia sera zinazowakamua masikini kuwatajirisha mabepari wachache. Badala ya kuwa watumishi wa watu wamegeuka kuwa mabwana zao. Wasomaji watajiuliza: Kwa nini Watanzania, kila wanapokerwa na jambo, wanaimba, “ Kama si juhudi zako Nyerere… x 3; … na uhuru, elimu, amani… tungepata wapi?”.

Ni kwa sababu Nyerere, kama mwanaharakati na mwana mapinduzi, alichochea moto wa maasi yasiyozimika, hadi ushindi upatikane kwa “Wasakatonge”.

2 comments:

Anonymous said...

Ndugu mwandishi, unapomtaja Mwl. Nyerere unanitonesha kidonda na natamani hata afufuke leo hii aone yanayotendeka.

Mwalimu alikuwa mtu mwenye kufuata misingi ya haki na utawala bora, kwasasa haya yote yamepotea tunapelekwa kama wanyama hakuna sheria wala kanuni za kufuata,wenye madaraka wenyewe sheria haiwahusu.

Mwalimu tutamkumbuka milele!!

Fatuma Mussa

Anonymous said...

kuna haja kubwa ya kuleta mapinduzi ambayo mwalimu nyerere liyasimamia kwa nguvu zake zote wakati alipokuwa hai. viongozi wa siku hizi wameshindwa kushika yale ambayo mwalimu aliwafundisha. basi kama kuna mambo ambayo mwalimu alifeli ni pamoja na kushindwa kutuachia urithi wa viongozi bora, na jambo hili ndilo linalotusikitisha wananchi wa hali ya chini.
mwanaharakati.