Thursday, October 30, 2008

Mfululizo wa Semina za GDSS.

Mada ya Jumatano hii ya tarehe 29/10/2008 ilikuwa ni mrejesho wa Mwenge wa Kampeni ya Lengo la Tatu la Milenia: Kupunguza Vifo Vya Watoto wachanga na akina Mama Wajawazito. Mapema mwaka huu FemAct walikabidhiwa mwenge kama ishara ya kupewa jukumu la kuhakikisha utekelezaji wa Lengo la Tatu la Millenia.

Wawasilishaji wakuu walikuwa ni dada Jesca Mkuchu(Pichani) Mwenyekiti wa FemAct na Ussu Mallya- Mkurugenzi wa TGNP. Lengo la Mrejesho huu ni; kukabidhi mwenge kwa wanaharakati na kupata fursa ya kutandaa na kupashana habari zaidi juu ya utekelezaji wa lengo la namba tatu la malengo ya millenia.

Katika kufanya uchambuzi yakinifu wanaharakati walinabaini kuwa lengo hilo la millenia linakabiliwa na changamato kadhaa wa kadha baadhi ni kama zifuatazo: Lengo hilo lina ufinyu wa dira, kwa sababu halilengi kumkomboa mwanamke katika kila nyanja, pili Malengo haya hajatilia mkazo maazimio ya Beijing ya mwaka 1995, kwa sababu katika maazimio Kumi na mbili ya Beijing ni azimio moja tu ndio lililochukuliwa.

Wanaharakati waliangalia uwezekano wa serikali yetu kutimiza malengo hayo kabla ifikapo mwaka 2015 kama ilivyoahidiwa, na kujaribu kuangali ni kwa kiasi gani malengo hayo yamekamilishwa.

Dada Halima Mselem kutoka TAMWA aliangalia uwezo wa serikali katika kudhibiti unyanyasaji wa kijinsia na upatikanaji wa haki sawa katika elimu kati ya watoto wa kike na wakiume. Na alishauri pawepo na mpango maalumu wa serikali wa kutenga fedha kwa ajili ya kukomesha unyanyasaji wa kijinsia.

Dada Jonoveva Katto kutoka TAWALA, yeye aliangalia utekelezaji wa lengo la tatu hasa katika upande wa sheria, ambapo alitanabaisha vipengele kadhaa vya sheria ambavyo bado vinaendeleza ukandamizaji kwa wanawake. Sheria hizo ni zile za Mirathi, kwa mfano, sheria ya mirathi ya kimila ya mwaka 1963 hamruhusu mwanamke kurithi na kumiliki mali. Na sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kifungu cha 60, kinaeleza wazi kwamba mali zinazopatikana katika ndoa zinapaswa kuandikishwa kwa jina la mwanaume, sheria hii mara nyingi huleta msuguano hasa pale mwanaume anapoamua kuoa mke mwengine na kumfukuza mwanamke bila kumpa kitu chochote walichochuma wote.

Dada Festa Andrew kutoka UTU Mwanamke yeye aliongelea juu ya hali ya afya ya Uzazi ambapo alitabanaisha kwamba hali bado si nzuri nchini Tanzania ambapo kwa wastani kila baada ya lisaa limoja mwanamke mmoja mazazi anafariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi salama. Hivyo bado kuna haja ya wanaharakati kuendelea kuisisitiza serikali kuongeza fedha zaidi katika swala hili la afya ya uzazi, tofauti na ahadi za sasa za wanasiasa ambazo zinaendeleza kuleta madhara kwa wazazi.

Changamato kwa wanaharakati ni pamoja na kuishinikiza serikali ili iweze kuongeza nguvu na kutekeleza makubaliano ya lengo la tatu la milenia kama lilivyoafikiwa na wakuu wa maataifa 189. Kwa sasa bado serikali inasusua katika utekelezaji wa lengo hilo kutokana na kutoa kipaumbele kidogo katika sekta hiyo.

Je Wanaharakati wanaweza kufanya nini ili kuhakikisha kwamba lengo hili la tatu linafanikiwa kwa wakati husika? Je, takwimu zinazotolewa na maofisa wa serikali zina ukweli ndani yake? Nini kifanyike ili kuboresha kampeni hii ya utekelezaji wa lengo la tatu la millenia?

2 comments:

Anonymous said...

lengo hili la tatu la millenia linaweza lisifikiwe kwa sababu bado serikali yetu haijawa tayari katika kulitekeleza kwa vitendo badala yake imekuwa ikieleza kwa manaeno ya kisisa tu.

Anonymous said...

Mwanaharakati hatakiwi kukata tamaa, anachotakiwa ni kuendelea kuishinikiza serikali kutekeleza lengo la tatu la millenia
Ripoti zinazotolewa na viongozi hazina uhakika. Wengi wanatoa ripoti ili kusafisha jina la sekta yao tu na si uhalisia wa utendaji wao
By Eva