Thursday, October 16, 2008

Mrejesho wa Semina ya GDSS ya Jumatano ya tarehe 15/10/2008

Mada ilikuwa ni Uibuaji wa Maswala Makuu Yahusuyo Ukatili wa Jinsia Katika Jamii.
Semina hii ilihudhuriwa na wanaharakati kutoka katika vikundi mbalimbali ndani ya jiji la Dar es Salaam na waliweza kuibua maswala ambayo yanasababisha ukatili wa kijinsia ama aina nyingine ya ukatili dhidi ya utu na watu wanyonge. Baadhi ya Vikundi hivyo ni pamoja na; Chama cha Viziwi (CHAVITA), Albino Revolution Cultural Troupe, Mbagala Group, Tegeta Group, Kagera Youth, Mwananyamala group, Kisarawe IGN, Kinondoni IGN, Youth and Women Program (KWYP- Kigogo), Segerea Group, Kamene Sec. School, Makuburi Women Deveolpment Association (MWDA), Tabata Youth, na Magomeni Group. Washiriki wa semina waliweza kuibua maswala mbalimbali katika maeneo yao ambayo yanasababisha ukatili wa kijinsia katika jamii, baadhi ya maswala hayo ni;

Maswala yanayosababisha Ukatili wa Kijinsia katika jamii ni pamoja na; Wanawake kunyimwa haki ya kumiliki mali ndani ya jamii na familia ama baada ya kufiwa; ukosefu wa haki katika mirathi kwa kigezo cha jinsia; rushwa ya ngono katika ajira ama kupandishwa vyeo makazini; ubakaji katika ndoa; unyanyasaji wa wasichana wanaofanya kazi za ndani; wanawake kutekelezwa na wanaume baada ya kupata ujauzito au watoto wao waliojifungua; na Wazazi kuwaachisha shule watoto wa kike kwa ajili ya ajira au kuolewa.

Katika elimu maswala yafuatayo yaliibuliwa; adhabu kali kwa wanafunzi ambazo hazilingani na makosa; wanafunzi kurudishwa nyumbani kwa makosa madogo-madogo; Tuition inawanyanyapaa watoto maskini wasio na uwezo wa kulipia; Usafiri kwa wanafunzi ni kero kubwa inayowasababisha wanafunzi kutumbukia katika matatizo makubwa –mf. Mimba; Watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi mara nyingi hawachukuliwi hatua stahiki na serikali hii inachangia wanafunzi kuendele kupewa mimba kiholela; na Ubaguzi ndani ya familia dhidi ya mtoto wa kike katika kupata elimu na haki zingine.

Matatizo na kero za Walemavu; Unyanyasaji ndani ya jamii; Unyanyasaji ndani ya ndoa,hasahasa walemavu wanapoolewa na watu ambao hawana ulemavu; unyanyasaji ndani ya familia hasa kuachishwa shule na unyanyasaji mwengine; kutengwa katika maneo ya biashara; unyanyasaji katika elimu- ukosefu wa dhana za elimu; ukosefu wa wakalimani, hata katika taarifa Muhimu za kitaifa -mf. hotuba ya rais; Mauaji ya Albino, serikali imeshindwa kuwalinda albino; na Walimu kuwadharau Albino kwa uwezo wao wa kuona ni mdogo.

Kero za jumla zilizopo katika jamii ni pamoja na; ukosefu wa maji safi na salama; shida ya usafiri; serikali za mitaa kushindwa kukaa vikao vya maendeleo; Rushwa katika ofisi za serikali; kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya; ukosefu wa huduma za afya; upungufu wa vituo vya usalama; unyanyasaji wa mama ntilie; na kushamiri kwa mabanda yanayoonyesha video za uchi wakati wa mchana kwa watoto walio na umri mdogo.


Wanaharakati waliazimia mambo yafuatayo ya kutekeleza kutokana na kero walizozioanisha; Jamii ielimishwe ili iweze kutoa taarifa endapo vitendo vya unyanyasaji vinatokea katika maeneo yao; Walemavu kujiunga katika mitandao mbalimbali ya wanaharakati ili kuweza kupata na kutoa taarifa mbalimbali na Jamii ielimishwe ili iweze kuwa na mtazamo sawa juu ya watu wenye ulemavu; Wanaharakati wakusanye nguvu za pamoja katika kuleta Mabadaliko katika jamii zao; na vikundi vikusanye nguvu zaidi katika kupambana na ukatili wa kijinsia.

6 comments:

Anonymous said...

Kweli ipo haja ya wanaharakati kuungana na kupambana na hali zote za ukandamizaji zinazoendelea katika jamii yetu, kwa sababu jamii yenyewe ndiyo inatakiwa kubadilika na isisubiri serikali ama nguvu nyingine kutoka nje ije kuwabadailisha. mapambano yanaendelea!

Anonymous said...

wananchi wana kero nyingi sana zinazowagasi, na hakuna wa kuzitauta ila wao wenyewe. wananchi tuungane na tupambane hali hii ya ukandamizaji.
mdau

Anonymous said...

hongereni wanaharakati kwa kuibua mambo yanayowakera

Anonymous said...

Serikali haijafanya juhudi za kutosha kutatua kero za wananchi, wananachi wanapaswa kuiwajibisha serikali katika chaguzi zinakuja kwa kutowachagua viongozi ambao hawasikilizi matakwa ya wananchi.

Anonymous said...

ni kazi ya wananchi kuibua kero kama izi kwa faida ya vizazi vijavyo
mwanaharakati

Anonymous said...

ni kazi ya wananchi kuibua kero kama izi kwa faida ya vizazi vijavyo.
mwanaharakati