Thursday, October 9, 2008

Mrejesho wa Semina za GDSS

Mada: Changamoto Zilizopo Katika Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata na Ushiriki wa Wananchi Nchini..


Mada hii iliwakilishwa na Frank Samweli(Pichani) Mwanasheria wa Kujitegemea, jumatano ya tarehe 8/10/2008. Lengo la mada hii ni kuainisha changamoto zilizopo katika mchakato mzima wa uendeshaji wa mabaraza ya kata kwa kuangalia uundaji wake, muundo, utendaji wake wa kazi, ushiriki wa wananchi na Mapungufu yanayojitokeza katika uendeshaji wa mabaraza haya.

Mabaraza haya yalianzishwa kipindi cha ukoloni na baada ya uhuru yakaendelea kuwepo kwa lengo la kuamua kesi ndogo ndogo, kurahisisha mchakato wa kupata haki kwa wananchi, na kupunguza msongamano katika mahakama za wilaya. Mabaraza yanaundwa na sheria ya mabaraza ya kata namba 7 ya mwaka 1985, iliyorekebishwa katika sheria mpya sura ya 206 ya mwaka 2002.

Tangu yaliyoanzishwa tena, Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yamekuwa na mafanikio yafuatayo: kuleta hali ya utulivu na amani, kuleta upatanishi kati ya pande mbili zinazodaiana, kurahisisha upatikanji wa haki kwa wananchi, na kupunguza msongamano wa kesi katika mahakama za wilaya.

Matatizo ambayo yamejitokeza katika uendeshaji wa mabaraza haya ya kata ni pamoja na yafuatayo;
Hakuna mishahara rasmi kwa wajumbe wa baraza. Wajumbe wa baraza wanapata posho kutokana na vikao wanavyokaa na kesi wanazosuluhusha. Kukosekanana kwa posho kwa wajumbe kumesababisha mabaraza haya kupungua ubora wake katika utendaji wake wa kazi kwa kulazimisha kutoza faini ili wajumbe wapate posho.(Dada Talaka Nyanja akichangia hoja, yeye pia ni Mjumbe wa baraza la Usuluhishi la kata ya Mabibo)

• Wajumbe walio wengi hawana ujuzi na mambo ya sheria, hii inasababisha kesi nyingi kuamuliwa kwa utashi wa wajumbe waliopo katika baraza hilo na hivyo kuwanyima haki wale ambao waliopeleka mashitaka katika baraza.
• Mabaraza haya hayapo kila siku. Mabaraza ya kata yanakaa kwa wiki mara moja ama mara mbili kutokana na wajumbe kuwa na shughuli zingine za kuwaingizia kipato cha kujikimu kimaisha, hii imesababisha kesi nyingi kuamuliwa katika siku moja na hukumu kutolewa bila kusikiliza maelezo zaidi kutoka kwa walalamikiwa.

• Uteuzi wa Wajumbe wa Mabaraza haya mara nyingi huzingatia utashi wa
Kisiasa Kwa sababu wajumbe wanateuliwa na kamati ya Maendekleo ya kata ambayo inaongozwa na diwani kitu ambacho kinapelekea wajumbe hawa kuwa na utashi wa kisiasa. Pia wajumbe wa mabaraza haya huchaguliwa kwa kificho sana kitu ambacho kinaleta manung`unuko kwa wananchi na kukosa imani na maamuzi yanayotolewa na mabaza haya mara kwa mara. (Dada Harieth Kabende akichangia hoja juu ya usiri wa Uteuzi wa Wajumbe wa Mabaraza)

Wanaharakati bado wana nafasi ya kuhakikisha kwamba kasoro hizi ndogondogo zilizopo katika mabaraza haya zinarekebishwa ili kongeza tija katika utendaji wa mabaraza haya, kwani mabaraza haya yakitumiwa vizuri yanaweza kupunguza mzigo wa wananchi katika kutafuta haki zao katika mahakama za wilaya.

Je, wanaharakati wanafanya nini kuhakikisha mabaraza haya yanaboreshwa? Je, Hatua zipi zitumike katika Kuboresha utendaji kazi wa mabaraza haya?

3 comments:

Anonymous said...

jambo la kuangalia kusiwepo mazingira yarushwa ambayo yatasababisha mtu kukosa haki zake na pia wawepo watalaam wa aina mbali mbali kama madaktari kwa kesi kama ubakaji mtu anapo mpa mimba kwa mtu anayekataa ni rahisi kuthibitisha na pia watalaam wa ardhi kunapo tokea migogoro ya ardhi na pia wana sheria wasaidie kuamua kesi sawasawa navifungu vya sheria na posho zisikosekane na halimashauri zinazo husika
app

Anonymous said...

jambo la kuangalia kusiwepo mazingira yarushwa ambayo yatasababisha mtu kukosa haki zake na pia wawepo watalaam wa aina mbali mbali kama madaktari kwa kesi kama ubakaji mtu anapo mpa mimba kwa mtu anayekataa ni rahisi kuthibitisha na pia watalaam wa ardhi kunapo tokea migogoro ya ardhi na pia wana sheria wasaidie kuamua kesi sawasawa navifungu vya sheria na posho zisikosekane na halimashauri zinazo husika
app

Anonymous said...

katika mabaraza haya watu wamezidi kupeana madaraka kwa mtindo wa kichama zaidi matokeo yake sisi wengine tusiokuwa na vyama tunakosa imani na mabaraza haya kabisa. nadhani sasa wakati umefika kwa serikali kuangalia upya mtindo wa kupeana madaraka katika mabaraza haya ili yawe kweli kwa ajili ya kutoa haki kwa raia.