Thursday, September 29, 2011

Prof.WANGARI MAATHAI KUZIKWA KITAIFA


Rais wa Kenya Mwai Kibaki ametangaza siku mbili za maombelezo kufuatia kifo cha Profesa Wangari Maathai.

Kulingana na taarifa ya rais Kibaki iliyotumwa kutoka Ikulu, hayati Profesa Maathai atafanyiwa mazishi yenye hadhi ya kitaifa.

Pia ametangaza siku mbili za kuomboleza kifo cha mwanaharakati huyo wa kutetea haki za mazingira.

Kuanzia leo hadi Ijumaa bendera kote nchini Kenya zitapeperushwa nusu mlingoti.
Haya ndio yatakuwa mazishi ya kitaifa ya tatu kufanywa tangu Kenya ipate uhuru mwaka 1963.

Mazishi ya kwanza yalifanyika mwaka 1978 baada ya kifo cha rais mwanzilishi wa Kenya Jomo Kenyatta na mara ya pili ni baada ya kifo cha makamu wa rais Michael Kijana Wamalwa.

Tofauti na viongozi hawa Profesa Maathai hakuwa kiongozi wa serikali wakati wa kifo chake.
Awali taarifa kutoka familia ya mwanaharakati huyo ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza mwafrika kushinda tuzo ya amani ya Nobel, ilisema bado wanajadiliana kuhusu siku ya maziko na eneo gani.

Profesa Maathai alifariki Jumapili usiku baada ya kuugua saratani ya uzazi.
Viongozi wamekuwa wakituma salamu zao za rambirambi kutoka pembe zote duniani.

Wednesday, September 28, 2011

Wasioona wapewa nakala 1,500 za Katiba

WIZARA ya Katiba na Sheria imeikabidhi asasi ya Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu (SWAUTI), nakala 1,500 za Katiba zilizochapwa kwa maandishi ya nukta nundu ili washiriki kikamilifu katika mchakato wa Katiba mpya.

Akizungumza wakati wa kukabidhi nakala hizo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Oliver Mhaiki alisema lengo la kutengeza nakala hizo zenye thamani ya Sh milioni 32 ni kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu ya Katiba.

Mhaiki alisema upatikanaji wa Katiba kwa makundi yote ni muhimu kwa kuwa Katiba ndiyo sheria mama hivyo wananchi wanatakiwa kuifahamu na kuielewa ili washiriki kikamilifu katika kuandaa Katiba mpya baada ya miaka 50 ya Uhuru.

“Katiba hii imechapwa na Kampuni ya Edpar Corporation na gharama ya kutengeneza nakala moja ya Katiba kwa maandishi ya nukta nundu ni Sh 21,000 wakati kwa maandishi ya kawaida ni Sh 3,500, hii ni gharama kubwa ni lazima mzitunze ili ziwanufaishe na wengine,” alisema Katibu Mkuu Mhaiki.

Katibu wa Swauta, Stella Jailos aliishukuru Serikali kwa kupata Katiba hiyo ambayo hawaifahamu toka miaka 50 ya Uhuru na kuwaomba wasiishie hapo, bali wawakumbuke hata katika Katiba mpya.

Alisema, Katiba hiyo itawasaidia kushiriki katika kuandikwa kwa Katiba mpya kwa kuwa wasingeweza kutoa mapendekezo wakati yaliyoandikwa nyuma hawayafahamu na kuahidi kuwa watazisambaza nchini kupitia katika matawi ya asasi yao.

Alisema, kuna baadhi ya sheria zinazowahusu kama wananchi, lakini hawazifahamu na kuiomba Serikali kuzichapa katika maandishi hayo ili wazifahamu ambapo Katibu Mhaiki aliahidi kulishughulikia.

Mwenyekiti wa Swauti, Modesta Mpelembwa alivitaka vyombo vya habari kuweka wakalimani hasa wakati wa shughuli za Bunge zikiendelea ili wapate haki yao ya kupata habari na kuelewa nini kinachoendelea.

Tuesday, September 27, 2011

‘Katiba iwe ya Kitanzania’

JAJI Mkuu Mohamed Othman Chande, amesema mabadiliko ya Katiba yatakayofanyika nchini yasiwe ya kuiga kutoka nchi nyingine bali yawe ya Watanzania wenyewe.

Jaji Chande alisema hayo Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kufungua jengo jipya la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) cha Jaji Mwalusanya uliokwenda sambamba na sherehe za miaka 16 ya LHRC.

Alisema “haki za binadamu si za kijamii tu au kisiasa, bali zinalenga kwa watu wote kuwa na haki ya kupata kazi, nyumba ... kuna nchi kama Kenya na Afrika Kusini zimefanya
mabadiliko ya Katiba, hivyo kama sisi tunafanya mabadiliko tuangalie wananchi wetu na si tuige katiba za wenzetu”.

Alisema pamoja na kwamba ni kweli Katiba iliyopo ina upungufu, marekebisho yanatakiwa waachiwe Watanzania wenyewe kwa faida yao.

Akizungumzia adhabu ya kifo Jaji Mkuu alisema adhabu hiyo inakiuka Katiba na katika mchakato wa marekebisho, suala hilo litaangaliwa.

“Utafiti unaonesha kwamba kila mwaka nchi mbili au tatu zinafuta adhabu ya kifo, na Tanzania ni nchi ambayo adhabu hiyo haitekelezwi, kwa sababu inaathiri haki za binadamu na msimamo wa Umoja wa Mataifa unaosisitiza nchi zote kufuta adhabu hiyo,” alisema.

Kuhusu kesi za uchaguzi, alisema tayari mahakama zimeanza kuzisikiliza zaidi ya 20 katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kilwa na Arusha Mjini.

Aidha, alitaka wananchi waelimishwe zaidi kuhusu sheria ili wafahamu haki zao na kuitaka Serikali kukamilisha sera ya kutoa msaada wa kisheria haraka ili kusaidia wasiojiweza wapate haki zao.

Pia alisema kwa kutambua mchango wa kituo hicho, mahakama imeahidi ushirikiano wa hali ya juu katika utoaji haki.

Mwenyekiti wa Bodi ya LHRC, Askofu Elinaza Sendoro, alisema kituo hicho kimekuwa
kikitoa msaada wa sheria kwa wasio na uwezo ambapo katika kesi wanazopokea nyingi ni mashauri ya ndoa na viwanja (migogoro ya ardhi).

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Francis Kiwanga, alisema ardhi inayofaa kwa kilimo inaweza kutoweka kutokana na kutolindwa na kugawanywa bila mpangilio maalumu.

“Wapo wajanja wachache kwa kutumia viongozi walio serikalini, wanawadanganya wananchi na kuwapora ardhi, hivyo ukiwapo uwezeshaji wa sheria, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ardhi nchini,” alisema.

Alisema bado suala la utawala wa ardhi halijapangwa vizuri, hivyo upo umuhimu wa kuwajengea wananchi uwezo wa kufahamu haki za ardhi ili wazilinde.

Monday, September 26, 2011

Profesa Wangari Maathai afariki dunia

Mtunukiwa wa tuzo ya Amani ya Nobel Prof Wangari Maathai ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 71.

Mwanaharakati huyo mashuhuri wa mazingira na haki za binadamu wa Kenya Profesa Wangari Maathai amefariki dunia mjini Nairobi usiku wa kuamkia , Jumatatu kutokana na maradhi ya saratani.

Prof Karanja Njoroge ambaye ni mkurugenzi wa Green Belt Movement, shirika ambalo Prof Maathai alilianzisha amethibitisha kifo hicho.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Prof Njoroge amesema wakati wa kifo chake Wangari alikuwa na wanafamilia na marafiki.
Profesa Wangari Maathai alipata tuzo la amani ya Nobel mwaka 2004, kufuatia juhudi za kupigania uhifadhi wa mazingira nchini Kenya.

Mbali ya kuwa Mwanaharakati wa Maswala ya Mazingira na haki za binadamu , Wangari Maathai pia alikuwa mwanasiasa shupavu. Amewahi kuhudumu kama Mbunge na Naibu waziri wa Mazingira nchini Kenya.
Prof Maathai pia katika uhai wake alipata tuzo mbalimbali za kimataifa kwa kutambua mchango wake.Prof. Wangari Muta Maathai alianzisha vuguvugu la Green Belt mnamo mwaka 1977, ambapo alifanya kazi na wanawake kote nchini kuboresha maslahi yao na kuhifadhi mazingira.

Alikuwa mtetezi mashuhuri wa matumizi bora ya mali asili . Shughuli zake zilitambuliwa mara kwa mara kote duniani.Marehemu ameacha watoto watatu, wawili wakiume na mmoja wa kike.

Friday, September 23, 2011

BP yauzwa kwa Puma

KAMPUNI ya Mafuta ya BP Tanzania Limited, imewaomba radhi Watanzania na Serikali kutokana na kufanya mgomo wa kutoa huduma ya mafuta ikipinga fomula mpya iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

BP iligoma kuuza bidhaa yake kwa kutumia fomula hiyo takriban mwezi mmoja uliopita kwa madai kuwa ingekuwa inauza chini ya gharama halisi na hivyo kupata hasara kubwa.

Kutokana na hatua hiyo, Ewura iliifungia leseni na hivyo isijihusishe na biashara hiyo kwa miezi mitatu.

Uamuzi ambao haukukubaliwa na BP hivyo ikaamua kukata rufaa Mahakama ya Ushindani Kibiashara (FTC).

Mkurugenzi Mkuu wa BP Tanzania, Engelhardt Kongoro, amesema kuwa wakati EWURA inachukua uamuzi wa kuifungia kampuni hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ilikuwa inashauriana na wanahisa wa kampuni hiyo, kuomba ruhusa ya kama wauze mafuta hayo kwa bei ya hasara au la.

“Tulifanya hivyo, kwa vile Bodi haina mamlaka ya kuuza bidhaa zake kwa bei ya chini hadi inapopata ruhusa kutoka kwa wanahisa,” alisema Kongoro.

Wanahisa wa kampuni hiyo ni Serikali ya Tanzania na Kampuni ya BP ya Uingereza. Kongoro alisema baada ya kuchelewa kupata ruhusa kutoka kwa wanahisa, hawakutekeleza agizo la Ewura, hali ambayo ilifanya ifungiwe kuuza bidhaa zake Agosti 12.

Kampuni ya BP kwa sasa imeuzwa kwa Puma Energy Tanzania Investiment Limited, ambayo imeonesha kusikitishwa na hatua zilizochukuliwa na wawekezaji hao wa zamani, ambazo ni wazi kuwa zilikiuka sheria na taratibu za nchi.

“Kwa hali hiyo, BP Tanzania inapenda kuwaomba radhi Serikali ya Tanzania, Ewura, Watanzania na wateja wetu kwa jumla, kwa usumbufu uliojitokeza wakati tuliposimamisha huduma zetu,” alisema Kongoro.

Mkurugenzi huyo alisema kutokana na uamuzi huo wa kuomba radhi, BP Tanzania
imewaagiza wanasheria wake kufuta kesi zote mbili ilizofungua FCT.

Kongoro alisema wakirejeshewa leseni yao, wawekezaji wapya; Puma Energy, itaendelea na biashara ya mafuta kama kawaida na itauza bidhaa hiyo kwa bei ya Serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema Bodi ya Ewura itairejeshea leseni kampuni hiyo itakapotimiza masharti.

Moja ni kuwaambia wananchi kwa nini waligoma kuuza mafuta, kuomba radhi kwa wananchi, kufuta kesi na kulipa gharama za kesi hiyo.

Wakati huo huo, BP Tanzania imetangaza rasmi kuuzwa kwa kampuni hiyo kwa Puma Energy kuanzia mwezi huu.

Kwa hatua hiyo, Puma itamiliki asilimia 50 ya hisa na Serikali kiasi hicho hicho.

Novemba Puma na BP Afrika zilikamilisha taratibu za kuuzwa kwa hisa za BP katika nchi tano zilizo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania.

Kwa hali hiyo, baada ya taratibu kukamilika, Puma ndiyo itakuwa inaongoza menejimenti ya BP wakati taratibu za makabidhiano zikiendelea kufanywa katika ngazi mbalimbali.

Kampeni za ubunge Igunga sasa na Bastola


Aden Rage akimnadi mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM huko Igunga

Thursday, September 22, 2011

Askofu Kilaini aonya ushoga katika Katiba

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini ameonya Taifa kutokukubali kuingiza suala la ushoga katika Katiba mpya kwa kuwa kufanya hivyo ni kuliingiza taifa katika laana ya Sodoma na Gomora.

Amesema huo ni ugonjwa unaohitaji tiba na si kuubeba kama kitu cha kawaida kwa kuwa bila kuutibu, Watanzania wengi wataugua na kumalizika kabisa hasa watoto na vijana.

Askofu Kilaini aliyewahi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam alipotakiwa kuzungumza kwa nafasi ya kiongozi wa dini na waandishi wa habari nje ya Kongamano la Maaskofu la siku mbili linalojadili masuala ya Katiba na Utawala Bora.

Kongamano hilo limeandaliwa na Kikundi cha Mazungumzo cha Umoja wa Makanisa (TEDG) ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa kushirikiana na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC).

“Katika hilo hakuna kukwepa kuwa huo ni ugonjwa na ugonjwa unatafutiwa dawa si kuubeba, ushoga si maumbile ya kawaida ya binadamu, bali ni ugonjwa, Taifa lazima liwe macho katika hili, tuliweke taifa katika laana ya Sodoma na Gomora (miji iliyoangamizwa na Mungu kutokana na kukithiri kwa matendo maovu), “ alisema Askofu Kilaini.

Alisema ikiwa watatambulika na kutokea kupewa kulea yatima watakapofunga ndoa, mtoto atamuita nani baba au mama kati yao, hivyo tatizo litakuwa kubwa zaidi kuliko inavyofikiriwa jambo analoamini ni nguvu ya mataifa tajiri kuharibu vizazi vya Watanzania.

Alisema jambo hili si la kawaida kama linavyotaka kufanywa, bali linatakiwa kutafutiwa dawa ili liishe na si kulilea kwa kuwa ni ugonjwa unaoambukiza.

“Hili si suala la dini tu bali ni suala la ubinadamu, waliokwisha kuingia wanapaswa kusaidiwa kutoka, si rahisi kurejea hali ya kawaida lakini wanaweza kuwa wanaume wazuri pia,” alisema askofu huyo maarufu.

Alipendekeza wasizuiwe kutoa maoni wakati wa mchakato wa Katiba mpya kwa kuwa ni Watanzania, lakini si kuingizwa na kutambuliwa na Katiba na kushauri elimu na ushauri iwe njia ya kuwasaidia huku wazazi wakihakikisha wanakuwa wazi kuzungumza na watoto wao kuhusu ubaya wa suala hilo.

Hivi karibuni katika Tamasha la 10 la Jinsia, mashoga zaidi ya 20 kutoka Zanzibar na Dar es Salaam walihudhuria na katika kuchangia mada, walitaka waruhusiwe kutoa maoni wakati wa mchakato wa Katiba mpya na iwatambue ili wapate ulinzi wa kikatiba.

Friday, September 9, 2011

Chadema yazindua kampeni, Mkapa atua Igunga

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezindua kampeni zake za kuwania Jimbo la Igunga huku Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, akiwataka wananchi kumchagua mgombea wa chama hicho, Joseph Kashindye ili alinde rasilimali za wana Igunga.

Wakati Chadema wakizindua kampeni hizo kwa mtindo wa kumwaga tuhuma na kashfa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Rais wa Awamu ya Tatu, alitua Igunga tayari kwa uzinduzi wa kampeni za chama hicho na kuelezea furaha aliyonayo ya kusafiri kwa lami kutoka Dar es Salaam hadi Igunga.

Katika uzinduzi wa Chadema, Dk. Slaa aliwataka wananchi waliokuwa wamefurika katika Uwanja wa Sokoine mjini hapa, kumchagua Kashindye ili alinde rasilimali hizo na kupunguza aliowaita panya wanaozitafuna.

Alidai kuwa mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu, hawezi kuleta mabadiliko yoyote Igunga na kwa Taifa kutokana na alichoita kuwepo kwa mfumo mbovu wa CCM katika kusimamia maslahi ya wananchi.

Dk. Slaa alisema kuwa nchi inahitaji kutetewa na makamanda, ili ifanikiwe kwa kuwa CCM imeshindwa kazi ya kuwasaidia wananchi.

Aliwaambia polisi aliowaita wanaoagizwa kuwapiga mabomu wananchi, wasifanye hivyo kwa kuwa kazi ya Chadema, ni kuwatetea polisi wa vyeo vya chini ambao alidai wanapewa posho ndogo isiyokidhi mahitaji yao.

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kazi hivyo haifai kuwa madarakani wala kuongezewa wabunge kwa kuwa itazidi kuwadidimiza wananchi.

Kwa upande wake Kashindye alijinadi mbele ya wananchi hao kuwa wakiona mwalimu anaachia chaki na kwenda kwenye siasa, basi wajue hali ni mbaya kwa kuwa Taifa linahitaji ukombozi.

“Hata Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Mwalimu Julius), aliachia chaki alipoona hali ni mbaya na akaamua kuingia kwenye siasa na kuikomboa Tanzania tunayoishi leo,” alisema.

Alidai kuwa CCM wanadhani kuwa watumishi wa Serikali ni mali yao kitu ambacho si kweli na ameamua kuingia Chadema ili awatetee wananchi wa Igunga na Taifa kwa ujumla.

“CCM ni chama kinachokufa nisingeweza kuondoka na kuingia CCM kuwa mbunge wa kusinzia kwa kuwa hawana hoja,” alidai.

Alidai kuwa fedha nyingi za kujenga barabara zimeliwa kitu ambacho kimesababisha wananchi kuteseka kutokana na mfumo mbovu wa CCM.

“Nawaombeni mnitume niende huko bungeni niende nikawe Spika ya Igunga; nikaseme yote na tupate mafanikio wote,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Susan Kiwanga alisema ni lazima Igunga wahakikishe chama hicho kinashinda kwa kumchagua Kashindye ili awatetee bungeni.

Alisema, ataweka kambi Igunga na kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kuwa Chadema ni chama cha kutetea wanyonge ambao wamekuwa wakinyonywa na CCM kwa miaka nenda rudi.

Mkapa atua Igunga Lakini Mkapa baada ya kutua Igunga, aliweka bayana kuwa amefika kupambana na kumnadi mgombea wa CCM kwa kuwa anajisikia faraja na matunda ya CCM yakiwemo kutembelea barabara ya lami kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza.

Akiwahutubia wananchi katika Kitongoji cha Makomero alisema kuwa ni muhimu kwa wana Igunga kupuuza vyama vingine kwa kuwa CCM ikitoa ahadi, inatimiza na viongozi wake ni makini.

“Kazi yetu ni moja tu, kila mtu ahakikishe Dk. Kafumu anashinda na kila mtu ambaye amejiandikisha aende kupiga kura ili mambo yawe poa,” alisema Mkapa.

Wanafamilia watakiwa kuboresha mahusiano ya kumiliki mali

Na Juma Nyumayo, Dar es Salaam

KUTOKANA na migogoro mingi inayoibuka katika ngazi ya kaya na familia hapa nchini kutokana na kuwa na mahusiano mabaya katika kuzalisha na kumiliki mali, familia hizo zimetakiwa kujenga na kuboresha mahusiano yao kwa kufuata vigezo vya uwazi na upendo hatua kwa hatua kabla mali wanazozalisha hazijawatesa kwa kuwagombanisha kwa kile kinachodaiwa nani mmiliki halali kati ya mwanamke na mwanamume.

Hilo ni moja ya azimio lililofikiwa na washiriki wa warsha ya Uchumi na Ukombozi wa mwanamke kimapinduzi inayoendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Jinsia cha TGNP katika Ukumbi wa kitivo cha Uhandisi Chuo Kikuu cha dar es Salaam.

Katika hali ya kubaini tatizo kuu la wanandoa pia familia nyingi kusambaratika kutokana na migogoro ya nani amiliki mali, au kurithi wanawarsha hao wamechambua mbinu mbalimbali na kuja na mapendekezo ambayo huenda yakapunguza tatizo linalozikabili familia nyingi hapa nchini hasa kutokana na mfumo dume unamtenga mwanamke kumiliki mali hasa zenye thamani.

Sheikh wa wilaya ya Liwale, Adam Mpelengana, alisema ni muhimu kwa wanaume wote kutambua kuwa wanawake ni wasaidizi wa mwanamume na ni jukumu la mwanamume kumpenda na kufanyia haki anazostahili badala ya kumuachia kazi nyingi bila usaidizi.

"Mwanamke anatakiwa aenziwe apendwe kwa kila namna, haifai kuendekeza mila na desturi za kumtumikisha mwanamke,' alisisitiza Sheikh Mpelengana.
Awali Mchungaji wa KKT toka Shinyanga, Odorus Gyunda , alisema ni muhimu kubainisha wazi ukatili wanaofanyiwa wanawake ni kinyume cha mapenzi ya mungu.

"imeelezwa wazi kuwa Mwanaume ampende mke wake na mwanamke amtii mumewe," alisema na kubainisha kuwa hayo hayawezekani kama hakuna upendo na mawasiliano mema katika uzalishaji na taratibu zote za kuishi.

Hata hivyo wanawarsha hao wamependekeza kuwa ili kusiwe na migogoro katika matumizi ya fedha na umiliki wa mali ni vyema wenza wakashiriki kikamilifu maamuzi ya kupanga utafutaji wa fedha au mali hatua kwa hatua mapema.

jambo jingine lililoelezwa ni wanawake na wanaume kwenye kaya zinazotegemea kilimo wajue mahitaji yao ya chakula mapema wakati wa kuandaa mashamba ili wasije uza chakula chote kwa tamaa ya fedha.
Wakijadili suala la kudhibiti matumizi na kuweka kumbukumbu za mapato katika ngazi ya kaya washiriki hao wamependekeza kuwe na daftari la pamoja la kuwekea kumbukumbu za mapato na matumizi katika kila hatua.

Aidha wamewaasa wanawake kuwa makini na mchango wa nguvu kazi zao katika kuhudumia familia pia kuzalisha mali katika kaya na kuhoji matumizi na shughuli za kila mmoja katika kaya husika.

Vilevile imeelezwa wazi kuwa usafi na kujali afya za wanafamilia ni mtaji mkubwa katika kuleta mahusiano mema katika kutumia muda na kumiliki mali za kaya.

Washiriki hao hawakuishia hapo, walisema hayo yatawezekana iwapo, kutatengwa walao siku moja katika wiki kuzungumzia masuala na maendeleo ya kaya husika kwa kuwahusisha mume, mke na watoto ili kaya ziendeshwe kwa shughuli na bajeti zenye mtazamo wa kijinsia zaidi.

Thursday, September 8, 2011

WALALAMIKIA MIGOGORO YA ARDHI KUKWAMISHA MAENDELEO

Na Juma Nyumayo, Dar es Salaam

MIGOGORO ya Ardhi inayoendelea katika mikoa mbalmbali hapa nchini imetajwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya wanawake katika harakati zao za kujikwamua kiuchumi pia kuleta ukombozi wa mwanamke na maendeleo stahiki hapa nchini.

Hayo yameibuliwa na washiriki wa warsha inayoendelea katika Ukumbbi wa Kitivo cha Uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa uwasilishaji wa mifumo na vikwazo vinavyozuia wanawake kujikwamua kiuchumi.

Akiwasilisha Mada hiyo, Mwezeshaji toka TGNP, Rehema Mwateba alisema ni vyema washiriki wakaeleza hali halisi ya umiliki wa ardhi na migogoro inayendelea kujitokeza hivi sasa ikilinganishwa na mifumo iliyopo katika kumkomboa mwanamke kimapinduzi.

Mshiriki mmojawapo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro,Kibena Kingo, ametolea mfano wa mapigano yanayoibuka marakwa mara na yanayoendelea wilayani kwake kati ya wafugaji na wakulima, ambapo chanzo kikiwa ni matumizi ya Ardhi na kwamba mgogoro huo ni mkubwa.

Imeelezwa wafugaji hao wanaotokea mikoa ya kaskazini na kati wanalishia wanyama wao mazao ya wakulima bila kujali na hivyo kuwakwaza wananchi wewnyeji ambao wengi wao ni wakulima wa mazao ya chakula.

"Mgogoro wa ardhi ni mkubwa na waathirika wakubwa ni wanawake na watoto, hata hivyo ni lazima hatua zichukuliwe ili kutatua migogoro hii kabla hayajatokea mauaji makubwa," alishauri Kingo.

Wakati kingo akielezea mgogoro wa ardhi Morogoro bado Mwezeshaji toka TGNP Darus Badi alipaza sauti yake na kuthibitisha kuwa mtandao huo una rekodi ya migogoro ipatayo 60 ya ardhi katika mkoa huo na kwamba kuna haja ya kulichukulia uzito tatizo hilo.

" Tuna migogoro tunayoijua kule Morogoro na tukiwa kama wanaharakati lazima tushirikiane kuchukua hatua," alisema Badi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa halamashauri ya Mbinga Prisca haule alisema migogoro mingi ya ardhi huko Mbinga imeibuka kutokana na wakazi wa huko kutafuta maeneo ya kulima baada ya kuishiwa ardhi maeneo ya milimani.

"Kuna migogoro ya ardhi katika familia na nje ya familia kupigania ardhi ya kulima," alisema na kubainisha kuwa bado kuna mipango mibovu na sera isiyoeleweka katika umiliki wa ardhi.

Hata hivyo lawama azikuachwa kwa wawekezaji katika vitalu vya mbuga za wanyama hadi migodi ya madini kama ya Buzwagi, Geita hadi huko Namtumbo kwenye Urani( Uranium) ambako wananchi wa kawaida na hasa wanawake wanaona kama mchezo wa kuigiza wasijue kinachoendelea kwenye ardhi yao.

Lawama kibao zimeelekezwa pia kwa Mamlaka za vijiji na Miji kugawa ardhi kwa upendeleo na hasa kwa wale wanaotoa kitu kidogo kwaajili ya kupata viwanja vya makazi na kuwaacha kabisa wanawake nyuma.

Wakati wa Ufunguzi wa warsha hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia ya TGNP, Dkt. Diana Mwiru, aliwaasa washiriki kujadili mada mbalimbali kwa lengo la kujenga uelewa na kusaidi jamii tunapoelekea kusherehekea tamasha la Jinsia na Mika 50 tangu Tanganyika kupata Uhuru wake.

Dkt. Mwiru,alisema, katika miaka 50 iliyopita wanawake wa nchi hii wameendelea kuachwa nyuma katika kumiliki na utoaji wa maamuzi juu ya rasilimali ikiwa ni pamoja na ardhi.

Wednesday, September 7, 2011

WANAWAKE nchini wameshauriwa kuziangalia changamoto juu a uelewa wa masuala ya uchumi na ukombozi wa Wanawake

Na Juma Nyumayo, Dar es Salaam

WANAWAKE nchini wameshauriwa kuziangalia changamoto juu a uelewa wa masuala ya uchumi na ukombozi wa wanawake baada ya miaka 50 toka uhuru ambapo wanawake wengi waeachwa nyuma kielimu na kiuchumi.
Hayo yameelezwa leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia ya TGNP, Diana Mwiru, wakati wa Ufunguzi wa Warsha ya Uelewa wa Masuala ya uchumi na wanawake yanayoshirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani toka mikoa yote ya Tanzaia Bara.

Mwiru, amesema, katika miaka 50 iliyopita wanawake wa nchi hii wameendelea kuachwa nyuma katika kumiliki na utoaji wa maamuzi juu ya rasilimali.

Mkuu huyo, amebainisha kuwa wakati umefika hivi sasa kwa jamii ya kitanzania kuhakikisha maisha bora kwa kila mtanzania yaapatikana kwa kuwashirikisha watu wote kutafuta na kutumia rasilimali za taifa.
Aemesema ni muhimu wa serikali zetu kuhakikisha wananchi hasa wanawake wanashiriki katika mchakato wa bajeti na iwe na mtazamo wa kijinsia.ngi wao ni viongozi wa Dini, waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa asasi zisizo za iserikali waandishi wa Haari na wanaharakati wanawajibu wa kuhakikisha uchumi na ukomboziwa mwanamke kimapinduzi unakwenda sambama na elimuya mtoto wa kike.
Mwateba amesema mia na desturi ambazo ni vikwazo katika ukombozi huo a faa zibainishwe wazi na kwama zijengwe nguvu za pamoja katika kutetea haki za uchumi.

Katika hali nyingine washiriki wawarsha hiyo wameeleza kwa kuna mabadiliko mengi yanajitokeza hivi sasa na kwamba baadhi ya Sera na kanuni zinawakandamza wanawake katika harakati za kumkomboa
Prisca Haule, Mheshimiwa Diwani Viti Maalum halmashauri ya Mbinga alisema inashangaza kuona Diwani wa Viti maalum hana nafas kugombea uongozi wa juu kama Uenyekiti wa Halmashauri au Umeya wa Manispaa.
"Hizi sera zinatunyanasa na kutuweka nyuma a kuwa wanyonge, alisema Haule.
Kauli hiyo iliungwa Mkono na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini Kibena Kingo kuwa hata wabunge viti Maalumu nao hawawezi kuteuliwa kupata nafasi ya Uspika au Uwaziri Mkuu.
"Hawawezi kupata nafasi kama hizo hivyo ukombozi wa mwanamke unavikwazo vingi," alisema Kingo.

Wakati vikwaz hivyo vikibainishwa, Diwani Anna Lyimo kutoka Halmashauri ya Moshi amewalalamikia wanaume wa Moshi kuwaingilia wanawake katika zao lao la Ndizi ambalo kimsingi ni zao la chakula na likimilikiwa na wanawake.
Lyimo alisema kuingiliwa huko kumetokana na kuanguka kwa zao la Kahawa na kitendo hicho kinaibua mgogoro wa kimaslahi ya kiuchumi.

Mafunzo hayo ya siku tano yanaendelea katika Ukumbi wa Kitivo cha Uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo washiriki wanategemewa kujenga uelewa wa masuala ya uchumi na ukombozi wa waawake kimapinduzi na kuwaelewesha watoa maauzi katika maeno yao wanayotoka.

Marufuku sukari sasa kuuzwa nje

SERIKALI imesimamisha leseni na vibali vyote vya uuzaji wa sukari nje ya nchi na kusimamia mipaka ili kudhibiti upitishwaji holela wa bidhaa hiyo.

“Kuanzia sasa mfanyabiashara atakayekamatwa amehodhi bidhaa hiyo kwa ajili ya kulangua au kuuza nje ya nchi kinyume na maagizo ya Serikali, ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria na adhabu ni faini ya Sh milioni 30 au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote,”
amesema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mohammed Muya.

Hata hivyo akizungumza jana na waandishi wa habari kuhusu matatizo ya kupanda kwa bei ya sukari nchini, Muya alisema hatua hiyo inachukuliwa ingawa upo ugumu kutokana na mazingira ya soko la pamoja la Afrika Mashariki.

Lakini pia alisema Serikali imeamua kutoa leseni kwa wingi kwa wafanyabiashara wa sukari kuingiza bidhaa hiyo kwa wingi kutoka nje ya nchi, huku Serikali nayo ikiagiza tani 120,000 za bidhaa hiyo kwa lengo la kukabiliana na upungufu uliopo.

Alisema kiasi hicho cha sukari kinajumuisha tani 20,000 zilizoingizwa kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na tani 100,000 zilizobaki zitaagizwa kutoka kwingine.

Halikadhalika kwa upande wa hatua za muda mrefu za kudhibiti upungufu wa sukari nchini, Serikali inapitia maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa na kwa kushirikiana na Bodi ya Sukari nchini, itahakikisha hatua zinachukuliwa ili kupata wawekezaji katika eneo hilo.

Hata hivyo, Muya alisema kiwango cha uzalishaji sukari nchini kinatosheleza mahitaji, lakini tatizo kubwa ni bidhaa hiyo kuuzwa kwa magendo Kenya na Uganda.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa hatua za kudhibiti hali hiyo alizozitangaza jana ulianza mara moja.

Muya alisema tathmini iliyofanywa na wizara yake, ilibaini kuwa bei ya sukari Uganda na Kenya iko juu ikilinganishwa na bei ya bidhaa hiyo nchini.

Alisema Kenya sukari inauzwa Sh 4,000 za Tanzania kwa kilo na Uganda ni Sh 3,500 hali inayosababisha wafanyabiashara wengi nchini kuivusha kimagendo na kuiuza katika nchi hizo.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, hali ya sasa ya upatikanaji wa sukari nchini si nzuri kwa kuwa imepungua na kusababisha bei kupanda kutoka bei elekezi ya Sh 1,700 iliyokubaliwa na wadau katika kikao kilichosimamiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
Machi.

Alisema pamoja na hayo pia imefahamika sukari katika soko la dunia inauzwa kwa dola kati ya 700 na 900 za Marekani kwa tani na ikiingizwa nchini bila kodi bei yake inafikia Sh 1,300 kwa kilo.

Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania, Mathew Kombe, alisema kiasi cha sukari kilichozalishwa nchini mwaka huu ni tani 306,000 ambacho ni sawa na kilichozalishwa mwaka jana. “Kwa sasa kila kiwanda kinazalisha tani 44,000 wakati mahitaji ya nchi ni tani
31,000.”

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, Ashwin Rana, alisema uzalishaji wa bidhaa hiyo unaendelea kama kawaida na hakuna upungufu, tatizo ni uuzwaji kwa magendo nje ya nchi na kuitaka Serikali idhibiti tatizo hilo na si kuagiza sukari zaidi kutoka nje.

Viwanda vingine vinavyozalisha sukari pamoja na Kagera, ni Mtibwa, Kilombero na TPC, ambavyo vyote vilianza uzalishaji wa bidhaa hiyo Juni hadi Agosti mwaka huu.

Tuesday, September 6, 2011

Makongoro Nyerere Aapa Kuwaning'iniza Mafisadi CCM


MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere ametangaza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho(Nec), kuhoji sababu za watuhumiwa wa ufisadi kushindwa kujiuzulu hadi sasa huku akimtaka Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuachana na watuhumiwa hao.

Msimamo huo wa Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere unakuja kipindi ambacho kikao cha Nec ya CCM kinatarajiwa kufanyika mwezi huu baada ya kile cha Kamati Kuu (CC) kilichoketi Mjini Dodoma mwezi uliopita kutoa muda zaidi kwa watuhumiwa hao kujipima hadi mkutano huo wa Nec.

Akifungua mkutano maalumu wa Nec ya CCM wilayani Bunda, Makongoro alisema kilichopo sasa ni kama mchezo wa kuigiza ambao hauingii akilini, hivyo akasema ni vyema akawasilisha hoja kwenye kikao hicho kuhoji uhalali wa watuhumiwa hao kuendelea kubaki na nyadhifa zao ndani ya chama.

Uamuzi wa kuwataka watuhumiwa hao kujivua gamba uliamuliwa na Nec iliyoketi mjini Dodoma Aprili, ambako pia CC iliyokuwapo ilijiuzulu na kuundwa upya huku Sekretarieti iliyokuwa chini ya Katibu Mkuu, Yusuph Makamba ikivunjwa na kuundwa upya kama mwanzo wa kujenga mwelekeo mpya wa chama.

Tangu wakati huo, mpango wa kujivua gamba umekuwa ukipigwa danadana kwani awali, ilielezwa kwamba watuhumiwa walipewa siku 90 baada ya kutakiwa kupima tuhuma dhidi yao lakini baadaye CCM ikakanusha na hadi sasa wengi wao wanaendelea na nyadhifa zao.

Makongoro akizungumzia zaidi danadana hizo, alisema huenda kinachowatia kiburi kugoma kung'oka kwenye nyadhifa zao ni uhusiano wa karibu walionayo na Rais Kikwete.

Alimtaka Kikwete kuachana nao na kusimamia kikamilifu uamuzi uliofikiwa na CC ili kukijengea heshima chama hicho.
Alisema kutowajibika kwa wanachama hao kunakitia doa chama hicho mbele ya jamii ambayo imekuwa ikikiamini kutokana na historia yake ya uadilifu.

“Nasema mbele yenu; sifurahishwi na watuhumiwa hao kuendelea kubakia ndani ya chama. Nitawasilisha hoja mbele ya kikao cha halmashauri kuu kuhoji kwa nini bado wamo huku wakikichafua chama?”

Makongoro ambaye aliwataja watuhumiwa hao kwa majina, alisema kuendelea kuwamo ndani ya chama hicho kunakifanya kikose mvuto na mashiko kwa jamii.

Katika kikao cha Nec Aprili, mwaka huu Makongoro alikuwa mwiba kwa watuhumiwa hao huku akihoji mantiki ya mwenyekiti wake kuwanadi majukwaani wakati wa kampeni za urais wa mwaka jana.

Makongoro ambaye aliwasilisha hoja kwa aina yake akitumia neno 'site' kuwakilisha vijiwe vya wanachama, alisema mwenyekiti alivyowanadi watuhumiwa hao katika uchaguzi wa mwaka jana: “site walihoji sasa ndiyo nini?”

Mpango wa kujivua gamba ulitangazwa na Rais Kikwete wakati wa maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM mjini Dodoma, akisema lengo ni kukihuisha chama na kukirejesha katika misingi yake ya TANU na CCM ya mwaka 1977. Chanzo: Gazeti Mwananchi

Monday, September 5, 2011

Kamati ya kumchimba Jairo kuanza kazi leo

Mwenyekiti wa Kamati Teule ya kuchunguza tuhuma za Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, kuingilia Haki na Madaraka ya Bunge ya kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Ramo Makani, amesema leo kamati yake itakutana kwa mara ya kwanza na kupitia hadidu za rejea ili waanze kazi hiyo.

Makani ambaye ni mbunge wa (Tunduru Kaskazini-CCM), anawaongoza wabunge wengine ambao ni, Gosbert Blandes (Karagwe-CCM), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF), Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).

Akizung na gazeti hili jana, Makani alisema watakutana leo asubuhi na kuongeza kuwa mbali na kupitia hadibu za rejea, watapanga ratiba ya kufanya kazi hiyo.

Julai 26, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, liliunda kamati hiyo yenye wajumbe watano itakayokuwa na kazi ya kuchunguza sakata zima la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Kamati hiyo iliundwa kabla ya kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge, baada ya wabunge kuridhia ufanyika uchunguzi huo.

Spika Makinda pia alizitaja hadidu rejea za kamati hiyo kuwa ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilisha uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.

Nyingine ni kamati hiyo kuangalia uhalali wa utaratibu huo kisheria ama kikanuni, iwapo fedha hizo kama zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na kuangalia matumizi halisi ya fedha husika.

Pia kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kukamilisha uwasilishaji wa bajeti ya wizara hiyo bungeni.

Vilevile, kuchunguza mfumo wa serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na utaratibu wa kuliarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.

Nyingine ni kuangalia nafasi ya mamlaka ya uteuzi kwa ngazi ya makatibu wakuu katika kushughulikia masuala ya nidhamu ya anaowateua na kuangalia mambo mengine yoyote yanayohusiana na masuala hayo.

Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda usiozidi wiki nane na itawasilisha taarifa yake wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge, utakaoanza Novemba 8, mwaka huu.

Friday, September 2, 2011

Jairo awatikisa Kikwete, Pinda

-Luhanjo, Ngeleja ‘kubebeshwa msalaba?”
-Serikalini sasa kwafukuta kila eneo

BAADA ya Bunge kuunda Kamati Teule ya kuchunguza sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, hali sasa si shwari serikalini na Rais Jakaya Kikwete, anaelezwa kujiandaa kufanya maamuzi mazito kusafisha hali ya hewa ya kisiasa inayoelekea kuvuruga mkakati wake kukisafisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mtindo maarufu sasa wa ‘kujivua gamba’.

Habari za ndani ya Serikali zimethibitisha kwamba kwa sasa kuna mtikisiko mkubwa uliotokana na mkanganyiko uliosababishwa na uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kutangaza kurudishwa kazini kwa Jairo aliyekuwa likizo akisubiri kuchunguzwa, uamuzi ambao ulitenguliwa na Rais Kikwete.

Sakata hilo la Jairo sasa limewagusa kwa namna isiyo nzuri viongozi wote wa juu wa Serikali, akiwamo Rais Kikwete mwenyewe, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, (aliyetamani hata kutimuliwa kabisa kwa Jairo), Luhanjo (aliyemrudisha kazini) na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliyempokea wizarani kwa mbwembwe, akiruhusu hata wafanyakazi wengine kusukuma gari lake.

Kuguswa kwa waandamizi hao wa juu serikalini, kunatishiwa zaidi na hatua ya Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza sakata hilo, jambo ambalo si ishara nzuri kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Bunge kuchunguza mtendaji wa juu wa Ofisi ya Rais Ikulu, ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi.

Habari za ndani ya Serikali zinaeleza kwamba uamuzi wa kutengua uamuzi huo, saa chache baada ya kuwa umetangazwa na Luhanjo, ulitokana na Rais Kikwete kukwerwa na uamuzi huo ambao imethibitika kwamba ulifanyika katika mazingira tata.

Ikulu ililazimika kutoa taarifa ya ufafanuzi baada ya baadhi ya vyombo vya habari kutafsiri kwamba kulikuwapo na ugeugeu kwa ofisi moja (Ikulu) kutoa maamuzi yanayokinzana; yaani uamuzi wa kumrudisha Jairo kazini kwa mbwembwe na uamuzi wa kutaka aendelee kuwa likizo akisubiri hatima yake.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Agosti 26, 2011 kwa vyombo vya habari ikionyesha kuwa na uharaka (urgent) ilieleza hakukuwa na mkanganyiko wowote kati ya Rais Kikwete na Katibu Mkuu Kiongozi wake, Luhanjo, kwa maelezo kwamba wote walikua sahihi kwa mamlaka waliyonayo kisheria.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ikiwa na baadhi ya meneno yaliyowekewa msisitizo kwa herufi kubwa ilieleza;

“Julai 21, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi Phillemon Luhanjo, akitumia madaraka yake ya Mamlaka ya Nidhamu ya Watumishi wa Umma, alitangaza hatua ya kumpa likizo ya malipo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishatai na Madini, David Kitundu Jairo, ili kupisha uchunguzi aliokuwa ameuagiza ufanyike dhidi yake.

“Luhanjo alichukua hatua ya kumsimamisha Jairo kufuatia tuhuma zilizokuwa zimeelekezwa dhidi yake (kwake) na baadhi ya wabunge wakati wa mjadala kuhusu Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2011/12 katika kikao cha Bunge kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2011.

“Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa Wizara kuomba michango ya fedha kutoka kwenye taasisi zilizoko chini ya usimamizi wake ili kusaidia Bajeti ya Wizara hiyo kupita kwa urahisi.

“Kufuatia hatua hiyo ya kumsimamisha kazi Bw. Jairo, Katibu Mkuu Kiongozi alimwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kufanya ukaguzi maalumu na uchunguzi wa awali juu ya tuhuma hizo.

“Tarehe 9 Agosti, 2011, Utouh aliwasilisha Ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, na tarehe 23, Agosti, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi akiambatana na Utouh, alitangaza mbele ya waandishi wa habari matokeo ya ukaguzi huo maalumu na uchunguzi wa awali juu ya tuhuma dhidi ya Jairo,” ilieleza taarifa hiyo.

Katika Ripoti yake mbele ya waandishi wa habari, taarifa ya Ikulu ilinukuu taarifa ya Utouh ikieleza: “Ukaguzi maalum haukuthibitisha kuwapo kwa usahihi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David Kitundu Jairo.”

Taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kwamba Katibu Mkuu Kiongozi alitumia taarifa ya CAG kuwaambia waandishi wa habari kwamba: “Matokeo ya uchunguzi huo ni kwamba tuhuma zilizotolewa Bungeni tarehe 18 Julai, 2011, hazikuweza kuthibitika.”

Akitumia vifungu vya sheria, Luhanjo amenukuliwa na Ikulu akisema; ”mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu, Nishati na Madini, David Kitundu Jairo, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma (notice) na Hati ya Mashitaka kwa sababu Bwana David Kitundu Jairo, hajapatikana na kosa la kinidhamu (disciplinary offence) kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi Maalumu.”

Luhanjo alinukuliwa akisema kwamba kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya Utumishi Umma ya Mwaka 2002 na kanuni zake za Mwaka 2003, aliamuru Jairo aendele kazini siku ya Jumatano Agosti 24, 2011.

Katika ufafanuzi wake, Ikulu ilieleza kwamba, “baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya CAG na uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu suala hilo asubuhi ya tarehe 25 Agosti, 2011, Rais Kikwete, aliamua kuwa Jairo asirudi kazini mpaka kwanza yeye Rais atapoamua namna gani ya kurudi kazini, lini na wapi.

“Katibu Mkuu Kiongozi alifikisha uamuzi huo wa Rais kwa David Jairo ambaye mapema asubuhi ya siku hiyo alikuwa ameripoti kazini. Ndugu Jairo alitii uamuzi huo wa Rais. Tunapenda kusisitiza kuwa Rais hajawa kigeugeu kwa sababu alifanya uamuzi mmoja tu baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi.”

Taarifa ya Ikulu ilionyesha pia kwamba uamuzi huo aliufanya kabla ya Bunge kulizungumzia suala hilo na hivyo uamuzi huo wa Rais haukutokana na shinikizo la Bunge na kwamba pamoja na kumweleza Katibu Mkuu Kiongozi, Rais pia alimfahamisha Waziri Mkuu kuhusu uamuzi wake huo asubuhi hiyo ya Agosti 25, 2011.

Maelezo hayo ya Ikulu yanaashiria kwamba kwamba uamuzi wa Luhanjo umechokoza mambo mengi yanayomhusu mtendaji huyo wa juu serikalini, zikiwamo taarifa zinazohusu muda wake wa kustaafu na maamuzi na mahusiano yake kikazi na watendaji wengine katika wizara alizowahi kufanya kazi kabla ya kuhamishiwa Ikulu.

Luhanjo amewahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na WIzara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuhamishiwa Ikulu kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, nafasi ambayo inaelezwa kwamba alitarajiwa kuwa amestaafu kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010.

Baadhi ya wachambuzi na asasi za kiraia na vyombo vya habari vimekuwa vikitoa tafsiri mbaya kwa Serikali kuhusu suala hilo la Jairo vikianzia na kauli ya Pinda Bungeni kwamba angekuwa na mamlaka kisheria angemchukulia hatua Jairo siku hiyohiyo ya tuhuma, kabla ya Serikali kumpa likizo na kutokea kwa utata baada ya taarifa ya CAG.

Miongoni mwa waliotoa matamko waziwazi ni Mbunge wa zamani wa Bumbuli na mtendaji mwandamizi mstaafu serikalini William Shellukindo, ambaye alisema moja kwa moja kwamba Luhanjo ameshindwa kumsaidia Rais Kikwete.
Shelukindo ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Rais Ikulu (cheo ambacho sasa kinaitwa Katibu Mkuu Kiongozi) katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi Jumapili iliyopita akisema Luhanjo ameonyesha utovu wa nidhamu na ameidhalilisha Ikulu kutangaza kumrejesha Jairo bila kupitia bungeni.

Soma zaidi