Monday, September 15, 2014

TGNP Mtandao yapeleka vuguvugu la katiba Mpya vijijini




 TGNP Mtandao wiki hii utaendesha semina za kuwajengea uwezo wananchi wa vijijini juu ya hali halisi ya mchakato wa katiba ulipofikia na namna ya wao kuendelea kuufuatilia na kuchukua hatua.

Lengo ni kuwaeleza wananchi juu ya kuendelea kufuatilia mchakato wa katiba mpya hatua kwa hatua ili kuhakikisha wanalinda masuala yao muhimu yaliyoko kwenye rasimu ya pili yasiondolewe au kutupiliwa mbali.

Akizungumza mratibu wa mradi huo kutoka TGNP Anna Sangai alisema kuwa TGNP baada ya kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na kuendesha mabaraza ya katiba ya kitaasisi imeona kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo wananchi waweze kuendelea kufuatilia mchakato huu  hatua kwa hatua, kuendelea kudai masuala ya haki za wanawake  na makundi yaliyoko pembebozoni yanapata nafasi ya kuingizwa kwenye katiba mpya.

“Tunaandaa mikutano mikubwa miwili vijijini  kufuatia hali halsisi ya mchakato wa katiba hivi sasa. Tutawakutanisha wanawake na wanaume  vijijini kuweka uelewa wa pamoja juu ya mchakato wa katiba mpya,  na kuendesha mijadala ya wazi (GDSS) ili kuwapa wananchi fursa ya kupaaza sauti zao juu ya kile wanancho kiona katika mchakato huu”alisema na kuongeza:
“Hatuwezi kuwapeleka watu wote Dodoma kushinikiza masuala yao yaingizwe na kama tunavyojua Bunge linaahirishwa Oktoba 4, lakini kila mmoja akipata uelewa anaweza kupaaza sauti yake pale alipo na akasikika”

Sangai alisema kuwa semina zitaendeshwa kwenye vituo vya taarifa na maarifa ambavyo vitachaguliwa katika wilaya za Mbeya Vijijini, Morogoro Vijijini, Kishapu, Bagamoyo, Kisarawe na Maneromango.

 Pia katika mikutano hiyo ya wazi itakayowashirikisha wananchi wote wa kata husika  wanaharakati hao watajadili juu ya kuhakikisha sauti za wananchi waliko pemeboni zinapata nafasi, kujadili namna watakavyoshiriki mchakato unaofuata ukiwepo kura za maoni,  kujadili hatima ya katiba mpya na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


No comments: