MTANDAO WA JINSIA TANZANIA - (TGNP)
MAJADILIANO YA MAPENDEKEZO YA KAMATI BUNGE
MAALUM LA KATIBA
KIKAO CHA 36-37
Katika bunge la 36 na 37 lilianza
rasmi kujadili rasimu ya katiba na Mwenyekiti wa bunge maalum la katiba
mheshimiwa Samwel Sitta aliwaelekeza
Wajumbe kujikita katika majadiliano kwa
kuzingatia sura ya 9 na 15 ambazo zinahusu Kuundwa
na madaraka ya bunge la jamhuri ya muungano na Ulinzi na usalama wa Jamhuri ya
Muungano, sambamba na kujadili sura mpya ambayo haikuwepo katika rasimu
nayo ni sura ya uchumi na maendeleo, utawala,Muundo wa serikali na muungano. Haya ndiyo maeneo walioelekezwa
wajumbe kujikita katika majadiliano yao na kujenga hoja ambazo zinagusa maeneo
hayo .
Mwelekeo wa majadiliano ulijikita zaidi kwenye
masuala yafuatayo: Wajumbe wengi walipendekeza kuwepo na kipengele ambacho
kitatambulika kikatiba ambacho kitaruhusu haki ya kugoma kama wafanyakazi au
watu wengine wowote ambao watakua na sababu za msingi za kufanya hivyo, mgomo
wao utambulike kuwa halali na bunge litatunga sheria itayoongoza uwepo na
usimamizi wa kipengele hicho.Na hii inaweza kuwekwa chini ya ibara ya 36 ambayo
inazungumza juu ya haki ya mfanyakazi.
Hata hivyo, wajumbe walionekana
kuelekeza majadiliano yao kwenye Ibara ya 47ambayo inazungumzia haki ya mwanamke wakiongozwa na Mheshimiwa, Avemarie Semakafu na Doreen Maro, wajumbe
walipendekeza kiongezwe kipengele (h)
ambacho kipekee kitazungumzia haki ya
kupata huduma bora na salama ya uzazi bure ili kuepusha vifo vingi
vinavyotokana na ujauzito. Pia wajumbe walipendekeza kiongezwe kipengele (i)
ambacho kitazungumzia haki ya mwanamke mjamzito kulindwa na kazi ngumu
zinazohatarisha maisha yake na ya mtoto aliye tumboni. Na ili kulisimamia hili
bunge litatunga sheria ambayo itasimamia na kuelekeza utekelezaji wa haki hii.
Hoja nyingine iliyozungumzwa sana ni kuhusu suala
la mahakama ya kadhi kwa Waislamu, suala hili lilijadiliwa sana na wajumbe waliowengi na wajumbe
walitofautiana, lakini wengi walipendekeza kwamba suala la mahakama ya kadhi
libaki chini ya ibara ya 32 ambayo inahusu uhuru wa imani ya dini kwani taifa
letu halina dini na kama tutaanza kuingiza masuala ya dini kwa upande mmoja
katika katiba tutakua hatujawatendea
haki upande mwingine ambao ni wa wakristo.
Vilevile suala la Haki ya mtoto lilijadiliwa sana na wajumbe
walio wakiongozwa na Mheshiwa:Mary
Mwanjelwa, Avemarie Semakafu, Askofu Thomas Maige, Paul Mapunda, wengi
walipendekeza kuwepo na kipengele ambacho kitafafanua mtoto ni kuanzia miaka
mingapi, ili kuondoa tatizo la unyanyasaji kwa watoto suala ambalo limekua sugu
katika taifa letu na limeathiri watoto wengi.
Suala la 50/50 nalo lilizungumzwa
sana na wabunge walio wengi wakiongozwa na Mheshimiwa: Doreen Maro,Faustina, na
kukubaliana litambulike na liingizwe katika katiba na bunge litatunga sheria ya
kusimamia utekelezaji wa suala hili. Suala hili linaweza kuongezewa kipengele
chini ya ibara ya 47 ambayo inazungumzia masuala ya haki za wanawake.
Kwa kiasi kikubwa majadiliano
yaligusa masuala mbalimbali ya kijinsia na wajumbe waliowengi walionekana kuwa
na uelewa kuhusu masuala ya jinsia maana kila mara mjumbe aliposimamam kuelezea
hoja Fulani alikua akitamka maneno uwiano wa kijinsia,jinsia na uzingatiaji wa
makundi yote.Hivyo basi hii inatoa taswira ya jitihada ya mapendekezo
yaliyotolewa na asasi mbalimbali zinazotetea haki za wanawake ikiwepo Jukwaa la
Wanawake na Katiba.
No comments:
Post a Comment