WANAWAKE wanaowanyanyasa waume zao kijinsia wametakiwa kuacha tabia hiyo mara moja kwa kuwa siyo desturi kwa mwanamke kujihusisha na matendo maovu yakiwemo ya ukatili wa kijinsia.
Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati wa akizindua kampeni ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia ya ‘Kuwa Mfano wa Kuigwa’ na Mradi wa CHAMPION.
“Ipo dhana potofu kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia hufanywa dhidi ya wanawake tu, hii si kweli, wapo baadhi ya wanawake wachache ambao hudiriki kufanya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wenza wao,” alisema Mama Kikwete katika hotuba yake
iliyosomwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani.
Mama Kikwete alisema wanawake hao yawezekana wanawanyanyasa waume zao kutokana na kipato chake au uduni wa maisha na ambao hufanya ukatili huo ni wabaya zaidi ya wanaume kwa kuwa hudhamiria vitendo hivyo bila huruma.
“Unyanyasaji wa kijinsia ni moja ya changamoto kubwa ulimwenguni na zipo sababu balimbali zinazosababisha unyanyasaji wa kijinsia lakini kwa hapa nchini mila potofu na hali duni ya uchumi ni moja ya vichocheo vya kuwapo kwa unyanyasaji wa kijinsia,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa utafiti, asilimia 44 ya wanawake wameshawahi kukutana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wenza wao, hivyo unahitajika ushiriki wa pamoja kukomesha hali hiyo.
“Pamoja na takwimu hizo, lakini jambo la kutia moyo ni kwamba zaidi ya asilimia 50 ya wanaume hawashiriki katika vitendo vya kunyanyasa wenza wao. Kwa mantiki hiyo ni vema kuwatambua wanaume hao kuwa ni mfano wa kuigwa na wengine,” aliongeza Mama Kikwete.
Aliwataka kina baba kutumia ushawishi wao kwa wenza wao na jamii kwa ujumla bila ya kutumia mabavu kuamsha majadiliano juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, kuvipinga kwa nguvu zote na kuonesha mfano kwa wenzao katika kupinga unyanyasaji wa kijinsia.
Alisema anategemea kila mmoja ataunga mkono kampeni hiyo kwani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinakwamisha na kudumaza mchango wa wanawake katika shughuli za uchumi na maendeleo ya nchi.
Pia aliishukuru Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (USAID) Tanzania na Engenderhealth- Champion kwa juhudi zao za kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na kuupongeza Mradi wa CHAMPION na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kufanikisha kampeni hiyo.
No comments:
Post a Comment