WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Kwiro ya mjini Mahenge wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro, ambao ni wanachama cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wamewaomba viongozi ngazi ya juu wa CCM kuwawajibisha na kuwavua magamba mafisadi wote wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali.
Wamesema kutowawajibisha kwa kuwavua magamba mafisadi hao, kutaendelea kuwafanya wananchi waendelee kutokuwa na imani na CCM pamoja na Serikali yao kutokana na viongozi wenye dhamana kushindwa kuchukua maamuzi magumu ya kuwavua magamba waliotuhumiwa
ufisadi. Wanafunzi hao ambao wengi wao ni wa kidato cha tano na sita, walisema hayo kwa nyakati tofauti hivi karibuni mjini Mahenge mbele ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Sarah Msafiri, ambaye pia ni Mbunge wa Vijana kwa tiketi ya UVCCM.
Mjumbe huyo wa NEC Taifa alifanya ziara katika wilaya za Mkoa wa Morogoro ili kukutana na vijana kwa lengo ya kupata maoni na changamoto zinazolikabili kundi hilo ikiwa pamoja na kutoa misaada ya vifaa vya aina mbalimbali vitakavyotumiwa kuanzisha miradi ya maendeleo
ya vijana.
Akizungumzia dhana ya kujivua magamba, mwanafunzi wa kidato cha sita, Frank Mauya, alisema kitendo cha viongozi wa juu wa CCM kutekeleza maamuzi yaliyopitishwa na kujivua gamba kwa mafisadi kunakishusha chama chini na pia kuendelea kuchafuliwa.
“Ni kweli hawa aliotajwa kwa kashfa ya ufisadi, ni watuhumiwa tu, lakini kuendelea kuacha kwa sababu ya hizo ni tuhuma pekee, kunaendelea kuididimiza CCM na wananchi kupoteza imani ya Chama na Serikali,” alisema mwanafunzi huyo.
Naye Nurdin Makonya pia wa kidato cha sita, alisema hivi sasa Umoja wa Vijana wa CCM unatumika kama kivuli cha baadhi ya wakubwa ndani ya CCM ya kufanya kampeni za kuwania urais wa mwaka 2015.
“Sisi wanafunzi ambao ni wanachama wa UVCCM tunaona Umoja wetu unatumika vibaya kwa
baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wanapotoa matamko ambayo hayajengi umoja wa chama,” alisema Makonya.
“Kinachoonekana matamko yao yana mwelekeo wa kuwagawa wanachama na hilo ni kutokana na sababu ya mbio za urais katika uchaguzi mkuu wa 2015,” aliongeza mwanafunzi huyo.
Hata hivyo, alisema katika uchaguzi ujao wa ndani ya jumuiya za chama hicho, wenyeviti wa Umoja huo watakaochaguliwa pamoja na wajumbe wao, wasiwe watu wa kuandaliwa kwa ajili ya kuwachagua marais wajao, bali wawe ni chachu ya kupigania maendeleo ya kiuchumi na
kijamii kwa kundi la vijana nchini.
Akijibu baadhi ya hoja za wanafunzi hao, Mjumbe huyo wa NEC Taifa alisema dhana ya kujivua gamba bado ipo pale pale ni kuanzia kwa viongozi wa ngazi ya Taifa hadi wale wa chini na kinachohitajika ni ushahidi unaojitosheleza kuwafikisha mahakamani.
“Zipo tuhuma za ufisadi na endapo atajitokeza mtu mwenye ushahidi auwasilishe kwa viongozi
wa juu wa CCM na hao wanaotuhumiwa watafikishwa mahakamani ili wawajibishwe,” alisema Msafiri.
Hata hivyo, aliwataka vijana nchini wasikubali kutumiwa na makundi ambayo yana mwelekeo wa kuifanya nchi isitawalike na kuwasihi wajitokeze kwa wingi kutoa maoni ya uundwaji wa Katiba mpya mara Tume ya kukusanya maoni itakapoteuliwa na kuanza kufanya kazi mapema Januari mwakani.
No comments:
Post a Comment