Wednesday, December 7, 2011

Spika Atetea Posho Mpya

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amekiri nyongeza ya posho za vikao vya wabunge kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 kwa siku na kusema imesababishwa na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma.

Ametetea uamuzi wa nyongeza hizo kuwa una nia njema ya kuwawezesha wabunge wamudu
gharama za kuwawakilisha wananchi vizuri, kwa kuwa mishahara wanayolipwa ni midogo ikilinganishwa na gharama wanazoingia wakiwa bungeni.

Makinda alisema hayo Dar es Salaam jana baada ya kuzindua Ripoti ya Maendeleo ya
Wanawake Duniani kuhusu Haki kwa mwaka 2011.

Ripoti hiyo imeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Jinsia na Uwezeshaji kwa Wanawake
(UN Women) na Shirika la UN la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).

Makinda alitaja siku ambazo wabunge walilipwa posho hizo mpya kuwa ni Novemba 08, 09
na 11, mwaka huu pamoja na wiki ya pili ya Bunge la Mkutano wa Tano na kueleza kuwa
pasipo kuwa na vikao vya Bunge, wanacholipwa ni mshahara pekee.

“Ni vyema jamii ifahamu kuwa wabunge hawalipwi fedha nyingi kama inavyozungumzwa
na baadhi ya watu na kwamba, wanachobaki nacho baada ya makato ya mkopo wa gari na kodi, hakiwatoshi kumudu gharama zote wawapo Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge, kama vile malazi na nyinginezo,” alisema Makinda.

Akichanganua kipato cha mbunge kwa mwezi, Makinda alisema mbunge analipwa Sh
milioni 2.3 tu kama mshahara na katika malipo hayo, hukatwa Sh 700,000 za kodi na Sh
800,000 za mkopo wa gari. Kwa hesabu hizo, mbunge kwa mwezi anabakiwa na Sh 800,000 tu.

“Hebu fanyeni hesabu muone katika mshahara huo mbunge anabaki na shilingi ngapi?

Na mkumbuke pia kuwa fedha hiyo ndiyo anayoitumia kwa gharama za kutengeneza gari lake endapo litapata matatizo, mafuta na kwa ajili ya matumizi mengine kama atataka kwenda jimboni na kwingineko kwa sababu za kikazi,” alisema Makinda ambaye ni Mbunge wa Njombe Kusini (CCM).

Alisema posho ya Sh 70,000 isingemsaidia kumudu gharama hata za chumba kwa sababu
zimekuwa juu mno kutokana na mji wa Dodoma kuwa kituo cha elimu ya vyuo vikuu kwa sasa.

“Kila kitu kimepanda bei na kwa bahati mbaya nyumba zile za CDA (Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu) zilizokuwa nafuu zilichukuliwa na wabunge wa Bunge la Tisa kwa
mikataba binafsi na wengi hawajazirudisha hadi sasa ili kuwezesha wapya kuzipangisha,”
alisema Spika.

Kitendo hicho cha wabunge wa Bunge la Tisa kung’ang’ania nyumba za CDA kwa mujibu wa Makinda, kimesababisha wabunge wapya wapange hoteli ambako hutozwa fedha nyingi tofauti na kipato wanachokipata.

“Pia sio kweli kwamba posho hizo zinatolewa kinyemela kwa sababu zilipitishwa katika vikao halali na kukubaliwa kuwa atakayezipata ni yule mbunge atakayehudhuria vikao vya Bunge asubuhi mpaka vitakapoahirishwa tu.

“Atakayesaini asubuhi na jioni ndiye atakayekuwa na uhalali wa kulipwa. Hata Kabwe Zitto anayezizungumzia, hajapewa hata senti moja kwa kuwa hakuwepo vikaoni, alikuwa mbali,” alisisitiza Makinda na kuongeza kuwa mshahara huo ni wa tangu mwaka 2003 na haujawahi kufanyiwa marekebisho yoyote hadi sasa.

“Sioni kama kuna malipo ya kustaajabisha umma kwa sababu hali halisi inajionyesha wazi, mazingira ya gharama za maisha nazo zinaonekana kiasi cha kushawishi kuwepo kwa nyongeza hiyo katika posho,” alisema.

Hivi karibuni, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akikanusha kuwepo kwa nyongeza hiyo.

Dk. Kashililah katika taarifa hiyo alikiri kuwa wabunge wanataka waongezewe posho za vikao, lakini mapendekezo hayo, hayajaanza kutekelezwa.

Alisema mapendekezo ya nyongeza hiyo yaliibuka katika mkutano wa wabunge mjini Dodoma Novemba 8 mwaka huu, lakini hadi sasa hayajaanza kutekelezwa.

“Suala la mabadiliko ya posho za vikao vya Bunge lilijitokeza katika Mkutano wa Wabunge, tarehe 8 Novemba, 2011 walipoiomba Serikali iangalie upya suala hilo kwa lengo la kuboresha,” alisema Dk. Kashililah katika taarifa hiyo.

“Hadi tunapotoa tangazo hili (Jumapili), Serikali haijatoa taarifa iwapo posho hiyo imeongezeka kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000," taarifa hiyo ilieleza.

No comments: