Tuesday, December 13, 2011

Serikali Yasimama Kidete Kupinga Ushoga

SERIKALI imepinga kwa nguvu zote na kukataa mapendekezo manne yaliyotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa yakiwemo ya ndoa za jinsi moja, tohara kwa wanawake, mahari na ndoa za mitala ambayo yanakwenda kinyume cha misingi ya maadili,
utamaduni, mila na desturi za Watanzania.

Mapendekezo yaliyokataliwa na Serikali ya Tanzania yaliyoamuliwa na Baraza hilo, yalilenga kuruhusu haki ya ndoa za jinsi moja “ushoga,” kufutwa kwa ndoa za mitala (mke zaidi ya mmoja), kufuta utoaji wa mahari wakati wa kuoana pamoja na tohara za wanawake.

Mapendekezo hayo yalifikiwa kwenye mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la UN uliofanyika ,Oktoba mwaka huu mjini Geneva nchini Uswisi, baada ya kujadili taarifa za nchi mbalimbali kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu kwenye nchi zao zilizowasilishwa Julai mwaka huu.

Kukataliwa kwa mapendekezo hayo manne kati ya 53 yanayofanyiwa uchambuzi wa kina kwa
kuhusisha wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria kutoka wizara mbalimbali, kumelenga kudumisha utamaduni, maadili, mila na desturi za Watanzania kwa vile mapendekezo hayo ni pandikizi, si ya msingi na yameletwa kutaka kuyahalalisha.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua warsha ya siku tatu ya maofisa wa Serikali kutoka wizara mbalimbali na wakuu wa idara zake ya kupitia, kujadili na kutoa mapendekezo yao juu ya taarifa ya mapendekeo 153 yaliyopitishwa na Baraza hilo.

Kwa mujibu wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nchi mbalimbali ziliwasilisha taarifa zao zinazohusu Haki za Binadamu kwenye Baraza la Umoja huo Julai mwaka huu, ambapo mapendekezo 153 yaliyoamuliwa na Baraza hili yakiwemo manne ambayo Serikali ya Tanzania
imeyakataa moja kwa moja.

Masaju alisema Serikali imekubali mapendekezo 96 wakati mapendekezo 53 hayajakubaliwa na yatawasilishwa kwa wadau ili kuwashirikisha waweze kuyajadili ili kufikiwa makubaliano ya pamoja kabla ya kuwasilishwa tena kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

“Katika majadiliano juu ya mapendekezo ya Baraza la Umoja wa Mataifa, yaliyofikiwa 153, ambapo mapendekezo 96 yameafikiwa na kuungwa mkono ya Serikali ya Tanzania,” alisema Masaju na kuongeza: “Lakini mapendekezo 53 bado hayajafikiwa, ndiyo yanapaswa kwanza kujadiliwa na wadau wakiwemo watumishi wa Serikali ambayo yanagusa katika sekta zao, yanahitaji kuungwa mkono na wananchi, lakini haya manne tumeyakataa kabisa,” alisema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema Serikali imekataa pendekezo la kuingizwa kuwa ni jambo la haki za binadamu la kuwa na ndoa za jinsi moja kwa kuwa jambo hilo ni kwenda kinyume cha sheria za nchi na haliwezi kukubaliwa na jamii ya Watanzania pamoja na Waafrika kwa ujumla.

Pia Serikali imekataa kufuta ndoa za mitala ambazo zimekuwepo kulingana na msingi wa imani za dini na utamaduni wa baadhi ya makabila nchini, kama ilivyo kwa pendekezo la kufuta mahari wakati wa kuoana.

Alisema mila na desturi za makabila ya Tanzania, moja ya msingi wake ni wakati wa kuoana mke na mume, suala la mahari ni sehemu ya utamaduni ambao ukoo unaooa unatakiwa kutoa mahari kabla ya kufungwa ndoa, hivyo jambo hilo haliwezi kufutwa.

Lakini kwa upande wa tohara kwa wanawake, tayari Serikali ya Tanzania ililipiga marufuku kuanzia mwaka 1998, hivyo imeliunga mkono kwa kuwa Tanzania inazuia vitendo vya kuwafanyia tohara wanawake.

Pamoja na hayo, alisema maamuzi ya mapendekezo 53 yaliyoamuliwa kujadiliwa kwanza na
wadau pamoja na wataalamu wa sheria kutoka wizara mbalimbali yanatakiwa kuwasilishwa
makubaliano yake katika Baraza hilo la Umoja wa Mataifa kabla Mkutano wa 19 wa Haki za Binadamu utakaofanyika Machi mwakani.

Alisema Tanzania ni nchi inayotekeleza na kusimamia misingi mizuri ya haki za binadamu kwa kutoa uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, uwakilishi wa jinsia zote katika maamuzi na usawa wa binadamu.

Naye Mwakilishi wa Kamishina wa Haki za Binadamu katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki wa UN, Musa Gassama, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kusimamia vyema haki za binadamu kwa njia ya ushirikishwaji wa makundi na taasisi nyingine.

Hivi karibuni, Tanzania ilieleza kwamba haiko tayari kupokea misaada yenye masharti au shinikizo kuhusu kuruhusu ndoa za jinsi moja baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kutoa tamko hilo akiwa Australia.

Marekani nayo imeonesha dhamira kama hiyo ya kufuta misaada kwa nchi zisizoruhusu ndoa ya jinsi moja ambazo kwa mujibu wao, ni suala la haki za binadamu.

No comments: