Tuesday, December 2, 2008

Zitto: CCM ichunguzwe ilivyochota mapesa EPA


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema) mwenye ushawishi mkubwa nchini, Zitto Kabwe, anataka uchunguzi maalumu ufanywe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu matumizi ya CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ili ukweli wote ufahamike.

Sambamba na hilo, Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, amependekeza iundwe mahakama maalumu (Special Tribune) kwa ajili ya kesi zinazohusu Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika taarifa yake kwa Raia Mwema, Zitto anasema: "Njia pekee itakayowatoa CCM katika hili ni kwa wao kuruhusu uchunguzi maalumu kufanywa na CAG. Baada ya uchunguzi, Mkaguzi ataueleza umma CCM walitoa wapi fedha zao na walizitumia namna gani. Yeye pekee ndiye anayeweza kuwasafisha kama hawahusiki na fedha za EPA, na sio maneno ya baadhi ya viongozi wa CCM ya kujaribu kujitakasa."

Kwa mtazamo wa Zitto, kesi za Kisutu hazitaonyesha ukweli wote juu ya nini hasa kilitokea mwaka 2005 Benki Kuu. "Kesi ya Kisutu haitatuambia ukweli juu ya kikao cha baadhi ya viongozi wa CCM na Gavana wa Benki Kuu mara baada ya kugundua kuwa CCM hawakuwa na fedha za kutosha za kampeni baada ya Kikwete kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM," anasema Zitto katika taarifa yake hiyo.

Zitto anasema: "Suluhisho nililonalo mimi ni kuundwa kwa mahakama maalumu (special tribunal) ambayo panelists wake watakuwa Watanzania waliotumikia nchi kwa uadilifu kama majaji wastaafu, wanasheria wakuu wastaafu, magavana wastaafu wa Benki Kuu au wakuu wa taasisi za umma wastaafu, wahadhiri waliobobea katika masuala ya fedha na sheria.”

Mbunge huyo amependekeza kuwa mahakama hiyo maalumu iundwe kwa sheria ya Bunge. “Mahakama hii iweke mazingira ambayo watu waitwe na kusema kweli, ukweli wote. Mahakama hiyo maalumu iwe na uwezo wa kutoa amnesty kwa watu ambao itaridhika na ushahidi wao na ushirikiano wao katika kufikia ukweli wa matatizo yote yanayohusu rushwa kubwa kubwa zilizopata kutokea hapa nchini.”

Kwa mtazamo wake, mahakama hiyo isiwe ya EPA tu, bali pamoja na masuala kama ya Meremeta, IPTL na Deep Green. “Iwe mahakama ambayo ikimaliza muda wake itatufanya, kama Taifa, tujiangalie na kusema haya yasitokee tena. Tusonge mbele."

Anasema Zitto: "Ndio maana nikiwaona hawa Watanzania waliofikishwa mahakamani na wale watakaofikishwa siku za usoni kuhusiana sakata la EPA, nafsi yangu inasema mahakama haitakata mzizi wa fitina. Kesi zitaenda, wenye kufungwa watafungwa, lakini hatutamaliza tatizo la EPA au tatizo kama hilo siku za usoni".
Anaamini kwamba hilo lisipofanyika, EPA itajirudia kwa njia mbali mbali na kwamba EPA haitaisha kwa judicial approach. "EPA itaisha kwa juhudi za pamoja za kimahakama na za kisiasa. Lazima kama nchi tufikie mahali na kusema haitatokea tena kwa chama chochote cha siasa au wanasiasa kutumia fedha za umma kwa manufaa yao kisiasa."

"Hatuwezi kuwa taifa ambalo kila siku tunajadili mambo yale yale na kurudia makosa yale yale. Hatuwezi kuwa Taifa ambalo vichwa vya habari vya magazeti vinapambwa na habari za ufisadi tu. Tunapaswa kutoka hapo kwa kusahihisha makosa, na kama tukifanya makosa mengine yawe makosa mapya," anasema mbunge huyo kijana.