Monday, December 22, 2008

Ufisadi mkubwa vyama vya siasa

PAMOJA na vyama vya siasa kuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa na ufisadi, imebainika kwamba ndani ya vyama karibu vyote vya siasa kuna ufisadi mkubwa katika mapato na matumizi ya mabilioni ya fedha za vyama hivyo.

Uchunguzi wa muda mrefu wa Raia Mwema umebaini kwamba vyama vya siasa vinakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992 kuhusiana na masuala yanayohusu fedha hali inayoeleza kuwa hakuna uadilifu katika matumizi ya mabilioni yanayoingia katika vyama hivyo ikiwa ni pamoja na ruzuku na fedha kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje.

Kumekuwa na matumizi makubwa ya fedha katika medani ya siasa katika miaka ya hivi karibuni, fedha ambazo baadhi zimebainika kuwa zinatoka nje ya nchi lakini hazitolewi maelezo kama sheria inavyoelekeza huku kiasi kingine kikubwa cha fedha kikitolewa na wafanyabiashara wa ndani wakiwamo ambao si raia wa Tanzania.

Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992 kinabainisha vyanzo vya mapato kwa vyama vya siasa kuwa ni pamoja na ada za wanachama, michango ya hiari, miradi ama hisa katika kampuni, ruzuku ya serikali na michango ama misaada kutoka vyanzo vingine lakini kwa sharti kwamba hesabu zake zinakuwa wazi.

Sehemu ya pili ya kifungu hicho inaelekeza vyama vya siasa kuwasilisha taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu michango kutoka nje ya nchi na pia kutoka kwa watu ambao si raia wa Tanzania hata kama wanaishi ama wanafanya biashara halali nchini lakini pia vyama vya siasa vinalazimika kuwasilisha hesabu sahihi kila mwaka.

Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amekiri kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika eneo la fedha kwa vyama vyote vya siasa, ingawa hakupenda kutaja jina la chama chochote cha siasa.

“Vyama vyote havizingatii sheria, hakuna hata chama kimoja kinachowasilisha chanzo cha mapato yake ya nje na ndani. Kama Jeetu Patel anawapa fedha TLP au chama chochote hawasemi, na kwa sheria yetu CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) hakagui hesabu za vyama vya siasa kwa kuwa si taasisi za umma,” alisema Tendwa wiki katika mahojiano ya simu na Raia Mwema.

Tendwa alizungumzia pia kuhusiana na udanganyifu mkubwa unaofanywa na vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na kutowasilisha taarifa sahihi za mapato yao, jambo ambalo amesema limetokana kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa Sheria ya Fedha za Umma ambayo haivitaji vyama vya siasa kama taasisi za umma.

“Hesabu za vyama zinaletwa kwa Msajili lakini ujue Msajili hakagui ila yeye anakaguliwa na CAG. Sisi tukisha kuwapa fedha (vyama vya siasa) wanakwenda huko wanatumia halafu wanaajiri mkaguzi wao wanayemjua wanakuja wanatudanganya kwamba wamekwenda vijijini, wamenunua sijui vitu gain, kumbe wengine uongo mtupu,” alisema Tendwa katika mahojiano hayo.

Alisema kwa sasa inaonyesha wazi kwamba kuna haja ya CAG kukagua hesabu za vyama vya siasa kwa maelezo kwamba udhaifu wa kisheria uliopo unatoa mwanya kwa fedha za umma zinazoingizwa katika siasa kupotea na lakini pia unatoa mwanya wa kuimarika kwa rushwa na ufisadi mwingine.

Katika kipindi cha bajeti ya miaka mitatu pekee 2005/2006 hadi mwaka 2008/2009, Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 72 kama ruzuku kwa vyama vya siasa, fedha ambazo hazijakaguliwa na CAG bali wakaguzi wanaoteuliwa na vyama husika na baadaye kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mwaka 2005/2006 zilitolewa Shilingi bilioni 39, mwaka 2006/2007 Shilingi bilioni 15 na mwaka 2008/2009 zimetengwa Shilingi bilioni 18 kwa ajili ya ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika dola.

Juhudi za kumpata CAG Ludovick Utouh, hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni jana Jumanne huku simu yake ya mkononi ikiendelea kuita bila majibu.

Kumekuwapo na manung’uniko makubwa miongoni mwa wana jamii kuhusiana na matumizi makubwa ya fedha katika siasa na wananchi wengi wamekuwa wakihoji mahali hasa yanakotoka mabilioni ya fedha zinazotumika katika shughuli za siasa nchini, baadhi zikiwa zinatumiwa na wagombea na sehemu nyingine ikitumika na vyama husika.

Mara baada ya kukabidhiwa kuongoza chama, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, alidhihirisha wazi kukwerwa kwake na jinsi fedha ilivyogeuzwa kuwa kigezo muhimu cha mtu kupata wadhifa wa kisiasa, hisia ambazo amezigusia katika hotuba zake mbalimbali.

Tayari kuna habari kwamba Kikwete amekuwa akipata wakati mgumu katika kutekeleza dhamira yake hiyo ya kuhakikisha kwamba fedha zinakuwa si kigezo cha kuwa kiongozi kutokana na kuguswa na matumizi makubwa ya fedha wakati wa kampeni za chama chake zilizomuingiza Ikulu lakini pia kuzungukwa na wasaidizi ambao au wameingia madarakani kwa kutumia fedha nyingi ama wanajiimarisha kwa kutumia fedha.

Baadhi ya wachunguzi wa kimataifa wamekuwa wakihoji hatima ya Tanzania kama Taifa kutokana na matumizi hayo makubwa ya fedha katika siasa na katika moja ya taarifa zake, Benki ya Dunia (WB), imeonyesha wazi kushitushwa na wingi wa fedha katika mchakato wa kisiasa nchini kutokana na kwamba vyanzo vya fedha hizo nyingi vina utata.

“Pamoja na nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi, bado kuna udhaifu mkubwa katika mfumo wa utawala unaochangia kukwama kwa vita dhidi ya rushwa katika siasa. Fedha za kuendeshea siasa zinaonyesha kuwa chanzo kikuu cha rushwa na ufisadi,na hii ni pamoja na kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa inataka vyama vya siasa kueleza vyanzo vyote vya mapato na kukaguliwa kila mwaka, utekelezaji wake ni kitendawili,” inaeleza sehemu ya ripoti ya WB ya hivi karibuni kuhusiana na hali ya rushwa
nchini.

Ripoti hiyo inabainisha kwamba suala la vyanzo vya mapato ya fedha za kuendeshea siasa limekuwa tatizo sugu kwa nchi nyingi duniani na inapendekeza kuunda chombo ama mfumo wa kuhakiki fedha za kuendeshea siasa.

“Inawezekana kufanikiwa kwa kuwapo kwa majadiliano kati ya vyama
vinavyoshiriki uchaguzi, ama kuwapo kwa Tume ya Bunge, ambayo itakuwa inaangalia na kuhakiki fedha za kampeni na pia ikiwezekana vyombo husika viweke ukomo wa kiwango kinachopaswa kuchangwa,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Katika kauli za kiaiasa zinazozungumzwa sasa kuhusiana na fedha katika siasa za Tanzania, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zitto Kabwe alidai majuzi kwamba ufike wakati CAG akague hesabu za vyama vya siasa kama njia ya kuvisafisha vyama vya siasa kutoka katika tuhuma za ufisadi.

katika kauli iliyokikera chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), Zitto amenukuliwa akitaka CAG afanye ukaguzi maalumu wa hesabu za CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

"Njia pekee itakayowatoa CCM katika hili ni kwa wao kuruhusu uchunguzi maalumu kufanywa na CAG. Baada ya uchunguzi, Mkaguzi ataueleza umma CCM walitoa wapi fedha zao na walizitumia namna gani. Yeye pekee ndiye anayeweza kuwasafisha kama hawahusiki na fedha za EPA, na si maneno ya baadhi ya viongozi wa CCM ya kujaribu kujitakasa," amenukuriwa Zitto akisema.

"Kesi ya Kisutu haitatuambia ukweli juu ya kikao cha baadhi ya viongozi wa CCM na Gavana wa Benki Kuu mara baada ya kugundua kuwa CCM hawakuwa na fedha za kutosha za kampeni baada ya Kikwete kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM," aliongeza mbunge huyo.

Akizungmza na Raia Mwema kwa njia ya simu jana, Zitto alisisitiza umuhimu wa CAG kukagua hesabu za vyama vya siasa kwa kuwa ni fedha za umma ambazo zinapaswa kukaguliwa kwa mujibu wa Katiba na sheria ya fedha za umma.

“Fedha zote hata za misaada kwa vyama vya siasa zinapaswa kukaguliwa na kwamba wakati wa uchaguzi vyama vyote viweke wazi taarifa za mapato na matumizi ya fedha zao za uchaguzi. Haya ni matakwa ya kikatiba na kisheria kwani fedha za ruzuku ni fedha za umma zinazotokana na kodi zetu,” alisema katika mazungumzo hayo ya simu.

Baadhi ya watu waliotoa maoni yao juu ya matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, kuhusu umuhimu wa vyama vya siasa kutaja vyanzo vya mapato kutoka nje ya nchi, waliiambia Raia Mwema ya kuwa utaratibu huo haufuatwi na umejaa usiri mkubwa karibu katika vyama vyote.

Mhadhiri wa Idara ya Uchumi ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Lenny Kasoga alisema ni kweli sheria inavitaka vyama vya siasa kutaja vyanzo vya mapato au misaada yao kutoka nje ya nchi, lakini utaratibu huo ni mgumu kuufuatilia kwa kuwa hakuna chama ambacho huweka wazi masuala ya fedha.

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Chadema Anthony Komu alisema kuwa kutaja vyanzo vya mapato kutoka nje kunategemea zaidi utashi wa wanasiasa, lakini kwa ufahamu wake viongozi wengi ni wadanganyifu.

“Chama chetu kinapendekeza kuwa ukaguzi wa hesabu za vyama ufanywe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ili vyanzo hivyo vijulikane,” alisema.

Kwa upande wake, Msemaji wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chama cha Wananchi (CUF) Suleiman Khalifa alisema ni mapungufu hayo ya ukaguzi yanayosababisha suala hilo lizungumzwe sasa na kwamba maoni ya wabunge wengi ni kwamba uletwe bungeni muswada wa kumpa uwezo zaidi CAG kukagua vyama vya siasa. Huenda muswada ukafikishwa bungeni mapema mwakani.

Huku hayo yakiendelea, Raia Mwema imeambiwa kwamba suala hilo la fedha za vyama, ni kati ya sababu zilizoutungua Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2008 uliokuwa uwasilishwe bungeni mwaka huu.

Sababu nyingine suala linaloonekana kutofurahiwa na baadhi ya vyama hivyo la muungano wa vyama kabla ya uchaguzi na sababu nyingine za kiufundi.

Hoja nyingine inayotajwa kusababisha kuahirishwa ghafla kuwasilishwa
bungeni kwa muswada huo ni suala la vyama vya siasa kuruhusiwa kuwa na vitengo vya ulinzi na usalama, hoja ambayo ilielezwa kuzua mjadala wakati muswada huo ulipojadiliwa na Kamati ya Sheria na Katiba ya Bunge.

Raia Mwema
Disemba 17, 2008