Tuesday, December 2, 2008
Waziri Mkuu ni sahihi, achaneni na semina hizi !
MWANZONI mwa wiki iliyopita Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kile ambacho tumekuwa tukikiamini kwa muda mrefu – kwamba idadi kubwa ya semina, warsha na makongamano yanayofanyika nchini yanalenga katika ulaji, na hayawasaidii wananchi wa kawaida; hususan wanavijiji.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wilayani Mpwapwa, Waziri Mkuu alisema kwamba ameshitushwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho wizara nyingi hutenga kwa ajili ya kuendesha semina, warsha na makongamano.
Lakini si tu kwamba Pinda aliishia katika kukemea uandaaji wa semina, warsha na makongamano hayo ya ulaji, lakini pia alisema kwamba kuanzia sasa hakuna wizara itakayoziandaa bila kwanza kupata kibali cha ofisi yake.
Tunapenda kumuunga mkono Waziri Mkuu kwa hatua hiyo sahihi aliyoichukua. Ingawa huko nyuma waliomtangulia walipata kukemea jambo hilo; lakini yeye amekwenda mbali zaidi kwa kuagiza kwamba semina, warsha na makongamano hayo yafanyike tu baada ya kupata kibali kutoka ofisi yake.
Tunadhani hiyo ni hatua murua itakayodhibiti ufanyaji holela wa semina, warsha na makongamano hayo ambayo, kama tulivyoeleza mwanzo, asilimia kubwa yanalenga katika ulaji na si kuwanufaisha walipa kodi wa nchi hii.
Kwa hakika, baadhi ya wizara zimekuwa zikirudia aina zile zile za semina, warsha na makongamano mwaka hadi mwaka. Matokeo yake ni kwamba makabati ya wizara hizo yamesheheni mada na maazimio ambayo hayafanyiwi kazi, na ndiyo maana tunasema kuwa hazina manufaa makubwa kwa walipa kodi wa nchi hii.
Ni matarajio yetu kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu itatoa vibali vya kufanya semina, warsha na makongamano hayo baada ya kufanyia maombi itakayopokea uchambuzi yakinifu na kuridhika kwamba mwisho wa yote kuna manufaa yatakayopatikana kwa kwa wananchi.
Tunamuunga mkono Waziri Mkuu tukitambua kuwa hatua hiyo ya kudhibiti warsha, semina na makongamano imekuja katika kipindi muafaka; kwani athari za anguko la uchumi wa dunia zimeshaanza kupiga hodi nchini mwetu.
Katika kipindi hiki cha anguko la uchumi wa dunia ambacho tunatarajia mapato ya Taifa ya nje na ndani kupungua kwa kiasi kikubwa, ni muhimu mno kwa Serikali yetu kuwa makini na matumizi yake ya pesa, kuwa makini na matumizi ya kila senti ya walipakodi nchini.
Ni matumaini yetu, hivyo basi, kwamba Waziri Mkuu Pinda, baada ya kuzishushia rungu semina, warsha na makongamano, pia ataangalia maeneo mengine yanayoteketeza fedha za Serikali na kuziba mianya hiyo haraka.