"NAAMINI katika usawa na utu wa binadamu wote, na wajibu wa kuwatumikia waishi vizuri pamoja na uhuru wao katika jamii ya amani na ushirikiano," Julius Nyerere.
Juzi, Desemba 10 watu wa Marekani wanaungana na jamii ya kimataifa kusherehekea Azimio la Haki za Binadamu na wanaume na wanawake wa kila utamaduni na imani, kila rangi na dini, katika nchi ndogo na kubwa, zilizoendelea na zinazoendelea.
Maneno ya Mwalimu yanagonga ukweli kwa Wamarekani. Tunaamini kwa dhati kwamba haki za binadamu na haki za msingi zilizomo katika Azimio la Haki za Binadamu zinaanzia kwenye kuzaliwa kwa binadamu wote.
Zaidi ya miaka sitini tokea lipitishwe azimio hilo Desemba 10, 1948, kumekuwa na maendeleo yanayoonekana katika kila bara kwa haki zilizoorodheshwa. Lakini, pamoja na kupita miongo sita, mamilioni ya watu bado wananyimwa haki za msingi na serikali zao.
Leo, karibu duniani kote, wanaume na wanawake wanafanya juhudi kupata haki za msingi ili kuishi kwa utu, kuzungumza bila woga, kuchagua watu wa kuwaongoza, kuwawajibisha viongozi wanaoshindwa kuwajibika na kupata haki sawa chini ya sheria.
Katika nchi nyingi, watu wanaojitolea kwa ujasiri kudai kwa njia ya amani haki za wananchi wenzao ndio wanaolengwa kuchukuliwa hatua na kufungwa na vyombo vya serikali.
Azimio la Haki za Binadamu ni zaidi ya orodha za haki kama zilivyoandikwa ni mwito wa kuchukua hatua. Azimio hilo linamtaka “kila mtu na kila chombo cha jamii ... kuheshimu haki hizi na uhuru kwa kuchukua hatua, kitaifa na kimataifa kupata kutambuliwa..."
Kama ahadi kubwa ya Azimio la Haki za Binadamu itatimizwa, jumuiya ya kimataifa na hasa zile nchi za kidemokrasia duniani, hazitakaa kimya huku kuna watu katika dunia hii ambao wanaishi bila kuwa na utu au chini ya utawala mbaya.
Kutokana na kuendelea kuwapo kwa wanaume na wanawake katika dunia hii ambao wanaendelea kunyimwa haki zao za msingi, sisi, ambao tunafaidi kujaaliwa uhuru lazima tuendelee kuunga mkono jitihada za kupata haki za msingi kwa wote na kuwaunga mkono wote ambao wanaupigania.
Kama Rais George Bush alivyosema: "Uhuru unaweza kupingwa, na uhuru unaweza kucheleweshwa, lakini uhuru hauwezi kunyimwa." Kwa muda, madikteta wanaweza kutawala, lakini hatimaye, wale wanaojitolea kupigania haki, huru na demokrasia watashinda, kama Havels na akina Mandela walivyofanya kabla yao.
Mara nyingi, watetezi wa leo wa uhuru wanashutumiwa na kushitakiwa na serikali zao wenyewe. Lakini katika historia, mashujaa hawa wanaume na wanawake watatambulika kwa wanayoyafanya. Wataheshimika kama wazalendo wenye uvumilivu ambao si tu wanahamasisha wananchi wenzao, lakini pia mfano wao unatoa matumaini kwa watu kila sehemu ambako wanapigania haki za msingi.
Kupamba moto kwa matakwa ya kuwa na haki za binadamu na demokrasia si matokeo ya juhudi binafsi za baadhi ya wasomi au uhamasishaji wa serikali za nje. Ukweli ni kwamba mwito huu unatokana na matakwa yenye nguvu ya binadamu ya kuishi kwa utu na uhuru na ushujaa binafsi wa wanaume na wanawake katika kila umri katika kila jamii ambao wanajitolea mhanga kwa ajili ya uhuru.
Tunaamini ya kuwa demokrasia ndiyo mfumo pekee wa serikali wenye uwezo kupata na kulinda haki za binadamu na uhuru wa msingi wa muda mrefu. Nchi ambazo utawala uko mikononi mwa viongozi wasiowajibika ndizo ambazo zinaongoza kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Lakini hakuna utawala ambao hauna kasoro. Demokrasia ni mfumo wa serikali ya watu na kwa ajili ya watu ambao unatokana na misingi ya binadamu kuwa na haki ya kuamua juu ya hatima ya maisha yao ya baadaye. Lakini sisi binadamu ni viumbe wenye kuweza kufanya makosa hivyo ni lazima kuwa na njia za kujisahihisha na kujipima kwenye serikali ya demokrasia.
Kujisahihisha na kujipima kunahitaji kuwa na asasi zenye nguvu za kiraia, vyombo huru vya habari vyenye nguvu, bunge na mahakama ambavyo vinafanya kazi yake bila kuhofia au kuipendezesha serikali na kuwapo kwa utawala unaoonekana wa sheria.
Demokrasia ya Marekani, kama zilivyo nyingine si nzuri kwa asilimia zote. Wananchi wetu wanajivunia historia ya kupambana katika kila kizazi tokea kuanzishwa kwa taifa hilo ili kuleta demokrasia hiyo karibu na msimamo unaoliliwa hata pale tunapopambana na mambo yasiyo na haki katika kila zama mpya.
Tunayachukulia kwa umakini mkubwa majukumu yetu ya Haki za Binadamu na katika nia thabiti ya kutimiza majukumu hayo tunaenzi kazi kubwa inayofanywa na na asasi za kiraia na vyombo huru vya habari.
Huwa hatuchukui maoni ya jinsi tunavyotekeleza demokrasia yetu kama kuingiliwa kwa mambo yetu ya ndani, na serikali nyingine nazo zisijisikie vibaya zinapoelezwa kuhusu demokrasia zao.
Serikali ya Marekani itaendelea kusikiliza na kujibu hapo hapo maoni mbalimbali kuhusu tunavyotimiza demokrasia yetu ikiwa ni pamoja na hatua tuliyochukua ya kulinda taifa letu kutokana na tishio la dunia la ugaidi. Sheria zetu, sera na jinsi tunavyofanya mambo vimebadilika sana katika miaka ya hivi karibuni.
Tunaendelea kulinda raia wasio na hatia wasishambuliwe wakati tunaendelea na jukumu letu la muda mrefu la kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa msingi. Kama sehemu ya juhudi hizi, Marekani inawasilisha ripoti kwa vyombo vya kimataifa kwa mujibu wa jukumu lake chini ya mikataba mbalimbali ya haki za binadamu.
Kujenga demokrasia makini dunia nzima ni kazi ya zama na vizazi mbalimbali, lakini kila mara ni kazi ya dharura ambayo haiwezi kusubiri. Demokrasia yetu wenyewe inajizungusha. Safari ya Marekani kuelekea kwenye uhuru na haki kwa wote imekuwa ndefu na ngumu, lakini tunajivuna kwamba tunaendelea kufanya maendeleo muhimu, matawi huru ya serikali, vyombo vya habari huru, uwazi wetu kwa dunia, na muhimu zaidi uvumilivu wa kiraia wa wazalendo wa Marekani umesaidia kuweka imani na matakwa ya kuanzishwa kwa taifa na jukumu letu la kimataifa la haki za binadamu.
Januari 20, mwakani demokrasia yetu wenyewe itaadhimisha tukio la kihistoria – kuapishwa kwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika kama Rais wa Marekani.
Martin Luther King, Jr., aliita tukio kama hilo "kutimiza ndoto nyingine isiyopata kutimizwa." Bado, tunatambua kwamba safari yetu ya kitaifa kuelekea kwenye umoja imara uliotabiriwa na waasisi wa taifa letu ni ndefu kuimaliza.
Njia ya demokrasia huwa si nzuri na mara nyingi haikunyooka, lakini ni ya uhakika. Njiani lazima kutakuwa na vizingiti na hata kukata tamaa. Mataifa mengine bado yana asasi dhaifu za serikali ya demokrasia na yanaendelea kuhangaika. Mengine yamejidhatiti kwa dhati kwenye demokrasia. Hatua za kusonga mbele zinaweza zikakwamishwa na mambo yasiyofaa. Kunaweza kuwa na kurudi nyuma kupita kiasi. Serikali zilizochaguliwa kwa njia ya kidemokrasi mara nyingi hazitawali kwa demokrasia zinapokuwa madarakani.
Mambo ya kuyazingatia kwa ajili ya kusonga mbele yako wazi: Wape raia uhuru mkubwa zaidi ili waweze kuutumia kwa ajili ya kusahihisha mapungufu yanayojitokeza ambayo yanakwamisha kuwapo kwa hali nzuri ya baadaye.
Katika dunia ya leo, matatizo yanayokabili mataifa ni nyeti hata kwa mataifa makubwa kuyakabili peke yake. Mchango wa asasi za kiraia, mawazo huru na habari katika kujadili matatizo ya kila nchi na ya kimataifa ni muhimu. Kuziwekea mpaka wa kisiasa asasi zisizokuwa za kiraia (NGO) na majadiliano ya umma ni vitendo ambavyo madhara yake ni kukwamisha maendeleo ya jamii yenyewe.
Katika kila eneo la dunia, kuna serikali ambazo zinaitikia miito ya kuwa na uhuru wa watu na wa kisiasa kwa kutowajibika kwa watu wao bali kuwanyanyasa wale wanaokuwa msitari wa mbele kupigania haki za binadamu na kuanika maonevu ya kila aina. Hivyo wananyanyasa asasi zisizokuwa za kiraia, vyombo huru vya habari ikiwa ni pamoja na intaneti.
Kwa asasi za kiraia na vyombo huru vya habari, uhuru wa kuzungumza, kukutana na watu na mkusanyiko wa amani ni oksijeni. Bila ya kuwa na vitu hivyo vya uhuru wa msingi, demokrasia inaminywa pumzi yake ya kupumua.
Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya serikali zinatumia madaraka vibaya dhidi ya NGOs, waandishi wa habari na wanaharakati wa vyama vingine vya kiraia.
Wakati demokrasia inapounga mkono kazi za wanaharakati wa haki za binadamu asasi za kiraia, tunawasaidia wanaume na wanawake katika nchi duniani kote kurekebisha mustakabali wao wenyewe katika uhuru. Na kwa kufanya hivyo, tunasaidia kujenga dunia nzuri zaidi na yenye usalama kwa watu wote. Lazima tuwalinde walindaji kwa sababu wao ni mawakala wa amani na mabadiliko ya demokrasia.
Kuna matakwa makubwa duniani yanayotaka kuwapo kwa uhuru mpana zaidi wa mtu na wa kisiasa kwa ajili ya kuwa na serikali yenye misingi ya demokrasia. Marekani inaunga mkono juhudi za wanaume na wanawake duniani kote kupata na kuonyesha haki zao.
Kuunga kwetu mkono kunaonyesha thamani kubwa ya watu wa Marekani. Kama Rais Bush alivyosema: "Uhuru ni haki ambayo haina mjadala wa kila mwanamume, mwanamke na mtoto na njia kuelekea kwenye amani ya kudumu katika dunia yetu ni uhuru."
Katika Marekani, tuko katika mchakato wetu wa demokrasia ya mpito wa kupata utawala mpya. Kazi ya Marekani ya kupigania uhuru duniani inazidi ile ya siasa zetu za ndani kwa sababu kuendelezwa kwa haki za binadamu na misingi ya demokrasia kuna thamani kubwa kwa wananchi wetu.
Utakapoingia madarakani utawala wa Barack Obama utakapoignai Januari hii, kazi hii muhimu ya uhuru wa binadamu itaendelea, itaimarishwa kwa kuungwa mkono na Bunge machachari lenye ushabiki wa masuala ya kimataifa na ya nyumbani kama ulivyo utamaduni wa watu wa Marekani.
Mwandishi wa makala hii, Mark Green, ni Balozi wa Marekani nchini Tanzania. Hii ni tafsiri isiyo rasmi ya makala yake ya Kiingereza kuhusu Haki za Binadamu ya kudhimisha siku ya Azimio la Haki za Binadamu lililotangazwa miaka 60 iliyopita.