Tuesday, December 2, 2008

Mramba, Yona wasota rumande


MAWAZIRI wawili waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa, Basil Pesambili Mramba na Daniel Ndhira Yona, wamepandishwa kizimbani wakituhumiwa kutumia madaraka vibaya wakiwa madarakani.

Mramba na Yona wote kwa pamoja wameshitakiwa kwa kuibeba kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya Washington DC, Marekani ambayo ilikuwa ikifanya kazi ya uhakiki wa mapato ya madini ya dhahabu nchini.

Mawaziri hao wawili walisomewa mashitaka yao na waendesha mashitaka kutokaTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hezron Mwankenja, kukiwa na ulinzi mkali wa makachero na askari magereza wenye silaha.

Pamoja na kutoa upendeleo wa kuongeza mkataba wa kampuni hiyo ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation, Mramba na Yona wakiwaWaziri wa Fedha na Waziri wa Nishati na Madini, waliisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 11 kutokana na kusamehe kodi kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Makosa hayo yameelezwa mahakamani hapo kutendwa katika kipindi cha mwaka 2002 na mwaka 2007, ambako Mramba aliandaa na kutoa matoleo ya Gazeti laSerikali (GN) yenye namba 423/2003, 424/2003, 497/2004, 498/2004, 377/2005 na 378/2005 ambayo yalilenga kutoa msamaha wa kodi kwa Alex Stewart (Assayers) Government BC uliofikia kiwango cha Sh 11, 752, 350, 148/- bila kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa mamlaka yao na nafasi zao, Mramba na Yona wamedaiwa mahakamani hapokwamba bila kuzingatia wajibu wao waliokabidhiwa na serikali waliingia mkataba ulioisababishia serikali hasara ya Sh 11, 752, 350, 148/- kutokana na kampuni hiyo ya uhakiki wa dhahabu.

Imedaiwa kwamba Mramba kupitia matoleo mbalimbali ya Gazeti la Serikali amewezesha kutolewa kwa msamaha wa kodi ya mapato iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo ya Alex Stewart kinyume cha sheria ya Kodi ya Mapato.

Kwa mujibu wa maelezo ya waendesha mashitaka hao, Mramba anadaiwa alitumia vibaya madaraka yake kwa kudharau ushauri wa TRA waliomtaka kutokubali kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa kampuni hiyo ya kigeni ambayo ililalamikiwa sana kwa kumega mapato ya dhahabu nchini.

Mawaziri hao wa zamani wanatuhumiwa pia kudharau maelekezo ya kamati ya ushauri ya serikali ambayo ilipendekeza kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkataba wa Alex Stewarts na badala yake waliongeza muda wa mkataba wa kampuni hiyo bila kuzingatia suala la kupitia upya ada iliyokuwa ikilipwa kwa kampuni hiyo na hivyo kuiingizia serikali hasara.

Katika kuongeza mkataba huo, Mramba na Yona wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kumshirikisha Dk. Enrique Segura wa Alex Stewarts katika kuingia naye mkataba wa nyongeza ya miaka miwili kuanzia Juni 14, 2005 hadi Juni 23, 2007 bila kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2002 na Sheria ya Madini ya mwaka 2002.

Mashitaka dhidi ya watuhumiwa hao yamefuatia kibali kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Elieza Feleshi kutoa kibali, juzi Jumatatu akisema kwamba viongozi hao waandamizi wametumia vibaya madaraka yao na wamesababisha hasara kwa mamlaka husika.

Watuhumiwa wote wawili walilazimika kupelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ikiwa ni pamoja na kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh. bilioni 3.9 kila mmoja, kwa kuzingatia kiwango cha fedha kilichopotea kwa makosa waliyoshitakiwa nayo.

Mramba na Yona walifikishwa Kisutu kwa gari maalumu la TAKUKURU aina ya Toyota Land Cruiser T319 ATD likisindikizwa na Toyota Rav 4 lenye namba T 528 AQQ likiwa na mawakili wa TAKUKURU na makachero huku kukiwa na magari mengine kadhaa yenye walinzi wa ziada.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo Desemba 2, 2008 itakapotajwa tena.

Raia Mwema
November 26, 2008