Monday, December 22, 2008

Seif: Hakuna sheria inayoagiza Serikali ya Tanganyika ifutwe

Desemba 4, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Seif Sharif Hamad, alitoa mada mjini Zanzibar iliyokuwa ikichambua hatma ya Zanzibar na mustakabali wa Muungano. Mwandishi Wetu ARISTARIKO KONGA, ameipata mada hiyo anapitia baadhi ya hoja na msimamo wa mwanasiasa huyo.

“[President Nyerere] managed half the work of a python… He swallowed Zanzibar all right but he did not crush its fighting force first. The live animal is a long time digesting, and its kicks are being felt hurtfully, and possibly even fatally, deep inside Tanganyika’s body politic.”

‘The Perils of Nyerere’ in The Economist of June 1964

SEIF Sharif Hamad amekichagua, nadhani kwa umakini mkubwa, kifungu hicho kutoka jarida la The Economist la mwaka 1964, akielezea mtazamo wake kwamba Tanganyika na mamlaka zake, tangu muda mrefu ilikuwa imepangilia kuimeza Zanzibar, si kwa bahati mbaya bali kwa makusudi, tena wakati mwingine kwa kutumia katiba na sheria.

“Mtafiti mmoja kutoka Argentina, Boaventura Santos de Sousa, aliwahi kuandika kwamba ‘mwandishi ingawa huandika kuhusu yaliyopita huwa anajaribu kueleza yaliyopo, si yaliyopita. Lakini, kwa kufanya hivyo, huwa pia anajiweka mbali na hali ya sasa na kwa hakika anaandika kwa ajili ya siku zijazo’.”

Kwa mujibu wa Seif, Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umepita katika masaibu kadhaa tokea uasisiwe takriban miaka 45 iliyopita, lakini mtikisiko ulioukumba katika siku za karibuni ni mkubwa sana. Kwamba ni mkubwa kwa sababu umegusa kiini cha Muungano huu ambapo suala linaloulizwa ni iwapo kwa kule kukubali kushirikiana katika baadhi ya mambo, je, Zanzibar na Tanganyika zimejifuta na hivyo kupoteza hadhi zake kama nchi?

“Hilo limekuwa ndiyo swali kubwa linaloulizwa na Wazanzibari, hasa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutamka bungeni kwamba Zanzibar si nchi.”

Seif anasema kwamba tangu kuasisiwa kwake, Muungano umejengeka kwa misingi ya hofu, kutiliana shaka na kutokuaminiana baina ya pande mbili zinazouunda, na wakati mwingine kumezua hata kutishia uhai wa Muungano wenyewe.

“Muungano umekuwa gumzo kuu katika takriban kila mjadala wa katiba na siasa katika nchi yetu. Umejitokeza na kujionyesha hivyo katika mwaka wa mwanzo wa Muungano kuhusiana na sakata la kuwa na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika, na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar; kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1964 – 1966; wakati wa kuunganisha vyama vya ASP na TANU kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977; katika mjadala wa Marekebisho ya Katiba wa 1983/84 na hatimaye kujiuzulu kwa Rais wa pili wa Zanzibar Sheikh Aboud Jumbe; wakati wa kuondolewa katika Uwaziri Kiongozi kwa mwandishi wa makala haya na hatimaye kufukuzwa katika CCM na wenzake sita mwaka 1988; katika harakati za madai ya kutaka kura ya maoni kuhusiana na Muungano huo mwaka 1989/90; wakati wa mjadala wa kuanzishwa vyama vingi mwaka 1991; katika sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) mwaka 1993; wakati wa mjadala wa G-55 kudai kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994; katika mjadala wa marekebisho ya 11 na 14 ya Katiba ya Muungano mwaka 1994/95; wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 1995 na ule wa 2000 na karibuni kabisa kuhusiana na suala la matarajio ya ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar na harakati za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki.

“Ukiondoa kuibuka kwake katika mijadala mikubwa ya kikatiba na kisiasa nchini, kwa upande mwingine katika uendeshaji wa shughuli za Serikali za kila siku, ‘matatizo na vikwazo kadhaa vya kiutawala na kiutendaji’ vimekuwa vikiripotiwa kila mara kwamba vinakwamisha uimarishaji wa Muungano.

Seif anasema tume na kamati kadhaa zimeundwa kuainisha matatizo ya Muungano na kupendekeza njia za kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda tume na kamati kadhaa, miongoni mwa nyingi, kuhusiana na masuala haya, ikiwamo Kamati ya Mtei, Tume ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1991, Kamati ya Shellukindo ya mwaka 1994, Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT), Kamati ya Jaji Mark Bomani ya mwaka 1995, Kamati ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998, Kamati ya 'Harmonization', na Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kussila).

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Seif Sharif anasema nayo iliunda kamati zake kwa madhumuni hayo hayo, ikiwamo Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992, Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna) ya 1997, Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman), Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000, Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje, Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya 2001, Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamati ya Mafuta, Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania, Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ), Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu, Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu ya mwaka 1996 hadi 1999, Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuyaondoa ya 2004.

“Ukiacha tume, kamati na ripoti hizo, kuanzia mwaka 1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya Pamoja ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar pamoja na Mawaziri wa Serikali zetu mbili ambao ulitarajiwa uwe ndilo jukwaa la kuzungumzia matatizo kutoka kwa washiriki wakuu wa Muungano huu na kuyapatia ufumbuzi unaofaa.

Utaratibu huu uliachwa kwa muda mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete, alilotoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali yake huko Ngurdoto, Arusha, Februari, 2006.

“Mikutano, makongamano, semina na warsha vimefanywa kujadili masuala haya na kupendekeza hatua za kuchukuliwa. Wasomi na wanafunzi wamefanya tafiti kadhaa na kujipatia shahada na stashahada hadi ngazi ya Ph.D juu ya Muungano lakini bado matatizo yako pale pale na yanaongezeka kila kukicha.

“Yanayoonekana na kuelezwa kama matatizo, mapungufu, dosari, kasoro na, kwa msamiati wa sasa, kero, yamekuwa ndiyo yale kwa yale. Nini basi kiini cha haya? Na vipi tutayatatua?

“Mimi nimeamua kutoa changamoto kupitia waraka huu kwa kuitazama historia ya Muungano, jinsi ulivyoundwa, matatizo yanayoukabili, nafasi na hadhi ya Zanzibar katika Muungano na nini hatma ya Zanzibar na mustakbali wa Muungano huko tuendako.

Nitakayoyaeleza yanaweza yakaonekana ni machungu kwa wakati huu wa sasa, lakini kama asemavyo Santos de Sousa yanaweza yakawa ndiyo ufumbuzi kwa siku zijazo.”

Katika mada yake Seif Sharif anajaribu kueleza asili na sababu za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ingawa anakiri hakuna jibu la moja kwa moja kuhusu chanzo hicho kwa kuwa kuna maelezo mengi.

“Maoni yanayotolewa kuhusu asili na sababu za Muungano yamekuwa yakitofautiana mno. Wapo wanaouleza Muungano huu kuwa ni wa pekee katika Bara la Afrika, kwani ndiyo pekee ulioweza kudumu katika kutimiza azma na malengo ya kuleta umoja wa Afrika (Pan-Africanism), na pia wapo wanauona kuwa ni jaribio la ukoloni mdogo wa nchi moja ya Kiafrika kuiteka na kuitawala nchi nyingine ya Kiafrika.

“Kutokana na maelezo na hoja nyingi na zinazokinzana kuhusu asili na sababu za Muungano, si rahisi kusema moja kwa moja kuwa maelezo yepi au hoja ipi ni sahihi. Utangulizi wa Mkataba wa Muungano wenyewe unataja sababu kuu ya kuunganisha nchi za Zanzibar na Tanganyika kuwa ni ‘maingiliano ya muda mrefu ya watu wa nchi mbili hizi na mahusiano yao ya kidugu na kirafiki … na … kuendeleza umoja wa watu wa Afrika.’ Lakini miaka 45 sasa baada ya uzoefu wa Muungano huu, Wazanzibari wanajiuliza kweli haya ndiyo madhumuni ya Muungano huu?

“Wazo la kuungana linaweza kurudishwa nyuma tokea zama za harakati za ukombozi wa nchi za Afrika. Waasisi na wakuu wa harakati za kupigania uhuru waliiona mipaka ya nchi zao iliyowekwa na wakoloni kuwa ni ‘mbinu za kibeberu’ zilizotekelezwa kwa ajili ya manufaa na maslahi yao. Kutokana na hisia hizo, mazungumzo ya kuanzisha aina fulani ya umoja miongoni mwa nchi huru za Afrika yalitawala duru za siasa katika miaka ya 50 na 60.

“Nadharia mbili zilijichomoza. Ya kwanza, ikishadidiwa na Kwame Nkrumah wa Ghana, ilikuwa ikitaka kuasisiwa kwa nchi moja tu ya Afrika nzima iliyoungana ikiwa na Serikali moja kwa bara zima. Nadharia hii ilipingwa na baadhi ya viongozi, wakiongozwa na Julius Nyerere wa Tanganyika, ambao walisisitiza haja ya kuanza na miungano ya maeneo (regional unions) chini ya mfumo wa Shirikisho badala ya kuwa na mpango wa Serikali moja.

“Katika kulifikia lengo hilo, viongozi wa kisiasa wa nchi tatu za Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanganyika – walikuwa wakifanya mikutano ya mara kwa mara kipindi chote cha kati ya mwaka 1961 na 1963 kuona jinsi gani wanaweza kutimiza ndoto hiyo. Mfumo wa Muungano uliokuwa ukiandaliwa ulikuwa ni ule wa Shirikisho. Tamko la Pamoja la viongozi hao lilisema: ‘Sisi, viongozi wa wananchi na Serikali za nchi za Afrika Mashariki … tunayakinisha nia zetu kuhusu kuwepo kwa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Mkutano wetu wa leo unasukumwa na hisia za umoja wa Afrika (Pan-Africanism), na siyo tamaa za maslahi binafsi ya eneo hili. … Ijapokuwa Zanzibar haikuwakilishwa katika mkutano huu, tunapaswa kuweka bayana kwamba nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika mikutano yetu kwa ajili ya uundwaji wa Shirikisho.’

“Lakini Umoja wa Afrika (Pan-Africanism) hauonekani kuwa ndiyo dhamira pekee au kama ndiyo dhamira halisi ya Muungano. Wengi wanaamini, na mimi nikiwa mmoja wao, kwamba dhana hiyo ilitumiwa tu kuficha njama za muda mrefu za Nyerere kutaka kuimeza na kuitawala Zanzibar. Katika mwaka 1961, wakati Tanganyika inakaribia kupata Uhuru wake, Nyerere alinukuliwa akisema: ‘Kama ningekuwa na uwezo wa kuvikokota visiwa vile [Zanzibar] na kuvitupa nje kabisa, katikati ya Bahari ya Hindi, basi ningefanya hivyo … Nahofia vitakuja kuniumiza kichwa sana.’

“Imani hii inatiliwa nguvu na mahusiano ya karibu na ya muda mrefu yaliyokuwepo kati ya chama kilichokuwa kikitawala Tanganyika, TANU, na ASP ambacho kilishika hatamu za utawala baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, mwezi mmoja tu baada ya Zanzibar kupata uhuru wake kutoka Uingereza hapo Desemba 10, 1963. Zilikuwepo taarifa tokea mwaka 1959 kwamba TANU na ASP zitakaposhika madaraka zitaziunganisha nchi mbili hizi kuwa Jamhuri moja.

“Wakati juhudi za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki zikiwa zinafifia, Nyerere aliona fursa Zanzibar ambayo hakutaka kuipoteza. Katika mazungumzo ya siri kati yake na Rais Abeid Amani Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, wakakubaliana kuziunganisha nchi mbili hizi. Hakukuwa na ushirikishwaji wa aina yoyote ule wa wananchi wa nchi hizi mbili katika maamuzi haya makubwa. Usiri uliogubika hatua hii kubwa unafichuliwa na si mwingine bali Nyerere mwenyewe pale aliposema: ‘[Tanganyika] tulipeleka polisi wetu Zanzibar. Baada ya kuyashinda matatizo kadhaa tukaungana. Sisi wenyewe kwa hiari zetu tulikubaliana kuungana. Karume na mimi tulikutana. Peke yetu wawili tu tulikutana. Nilipomtajia wazo la Muungano, Karume hakufikiri hata mara mbili. Pale pale alinitaka kuita mkutano wa waandishi wa habari kutangaza azma yetu. Nilimshauri asubiri kidogo kwani ilikuwa bado ni mapema mno kuweza kuviarifu vyombo vya habari’.’’

Kwa mujibu wa Seif Sharif Hamad, taarifa hizo ziliendelea kubaki kuwa siri hadi Aprili 26, 1964 pale Redio ya Tanganyika ilipotangaza kwamba siku hiyo marais wawili hao wangekutana katika Bunge la Tanganyika kubadilishana Hati za Muungano ambazo zimeunganisha Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja. “Hivyo inaonekana wazi kwamba tokea awali Muungano huu ulikosa ridhaa ya watu. Haukuwa Muungano wa watu, ulioundwa na watu, kwa maslahi ya watu. Bali ulikuwa na umeendelea kuwa ni Muungano uliosimamishwa kwa ridhaa ya watawala pekee. ’’

Katibu huyo mkuu wa CUF katika mada hiyo anaelezea mtazamo wake na hata kutumia maandiko na mitazamo ya watu wengine kuhusu kiini na matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kuanzia tafsiri ya mkataba wenyewe na hasa kuhusu mfumo wa muungano na mambo ya muungano yaliyomo kwenye mkataba.

“Ukitazama kwa jicho la sheria, kiini cha matatizo ya Muungano kinatokana na tafsiri ya Mkataba wa Muungano wa 1964. Hizi ndizo hati zinazounda, kupitia mkataba wa kimataifa, Jamhuri ya Muungano. Suala kubwa lililoumiza na linaloendelea kuumiza vichwa vya wengi na hivyo kuendelea kuulizwa ni mfumo gani wa Muungano ulikusudiwa kuwekwa na Mkataba huu? Ni muungano wa moja kwa moja (unitary) au wa shirikisho (federal)?

“Mfumo uliopo sasa ambao ulianza kutekelezwa 1964 ni ule wa serikali mbili – ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar. Tanganyika haikuwekewa serikali yake tofauti; madaraka yake kwa yale mambo yasiyo ya Muungano yalielezwa kwamba yatasimamiwa na kuendeshwa na Serikali hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, uhalali wa kisheria wa muundo huu umeendelea kuhojiwa na hata kupingwa kwamba hauwakilishi ipasavyo makusudio yaliyomo katika Mkataba ulioanzisha Muungano wenyewe.

“Mkataba wa Muungano wenyewe hauelezi bayana aina au mfumo wa Muungano inaouanzisha lakini uko wazi kuhusiana na mgawanyo wa madaraka inaouweka na idadi ya mamlaka (number of jurisdictions) zitakazokuwepo. Ibara ya (iii) (a) ya Mkataba huo inaanzisha ‘Bunge na Mamlaka ya Utendaji’ (Parliament and Executive) ndani ya na kwa ajili ya Zanzibar ikiwa na mamlaka kamili kuhusiana na mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa Zanzibar. Kwa upande mwingine, ibara ya (iv) ya Mkataba huo inaanzisha ‘Bunge na Mamlaka ya Utendaji’ (Parliament and Executive) ya Jamhuri ya Muungano ikiwa na mamlaka kamili katika eneo lote la Jamhuri ya Muungano kuhusiana na mambo ya Muungano na, pia, ikiwa na mamlaka kamili ndani ya, na kwa ajili ya Tanganyika kuhusiana na mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa Tanganyika. Kwa hivyo, katika sehemu ya pili, mamlaka mbili tofauti zimechanganywa pamoja.

“Mjadala mkubwa na mkali umekuja kuhusiana na tafsiri ya ibara hiyo ya (iv) na kule kuchanganya kwake mamlaka mbili hizo. Haya si masuala ya kisheria tu kama ambavyo baadhi yetu wanataka tuamini (ingawa nayo ni muhimu mno kama ilivyodhihirika hivi karibuni), bali pia ni masuala ya kisiasa kwa vile yanahusisha uwezo wa maamuzi, madaraka na mamlaka, na zaidi mchango wa gharama za uendeshaji na mgawanyo wa raslimali na mapato kati ya wahusika wakuu. Mambo haya, katika uzoefu wa nchi za wenzetu, ndiyo yaliyopelekea kuvunjika kwa miungano yao kwani huzaa kutiliana shaka na kutokuaminiana. Kwa vile yanachukua sura ya kisiasa (kutokana na sababu nilizozitaja), haya hayana chama wala itikadi kama nitakavyoonyesha huko mbele. Kama alivyowahi kusema Profesa Issa Shivji: ‘Mwisho wa yote, suala la Muungano linabakia kimsingi kuwa ni suala la kisiasa, na inapofikia kwenye siasa hasa, hotuba na kauli kali za jazba kuhusiana na mahusiano ya damu na ya kidugu, zote hazitafaa kitu.

“Kwa hakika, kinyume na inavyojaribiwa kuonyeshwa na wengi kwamba Tanganyika imepoteza kila kitu katika muundo huu wakati Zanzibar imekabidhi sehemu tu ya madaraka yake, muundo wa Serikali mbili umepelekea wengi kuamini kwamba kilichofanyika ni kiini macho tu kwani ni Zanzibar iliyokabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano. Na haya si maoni ya ngumbaru (kwa lugha ya Mwalimu Julius Nyerere) bali ni maoni ya watu wazito wakiwemo aliyekuwa Spika wa Bunge na ambaye sasa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ambaye alisema kwa jinsi mambo yalivyofanyika, Zanzibar inaonekana kama vile ni ‘invited guest’ (mgeni aliyealikwa) katika Muungano. Naye msomi mashuhuri ulimwenguni, Profesa Ali Mazrui alisema baada ya Muungano Zanzibar imepoteza kila kitu muhimu wakati Tanganyika imebadilika jina tu na kuwa Tanzania huku ikiwa na mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake, nembo yake ya Taifa, wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa Mataifa.”

Seif Shariff Hamad anazungumzia pia kwamba Mkataba wa Muungano haukufuta Serikali ya Tanganyika, kwa kuwa hakuna kifungu chochote kilichotoa maagizo ya kufutwa kwa serikali hiyo.

“Katika makubaliano ya kimataifa yaliyounda Muungano, ambayo hata hivyo katika muda wote wa uhai wa Muungano yamekuwa hayafuatwi, hakuna kifungu hata kimoja kilichotoa au kuagiza kwamba Serikali ya Tanganyika ifutwe kwa mujibu wa makubaliano hayo. Serikali ya Tanganyika, kama ilivyo ile ya Zanzibar, imelindwa na kifungu cha (v) kinachosomeka kwamba: “The existing laws of Tanganyika and of Zanzibar shall remain in force in their respective territories”. Kinachosemwa hapa ni kwamba ‘Sheria zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kufanya kazi na kuwa na nguvu katika maeneo yao.’

“Wataalamu wa katiba na sheria wanafahamu kwamba katiba ndiyo sheria mama ya sheria zote za nchi. Hivyo Katiba ya Tanganyika imelindwa na inapaswa kuwepo na Serikali yake iwepo, pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo yasiyo ya Muungano. Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la Tanganyika kwa yale mambo yaliyokuwa hayamo kwenye Muungano kama ambavyo Katiba (au kabla ya hapo Matangazo ya Kikatiba – Constitutional Decrees) na sheria za Zanzibar zinavyotumika katika eneo la Zanzibar kwa yale mambo ambayo si ya Muungano. Hiyo ndiyo tafsiri ya ‘maeneo yao’.

“Wazanzibari wanafahamu kwamba Serikali ya Tanganyika imefutwa kwa makusudi na Bunge la Tanganyika kinyume na Makubaliano ya Muungano ili kujipa nafasi kuitumia Serikali ya Muungano, kama kwamba ndiyo Serikali ya Tanganyika. Lengo ni hatimaye kuiua Serikali ya Zanzibar na kufanya Tanganyika mpya ikiwa na jina jipya la Tanzania lenye mipaka mipya, yaani kuwa nchi moja yenye Serikali Moja.

Itaendelea..

Raia Mwema
Disenba 17, 2008