Wednesday, December 17, 2008

Miaka Mitatu Ikulu: Rais akipunguza kasi, hatokwepa lawama

NAENDELEA na tathmini yangu ya Uongozi wa Awamu ya Nne wa Rais Jakaya Kikwete. Katika miaka mitatu tunaona, kuwa pamoja na dhamira njema ya Rais aliye madarakani, dhamira ya kutaka kutuongoza Watanzania ili tujitoe hapa tulipo, na kupiga hatua za maana na za haraka za kimaendeleo, bado anakwamishwa na baadhi ya watendaji wanaomzunguka.

Watendaji walio mbali na uhalisia, na baadhi ya watendaji walio chini, ni wale wenye kuiga matendo maovu ya watendaji waandamizi, baadhi ni wenye kumzunguka Rais.

Kama Rais aliye madarakani atapunguza kasi ya kuwashughulikia watenda maovu, basi, hataepuka lawama. Wengine tutabaki kuwa 'wapiga zumari'. Mwenye wajibu wa mwisho wa kukamata fagio na kusafisha uchafu unaomzunguka ni yule anayezungukwa na uchafu huo, maana yu karibu na fagio.

Wiki iliyopita nilimalizia kwa sentesi yenye kuhoji na kuwaachia wasomaji swali la kujiuliza na kutafakari. Niliandika; wenye kutumia madaraka yao vibaya na kufuja mali ya umma wanafanya hivyo kila siku. Hivi hawana uchungu na nchi yao? Na labda ni kwa kufanya mambo kwa mazoea tu, lakini katika karne hii ya 21, je, bado hatuoni kuwa msafara wa kiongozi mwandamizi wenye magari 30 ni ufujaji mkubwa wa rasilimali za nchi?

Nitasimulia kisa cha mzungu mmoja Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Kigeni. Mheshimiwa huyu alipata kunipa maelezo mafupi na kisha kuniuliza kwa kushangaa; Mheshimiwa yule alitoka kwenye moja ya nchi zinazotufadhili. Alikubaliana na afisa mmoja wa asasi isiyo ya Kiserikali ya Kitanzania, wakutane wakiwa safarini kwenda ughaibuni. Asasi ile ilipata misaada kutoka Shirika la misaada analoliongoza mheshimiwa huyo.

Kilichomshangaza Mkurugenzi yule ni kushindwa kwa wawili wale kufanya mazungumzo kwa vile yule Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Tanzania alipanda ndege daraja la kwanza na yule mzungu alibaki daraja la kawaida (Economy Class).

" Hivi unaweza kunifafanulia mantiki ya kitendo cha Mtanzania mwenzako yule?" Aliniuliza Mkurugenzi yule wa Shirika la Misaada.

Na hapa kuna mfano mwingine. Mwaka jana nikiwa mitaa ya jiji la Dar es Salaam nililiona barabarani gari la Mkuu wa Mkoa ulio mpakani kabisa na nchi ya jirani. Nikasoma magazetini kuwa mteule huyo alikuwa jijini kuhudhuria harambee ya kuchangisha fedha za elimu kwa mkoa wake.

Nilijiuliza; hivi ni kweli Mkuu huyo wa Mkoa alisafiri kwa gari lake hilo kwa siku mbili au zaidi kutoka makao makuu ya mkoa wake hadi Dar es Salaam? Kwa uchache, gharama za kuendesha gari lile hadi lifike Dar es Salaam ni shilingi milioni moja kwa kwenda na kurudi. Hapo hatujapiga hesabu ya gharama nyingine ikiwamo posho za njiani za mteule na dereva wake.

Na yawezekana kabisa, kuwa Mkuu wa Mkoa yule alipanda ndege kwenda Dar es Salaam na kumwamuru dereva wake aendeshe gari kutoka mkoani hadi Dar es Salaam alimradi tu mteule akiwa jijini avinjari akiwa na gari lenye kutambulisha cheo chake. Kwa mteule huyu, hajawa Mkuu wa Mkoa kama gari lake halijawa na sahani ya namba yenye kusomeka " RC XX"!

Naam! Mteule anaruka angani kwa ndege kutoka mkoa wa pembezoni na shangingi lake linakata mbuga kuitafuta Dar es Salaam! Je, kama mteule ametuma gari na kukaanga mafuta ya thamani ya shilingi milioni moja na zaidi kwa safari ya kwenda Dar es Salaam na kurudi kuchangisha fedha za elimu ya watoto wa mkoa wake, haoni kwamba milioni hizo zinazoteketea barabarani ni kodi za wananchi ambazo zingesaidia kuwasomesha watoto wa mkoa wake? Je, haikutosha kwake kupanda ndege kwa gharama isiyozidi shilingi laki tano kwa safari ya kwenda na kurudi na kwa saa chache?

Kwamba akiwa jijini ingekuwa nafuu kuazima gari jingine la serikali au hata kupanda teksi. Lakini, huu ni zaidi ya uzumbukuku. Na wala si kwa mteule niliyemtolea mfano tu, hali hii imezoeleka kwa baadhi ya wateule wetu. Ni hulka ya kupenda sana utukufu. Lakini inachangiwa pia na hulka ya kupenda kujipendelea, kuendekeza ubinafsi na kutokujali maslahi mapana ya taifa. Maana, mteule huyu, kama ni kwa fedha za mfukoni mwake asingekubali kusafiri kwa ndege kwenda Dar es Salaam na kisha kumwamuru dereva wake apeleke gari binafsi la mteule ili aje kulitumia akiwa Dar es Salaam! Asingeweza kufanya hivyo hata kama angeahidiwa kuchangiwa nusu ya gharama.

Naam. Majuzi hapa tumemsikia Waziri Mkuu Mizengo Pinda akikemea vitendo vya watendaji wa Wilaya na Mikoa kutokukaa ofisini. Alikemea pia semina zisizoisha. Alikuwa sahihi, lakini hata hapa tunaona umuhimu wake kukemea urefu wa misafara kwenye ziara zake za kikazi. Misafara mirefu ina maana ya watendaji wengi walioziacha ofisi zao kwenda kushuhudia kiongozi mwandamizi anapofanya kazi zake.

Katika taratibu za sasa, tuchukue mfano wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya Waziri Mkuu kwenye moja ya mikoa yetu. Hata kama ziara hii tutaiita ni ya kikazi, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kazi kusimama katika baadhi ya idara za serikali. Kama mheshimiwa atatua kwa ndege saa nne asubuhi, basi, hakuna huduma zitakazotolewa kwa wananchi siku hiyo. Kila mtendaji unayemtaka akusaidie atakujibu " leo tuna ugeni wa mheshimiwa!".

Kwa ufupi siku hiyo imekatika bila watu kuwa ofisini. Tuje sasa kwenye shughuli nzima ya kumpokea mheshimiwa. Kwa kawaida viwanja vingi vya ndege katika mikoa yetu hujengwa kiliomita 15 au zaidi kutoka makao makuu ya mkoa. Kwa uchache, msururu wa magari 20 utaanza kwenda kumpokea mheshimiwa saa moja au mbili kabla ya mheshimiwa kutua. Kwa safari ya kwenda uwanjani na kurudi, kila gari litatumia kwa uchache shilingi 50,000 za mafuta.

Na hapa inafuatwa kanuni ya kila mteule na dereva wake na pengine kabendera kake. Hakuna mteule atakayekuwa tayari kukaa kiti cha nyuma kwenye gari la mteule mwenzake wakati serikali imempa gari na dereva wake wa kumwamrisha twende huku , twende kule! Akiomba lifti, wateule wenzake watamshangaa.

Kwa uchache, orodha ya wateule watakaoumlaki mheshimiwa inaweza kuwa na Mkuu wa Mkoa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, DED, DAS, Meya, Ma-DC wa Wilaya zote za Mkoa, Wakurugenzi wa Idara, Madiwani wa Halmashauri, na wakati mwingine wakuu wa mikoa ya jirani nao hufunga safari kutoka kwenye vituo vyao vya kazi kwenda kwenye mkoa wa jirani "kumlaki" mheshimiwa.

Katika hali hii ngumu ya kiuchumi tumefika mahali kama zinavyofanya nchi nyingine zinazoendelea na zilizoendelea, tuangalie uwezekano wa serikali na mashirika ya umma kuwa na aina mbili tofauti za magari; yale yanayotumika mijini na yenye kubana matumizi ya mafuta na gharama za uendeshaji na yatakayotumika kwa safari za nje ya miji.

Kuwepo na "pool" ama yadi ya magari ya serikali kwa shughuli za nje ya miji ambapo watendaji watalazimika kwenda kuchukua magari hayo kwa safari hizo na kuyarudisha kwenye yadi baada ya ziara zao za kikazi. Kwa mantiki hiyo, kutakuwapo na idadi ya kutosha ya magari yatakayokuwa chini ya udhibiti wa serikali na kutumika na idara yeyote ile ya serikali pindi yatakapohitajika kwa safari za nje ya miji.

Hatua kama hiyo, itaipunguzia serikali mzigo wa gharama za uendeshaji na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kitakachotumika kuwasaidia Watanzania. Na katika kuyaandika haya, kuna watakaojisemea moyoni na kuniuliza kwa kunidhihaki; " Kwani hiyo diseli unalipia wewe bwana?"

Itaendelea.



0754 678 252
mjengwamaggid@gmail.com
http://mjengwa.blogspot.com