Frank Moyo
NDANI ya miaka 51 ya uhuru, kuna mambo mengi ya maendeleo yamefanyika. Kwa mfano, kuna ajira nyingi, rasmi na zisizokuwa rasmi, zimejitokeza. Wakati huu vijana wengi tumejiajiri kwenye usafiri wa bajaj, hii inasaidia kujikimu kimaisha.
Siyo kwamba tunapata fedha nyingi, lakini tunaweza kujikimu tu kimaisha.
Hata hivyo naweza kusema kuwa bado nchi yetu haijaendelea kama zilivyo nchi za wenzetu. Wenzetu wana treni zinazopita chini ya ardhi, wana barabara za angani (flyovers). Sisi bado reli na barabara ni zile zile tu.
Nashauri Serikali iwaangalie na wananchi walio katika ajira zisizo rasmi kwa kuwa ndiyo wengi kuliko watumishi wa umma na wafanyakazi walio katika sekta rasmi.
Serikali pia iimarishe miundombinu kama reli na barabara ili kuongeza maendeleo.
Japhet Kanyika
SAWA tumepata uhuru, lakini ni wa maneno tu. Hakuna uwajibikaji wa kweli wa kuleta maendeleo.
Kwa mfano elimu yetu tangu tumepata uhuru bado haijazaa matunda katika jamii. Watanzania wengi hawana elimu ya kuwawezesha kueleza kero zao, ukilinganisha na raia wa Kenya ambao wanajua haki zao kwetu bado.
Utakuta mtu hajui hata haki zake au anashindwa kueleza shida yake, mwisho anabaki na umasikini wake.
Kwa upande mwingine, ukiangalia maeneo ya vijijini, vijana wengi wamejiajiri kwenye biashara ya bodaboda, lakini hawana mafunzo ya kutosha ya biashara hiyo.
Isitoshe Serikali inaweka ukiritimba kwa vijana, mfano kijana akihitaji leseni ambayo gharama yake ni Sh40, 000 tu, atazungushwa hadi anajikuta ametoa Sh200, 000.
Kwa upande wa kilimo, mimi ni mkulima natoka wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Wakulima wengi hawana elimu ya kilimo, matokeo yake wanalima mashamba makubwa bila utaalamu, hivyo kuishia kupata mazao kiduchu. Wanatumia nguvu na fedha nyingi lakini hakuna cha zaidi wanachopata.
Nashauri Serikali iwekeze kwenye elimu ili wananchi wajikwamue kiuchumi.
David William
MIAKA 51 ya uhuru, bado hatuna la kujivunia kwa sababu vijana wengi hatuna ajira. Ukiacha vijana waliosoma hadi vyuo vikuu, lakini wengi wetu hatuna cha kufanya, tumebaki na umasikini mtupu.
Mimi ni mwanamichezo na nimechezea timu za Kombaini ya Makuburi na Simba ‘B’, lakini nimeshindwa kuendelea kwa sababu ya mazingira magumu. Sina uwezo wa kujikimu kimaisha wala kujikita kikamilifu kwenye michezo.
Hilo ndio tatizo linalotukumba sisi vijana. Naamini kabisa kwa kipaji changu hiki cha michezo ningefika mbali, lakini kwa umasikini huu nimeshindwa.
Serikali haina mkakati wowote wa kutukwamua vijana, ndiyo maana sioni faida za kusheherekea uhuru.
Kwa sasa najishughulisha na biashara ya taxi ili kujikimu kimaisha hata kama ndoto yangu ya kuwa mwanamichezo imepotea.
Naishauri Serikali iwekeze kwenye michezo kwa kutambua vipaji vya vijana na kuviendeleza. Waanzishe shule za soka na michezo mingine.
Huko ndiko tutakapotokea, siyo lazima vijana wote tukae ofisini, hata huku mitaani tunaweza kujikwamua. Kwa nchi za wenzetu wanamichezo wanalipwa vizuri kuliko hata maofisa wa Serikali.
Saleh Mpiga
NI kweli katika miaka hii 51 ya uhuru kuna mafanikio mengi yaliyopatikana. Uchumi umekua, kilimo kimeimarika, barabara zimejengwa na miundombinu mingine, ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Lakini bado kuna tatizo la ajira kwa vijana. Wengi hatuna ajira tunaishi maisha ya kubahatisha. Kibaya zaidi hata vijana waliosoma vyuo vikuu hawana ajira.
Chanzo cha tatizo hili ni utandawazi ambapo raia wa mataifa mengine wanakuja na kuchukua ajira zetu. Ukifuatilia utaona elimu zao ziko juu, sisi tunaishi kwa ujanja tu.
Tatizo jingine liko kwa viongozi wetu ambao wamekalia kujilimbikizia mali kuliko kujali maslahi ya umma. Wananchi wengi wanataabika kwa umasikini lakini wao wanafaidi kwa maisha ya anasa.
Ally Juma
KWA kweli mimi bado sijaona matunda ya uhuru, ikiwa hadi leo, wakulima vijijini wanakosa hata matreka ya kulimia.
Serikali imeshindwa kupeleka matrekta ili kuwasaidia wakulima, matokeo yake wanalima kwa kubahatisha tu na bei za vyakula zinakuwa juu kwa sababu kilimo hakijaboreshwa.
Mimi nimetokea Mzumbe, Morogoro ambako nilikuwa mkulima. Kule matrekta yanamilikiwa na watu wachache. Mbunge wetu alikuwa na matrekta yake ambayo hayakuwa yakitumia na wananchi wote.
Tunashindwa kuelewa kwa nini Serikali isipeleke matrekta hayo kwa Serikali za vijiji ili wananchi wachangie tu gharama za mafuta. Lakini kwa hali ya sasa mkulima atapata wapi fedha za kukodi trekta ili alime?
Hiyo ndiyo sababu ya vijana wengi kukimbilia mijini kutafuta vibarua. Ni tatizo la kitaifa.
Mimi sasa nimejiajiri kama dereva wa taxi. Tumeunda umoja na tuna mfuko wetu tunaokusanya fedha kwa ajili ya kukopeshana. Ila bado tunatafuta mfadhili wa kutuongeza mtaji, ili tupate mikopo ya maendeleo. Huo ndiyo ukombozi kwa vijana wasio na mitaji.
Naishauri Serikali iwekeze kwa vijana ili kuleta maendeleo ya kweli.
Zainab Kapoma
MAFANIKIO yaliyopatikana kwa miaka 51 ya uhuru kwa kweli yananichanganya. Hakuna kitu kinachoniuma kama vijana wetu wanaosoma hadi vyuo vikuu kukosa ajira, eti kwa sababu tu hawana uzoefu. Atapataje uzoefu wakati ndiyo katokea shule?
Wazee wanang’ang’ania madarakani huku vijana wakisotea ajira kwa muda mrefu. Watu wamekuwa madarakani tangu tupate uhuru lakini wamo tu. Sana sana wanawaachia watoto wao, huku vijana wengi wenye sifa wakisota tu.
Ndiyo maana nasema sioni mafanikio ya uhuru. Labda hilo treni waliloleta hapo juzi, kwa sababu tumekuwa wa kwanza kwa Afrika Mashariki na kati kuwa na treni la abira jijini Dar es Salaam.
Lakini nashauri kuwepo kwa utaratibu kwa vijana wenye elimu kupewa ajira haraka, siyo kwa watoto wa vigogo peke yao.
No comments:
Post a Comment