Wednesday, December 5, 2012

Wakili: Korti ilikosea kumvua Lema ubunge

WAKILI wa Serikali Mkuu Timon amedai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilikosea kutengua ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, kwa madai ya kutumia lugha za matusi kwa kuwa Bunge limeruhusu wanasiasa kutukanana kwenye kampeni.

Wakili Vitalis alitoa madai hayo jana, wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Lema, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),katika Mahakama ya Rufani jijini  Dar es Salaam.
Wakati wakili huyo wa serikali akitoa madai hayo, Wakili wa wajibu rufaa, ambao walishinda katika kesi ya msingi, Alute Mughway, naye alidai kuwa Mahakama Kuu, Arusha ilikosea katika uamuzi wake, pamoja na mambo mengine, kwa kukataa baadhi ya madai yao.
Lema alivuliwa ubunge April 5, 2012, katika hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalia, kufuatia kesi iliuyofunguliwa makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Lema kupitia kwa Wakili wake Method Kimomogoro alikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini Novemba 8, 2012 mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kuini kuwepo kwa dosari za kisheria, kutokana na pingamizi lililowekwa na upande  wa wajibu rufaa.
Hata hivyo mahakama hiyo ilimpa nafasi nyingine ya  kukata rufaa tena baada ya kumpa siku 14 kufanya marekebisho ya dosari hizo za kisheria na kuiwasilisha mahakamani ndani ya muda huo, amri ambayo aliitekeleaza.
Wakati Lema akikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kumvua ubunge, wajibu rufaa nao walikata rufaa (Cross Appeal) kupinga uamuzi wa mahakama hiyo, huku wakibainisha hoja nne.
Katika hoja ya kwanza hadi ya tatu walidai kuwa Jaji alikosea katika hukumu yake kwa kuchanganya vituo vilivyotolewa ushahidi na mashahidi wanne na hatimaye akakataa ushahidi wapo, pamoja na tarehe za ratiba ya kampeni ya CCM nay a Chadema.
Hoja ya nne walidai kuwa Jaji alikosea kwa kuamua kuwa hata kama Lema kwenye kampeni zake alidai kuwa Dk. Buriani ni mkazi wa Zanzibar hatafaa, wakidai kuwa ukazi si sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge.
Hatimaye rufaa hizo zilisikilizwa jana na jopo la   Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lililoundwa na Jaji Salum Massati, Jaji Bernard Luanda, chini ya uongozi wa  Jaji Nathalia Kimaro.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mawakili wawili ambao ni ndugu, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu na kaka yake Mghway, walipambana vikali kwa hoja za kisheria.
Lisu, Kada wa Chadema ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alikuwa akimtetea Lema mrufani (Lema), akisaidiana na Wakili  Method Kimomogolo, huku Mughway akiwatetea wajibu rufani ambao ni makada wa CCM.

No comments: