Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),
umetoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa madawati yaliyowekwa katika
vituo mbalimbali vya polisi nchini, ambayo yanatetea haki za jinsia
yanasimamiwa kikamilifu ili kupunguza unyonyaji na unyanyasaji nchini.
Wito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya,
jijini Dar es Salaam katika mjadala wa kupinga ukatili wa kijinsia,
kauli mbiu ya mtandao huo ni ‘Tokomeza Ukatili wa Kijinsia, Jitokeze
kutoa maoni ya Katiba Mpya’.
“Madawati haya yawe ni ya kusaidia na kukomesha ukatili wa kijinsia,
hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba kesi zote ambazo
zinafunguliwa zinasimamiwa kikamilifu,” allisema Mallya.
Usu alisema Mikoa ya Singida na Mara inaongoza kwa kiasi kikubwa kwa
ukatili wa kijinsia hususani katika suala la ukeketaji na sababu
nyingine ambayo inachangia ni ukosefu wa mgawanyo sawa wa matumizi ya
rasilimali za taifa.
Alisema ukatili wa kijinsia una sura tofauti na kwamba hali hiyo
inaongezeka kila uchao kutokana na kutokuwepo kwa sera makini za
kiuchumi zinazowalinda wanawake katika kumiliki mali.
No comments:
Post a Comment