KUJIRUDIA kwa matukio ya polisi kutumia silaha za moto dhidi ya
raia, kumepokewa kwa hisia tofauti, huku Mwanasheria Mkuu wa Kwanza wa
Serikali, Jaji Mark Bomani akilitaka jeshi hilo kuacha kutumia nguvu
wanapokuwa katika operesheni zao.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kuhusu tukio
la hivi karibuni la kupigwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la
Tanzania Daima, watu wa kada mbalimbali walisema, kitendo cha polisi
kutumia nguvu sio busara.
Jaji Bomani kitendo cha polisi kutumia nguvu
badala ya busara katika operesheni zao kinaweza kuleta uhasama kati ya
wananchi na jeshi hilo.
“Kwa ujumla matumizi ya nguvu kwa polisi si mazuri na nadhani tunatakiwa kubadilika katika hilo.” alisema Jaji Bomani.
Bomani alieleza kuwa kwa ujumla polisi wanatumia
vibaya silaha zao ingawa bado hajapata uhakika wa jinsi tukio la
kujeruhiwa kwa Matutu lilivyokuwa .
Alisema tukio la Mwangosi lilikuwa baya zaidi
lakini picha anayoiona na kuihusisha na tukio la juzi, ni kuwa kuna
matumizi mabaya ya mashambulizi ya polisi kwa raia.
Hata hivyo wakati Jaji Bomani akieleza hayo
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu
Amiri Ramadhan Manento alisema kila tukio linalofanywa na polisi
linatakiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kuanza kulizungumzia.
Jaji Manento alisema akiwa ni mwanasheria hawezi
kutoa hitimisho ya tukio la kujeruhiwa kwa Matutu kabla ya uchunguzi wa
kisheria kufanyika.
“Tunahitaji kujua mambo mengi, ya michakato ya
makosa ya jinai, (criminal procedure) kwa mfano polisi walipoingia
walifanya nini, walipotoka, ni maneno gani walimuuliza mtu wa kwanza
waliyekutana naye.
Tunahitaji kujua iwapo walitumia kizuizi cha usalama(safe cage) katika silaha zao au la” alisema Jaji Manento
Alisema kulingana na taarifa zilizopo katika
magazeti bado unahitajika uchunguzi wa kujua ni namna gani polisi
waliingia ndani ya nyumba hiyo.
Aidha Jaji huyo mstaafu alisema hawezi kuwahukumu
polisi moja kwa moja kwani hakuna ushahidi kuwa walikuwa wakimwinda
mwandishi, bali inawezekana waligundua kuwa ni mwandishi baada ya
kumjeruhi.
No comments:
Post a Comment