Thursday, April 19, 2012

Vifo vya watoto wachanga Tanzania vyapungua

TANZANIA imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 453 hadi 200 kwa kila watoto zaidi ya 100,000 kutoka mwaka 1990 hadi 2010.

Hata hivyo, mwaka 2010 vifo vya kinamama vimepungua kutoka 454 kwa kila wajawazito 100,000 hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za kutoa elimu ya uzazi inaleta matokeo mazuri.

Hayo yalisemwa juzi na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal wakati alipozindua Mkutano wa 26 wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), wenye lengo la kuangalia Malengo ya Maendeleo ya Milenia yamefikiwa pamoja na kujadili magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.

Dk. Bilal alisema vifo hivyo vimepungua kutokana na elimu inayotolewa kwa kinamama juu ya kuwahi hospitalini mapema ili wajifungue kwa usalama na kuokoa maisha ya watoto wachanga.

Alisema kwa upande wa malaria, Tanzania pia imepiga hatua kutokomeza ugonjwa huo hususan kutoa elimu juu ya kujikinga pamoja na kuhakikisha kinamama na watoto wanapata vyandarua.

“Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya kinamama na watoto, lakini bado tuna changamoto mbalimbali katika sekta ya afya hususan magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza hivyo Serikali inajitahidi kuhakikisha masuala ya utafiti wa magojwa yanafanyiwa kazi ili kujua ni magonjwa gani yanaongoza kuwaathiri wananchi ambao ndio nguvu kazi ya Taifa,” alisema Dk. Bilal.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwelecela Malecela alisema Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015 baadhi yamefikiwa kutokana na jitihada za Serikali kupunguza vifo vya watoto wachanga, vifo vya kinamama pamoja na baadhi ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.

Alisema wanafanyia utafiti wa magonjwa ya saratani hasa kwa vijana na watoto, na wanaendelea na utafiti wa magonjwa mbalimbali ili kuhakikisha magonjwa yasiyoambukiza yanapewa vipaumbele kama mengine.

No comments: