SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda, amewapoza mawaziri
kutokana na mashambulizi yaliyowakabili katika mkutano wa Bunge
ulioahirishwa juzi akiwataka wasijenge chuki na uhasama dhidi ya
wakosoaji.
Aidha, uelewa mdogo wa kanuni umeendelea kulisumbua Bunge, hali
ambayo Makinda juzi katika kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge,
aliwataka wabunge kusoma na kukariri kanuni hizo.
Akizungumzia nafasi ya wabunge na namna walivyoshambulia mawaziri
kadhaa, Makinda alisema yaliyosemwa ni kwa nia njema na hayapaswi kuwa
kiini cha chuki na uhasama.
Aliwataka mawaziri kutambua, kwamba wana dhamana na lengo la wabunge
ni kuhakikisha viongozi hao wanafanya vizuri katika utendaji wao.
Alisema wachangiaji wengi wanapotoa hoja zikiwamo za shutuma, dukuduku
lao huishia bungeni.
“Yaliyojadiliwa yote ni kwa nia njema. Isiwe kiini cha chuki na
uhasama. Msibebe chuki ndani ya roho zenu. Msichukue hasira mpaka
mkapasuka mifupa. Mnaambiwa namna ya kufanya kazi vizuri. Mkichukulia
kwamba ni uadui, mtapata shida,” alisema Makinda na kusisitiza juu ya
dhana nzima ya cheo ni dhamana kwa kuongeza: “Kama husemwi wamseme nani
na wewe ni Waziri?”
Akizungumzia umuhimu wa wabunge kuelewa kanuni, Makinda alitoa mfano
kwamba wapo wabunge waliompelekea barua wakitaka iundwe Kamati Teule
licha ya kwamba kanuni ziko wazi juu ya suala hilo.
Alisema Kiti cha Spika lazima kibebe lawama kutokana na wakati
mwingine kulazimika kutolea uamuzi wa masuala ambayo baadhi hawaridhiki
nayo, ikiwa ni pamoja na kulazimika kuchagua watu wachache wa kuchangia
hoja kutokana na idadi kubwa ya wabunge wanaojitokeza.
Wakati huo huo, alivitaka vyombo vya habari kufanya utafiti kabla ya
kuandika masuala mbalimbali akivitaka visishiriki katika ushabiki
unaojitokeza ndani ya Bunge, badala yake, vijikite kuchunguza.
Kauli ya Spika kuwaasa wabunge kutochukulia hasira yanayosemwa
bungeni, imekuja baada ya kujitokeza msuguano mkali baina ya wabunge na
mawaziri kadhaa, ambao walitakiwa kujiuzulu hali iliyosababisha
kuwasilisha taarifa ya nia ya kupiga kura ya kutomwamini Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ni miongoni mwa
mawaziri hao ambaye juzi katika kujitetea dhidi ya kuhusishwa na kashfa
ya ufisadi katika ugawaji vitalu vya uwindaji, aliishutumu Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, kuwa haikumtendea
haki.
Aliilalamikia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James
Lembeli (CCM), kwamba haikumshirikisha wala kumpa nafasi ya kujibu
tuhuma ilizozitoa juzi bungeni dhidi yake huku akisema “Mungu yupo”.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Lembeli, alimjibu Maige akimtaka ajibu
hoja badala ya kuzungumzia mchakato. Lembeli aliliambia Bunge, kwamba
Kamati ilifanya kazi kwa mujibu wa kanuni na yote yaliyo katika taarifa
yake, ni ya kweli.
“Nimtoe hofu Maige, kwamba Mungu ni mmoja, yupo kwa ajili ya watu
wote na kazi yake ni kusimamia haki... yako mengi ambayo hatukuyasema.
Kamati inasimamia wizara tatu. Kati ya hizo, wizara inayoipa shida ni ya
Maliasili. Imejaa watendaji walio na jeuri. Na pengine ndiyo maana hata
Maige hajapata taarifa ya Kamati yetu,” alisema Lembeli.
Taarifa ya Kamati ilihusu uchunguzi kuhusu utaratibu uliotumika
katika kukamata na kusafirisha twiga wawili nchi za nje na utaratibu
uliotumika kugawa vitalu vya uwindaji wa kitallii kwa msimu wa
2013-2018.
Naye Halima Mlacha anaripoti kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
kiko kwenye mchakato wa kuzungumza na vyama vingine vya upinzani vya
siasa, ili kufanya maandamano makubwa nchi nzima kumshinikiza Rais
Jakaya Kikwete awachukulie hatua mawaziri waliotuhumiwa kuhusika na
ubadhirifu bungeni.
Pia chama hicho kimemshauri Waziri Mkuu Mizengo Pinda ajiuzulu
kutokana na kutopatiwa nyenzo za kushughulikia sakata hilo na Rais
Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa
Lipumba, alisema amekuwa akipokea ujumbe mfupi kutoka kwa wanachama
mbalimbali wa chama hicho wakitaka yafanyike maandamano kushinikiza
hatua zichukuliwe dhidi ya mawaziri hao.
“Kwanza napenda kumpongeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kwa kufanikisha kutoa ripoti iliyofichua ubadhirifu na
wizi wa fedha za umma lakini pia nimesikitishwa na kushindwa kuchukuliwa
hatua dhidi ya mawaziri waliotuhumiwa,” alisema Lipumba.
Alisema kwa sasa kinachohitajika ni kwa Serikali kuwajibika katika
masuala yanayoibuliwa ya ubadhirifu wa fedha za umma. “Hili sakata la
juzi bungeni limeonyesha wazi kuwa mawaziri wanahitaji kuwajibika lakini
hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.”
Alisema kuwajibika kwa mawaziri hao kuko mikononi mwa Rais Kikwete
ambaye hata hivyo alishindwa kumpatia nyezo Waziri Mkuu za
kuwawawajibisha wale wote waliotuhumiwa bungeni kuhusika na ubadhirifu
na wizi wa fedha za Serikali.
“Ndio maana tunamshauri Pinda ajiuzulu yeye kwa kuwa yeye ndio
msimamizi mkuu wa mawaziri wengine wanapoharibu anapaswa kuwachukulia
hatua lakini hana nyenzo za kufanya hivyo,” alisisitiza.
Mawaziri hao ni Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.
Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu.
Mawaziri wengine wanaohusishwa na ubadhirifu huo ni Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika Dk. Jumanne Maghembe, Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja, Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, George Mkuchika na Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige.
No comments:
Post a Comment