Thursday, April 12, 2012

Upatikanaji huduma ya maji Kisarawe tatizo

Baadhi ya wakazi wa eneo la Kisarawe Mjini wakiwa wamepanga foleni ndefu za vyombo vya kutekea maji kwenye moja ya mabomba ya umma. Kumekuwa na shida kubwa ya upatikanaji wa huduma za maji kwa matumizi ya nyumbani na shughuli nyingine za wananchi eneo la Kisarawe hasa Kata ya Maneromango iliyopo nje kidogo ya mji huo. (Picha na Joachim Mushi wa Thehabari.com)


Na Joachim Mushi, Kisarawe

MGOGORO wa ukosefu wa maji ya matumizi ya nyumbani na shughuli nyingine bado ni kero kubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani hasa katika Kata ya Maneromango iliyopo nje ya Mji wa Kisarawe.

Uchunguzi uliofanywa na Thehabari.com hivi karibuni maeneo ya Kata ya Maneromango imebaini bado kuna shida kubwa ya maji kwa wakazi wa eneo hilo licha ya uwepo wa baadhi ya visima vya umma na watu binafsi vilivyochimbwa hivi karibuni.

Shida ya maji imepungua katika baadhi ya shule za msingi na sekondari pamoja na vituo vya afya pekee baada ya kujitokeza wafadhili kujenga mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua katika shule hizo na kituo cha afya.

Shule ambazo awali zilikuwa na shida kubwa ya maji na sasa zimenufaika na msaada wa kujengewa mfumo wa uvunaji maji ya mvua eneo la Maneromango ni pamoja na shule za msingi, Mengwa na Maneromango, Shule ya Sekondari Maneromango pamoja na kituo cha Afya cha Maneromango.

Akizungumza na mtandao huu Said Mzara mkazi wa Kijiji cha Boga amesema unafuu wa kupatikana kwa maji hutokea mvua zinaponyesha tu ambapo wananchi wengi hupata maji lakini baada ya kipindi hicho shida ya maji hurejea kama kawaida.

“Wanaonufaika kwa kiasi kikubwa na huduma za maji ni shule za msingi na sekondari pamoja na kituo chetu cha afya ambao wamejengewa mfumo wa kuvuna maji ya mvua, ukweli ni kwamba bado wananchi tunaitaji msaada wa kuboreshewa huduma za maji hasa visima vya umma,” alisema Mzara.

Muhamed Omar mkazi wa Kitongoji cha Msegamo anasema ushauri wa kuvuna maji ya mvua unaotolewa na wataalam na baadhi ya viongozi ni mgumu kwa wananchi wengi kutokana na kumiliki nyumba za nyasi ambazo ni hafifu kwa uvunaji maji ya mvua.

“Wanashauri tuvune maji ya mvua suala hili ni gumu kwa asilimia kubwa ya wakazi kwani bado tunamiliki nyumba za nyasi, isipokuwa kwa wakazi wa mjini sasa kwa hali hii utavunaje maji ya mvua?,” alihoji Omar ambaye ni mkulima na mfanyabiashara ndogo ndogo.

Mwandishi wa habari hizi ametembelea pia maeneo ya katikati ya Mji wa Wilaya ya Kisarawe ambapo amebaini bado kuna shida kubwa ya maji kutokana na kubaini foleni kubwa za maji katika maeneo ya mabomba ya maji.

Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)

No comments: