MGOMBEA wa ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari ameshinda katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Trasence Kagenzi, amemtangaza Nassari kuwa mshindi kwa kupata kura 32,672, na kumshinda mpinzani wake mkubwa, Sioi Sumari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura, 26,757.
Wananchi wa Arumeru Mashariki mkoani Arusha jana walipiga kura kwa amani katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge, na baada ya upigaji kura huo, matokeo ya awali yaliyobandikwa vituoni yalionesha mchuano mkali kati ya wagombea Joshua Nasari wa Chadema na Sioi Sumari wa CCM.
Matokeo ya awali jana, yalionesha kuwa Nasari alikuwa akiongoza katika vituo vya mjini wakati mwenzake Sioi alikuwa akitamba na kura nyingi katika maeneo ya nje ya mji wa Arumeru, katika mchuano mkali ambao unabashiri mshindi atapatikana kwa kumzidi mwenzake kura chache.
Upigaji kura ulianza saa moja asubuhi huku wapigakura wakionekana kumiminika kwa wingi katika baadhi ya vituo vya mji mdogo wa Usa River huku vituo vingine vikionekana kuwa na wapiga kura wachache, lakini baadaye ukaanza kuibuka vituko.
Hali ya ulinzi na usalama ilionekana kuwa shwari katika vituo vingi huku wananchi wakionekana kutii agizo la Polisi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) lililowataka kurejea makwao mara baada ya kupiga kura.
Katika matokeo ya awali, katika Shule ya Msingi Leganga, kituo cha kwanza CCM ilikuwa na kura 27 na kupitwa na Chadema iliyokuwa na kura 131. Kituo cha Pili CCM 26, Chadema 142; Ofisi ya Kitongoji cha Mji Mwema kituo cha kwanza CCM 23, Chadema 141; kituo cha pili CCM 52, Chadema 144, kituo cha tatu CCM 32, Chadema 125 na kituo cha nne CCM 126, Chadema 37.
Katika Kata ya Kikatiti Shule ya Msingi Chemchem, CCM 69, Chadema 104, kituo cha pili CCM 76, Chadema 101, kituo cha tatu CCM 59, Chadema 109, Kituo cha nne CCM 52, Chadema 139, kituo cha tano CCM 45, Chadema 105 na kituo cha sita, CCM 40 na Chadema 119. Kituo cha Leganga CCM 26, Chadema 142, kituo cha pili CCM 27 na Chadema 131.
Kituo cha Ngarasero kituo cha kwanza CCM 66, Chadema 93, kituo cha pili CCM 62, Chadema 93, kituo cha tatu CCM 51 na Chadema 116.
Katika kituo cha Kisambara kituo cha kwanza CCM 63, Chadema 116, kituo cha pili CCM 58, Chadema 113, kituo cha tatu CCM 60, Chadema 117, kituo cha nne CCM 53 na Chadema 118.
Awali kulijitokeza dosari mbalimbali ikiwemo ya baadhi ya mawakala wa Chadema kulalamikia kuzuiliwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura walivyopangiwa kwa saa kadhaa kutokana na kutokuwa na fomu maalumu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kukosa pia uthibitisho kutoka kwenye vyama vyao. Hata hivyo tatizo hilo lilishughulikiwa haraka na mawakala hao kuruhusiwa.
Kasoro nyingine ilikuwa ni kwa baadhi ya mawakala kulalamikia kutokuwa na madaftari ya orodha ya wapiga kura, hatua ambayo iliwafanya mawakala kuilalamikia Tume wakidai kuwa hatua hiyo inalenga kuwahujumu ili wasiwatambue wapigakura.
Msimamizi wa Uchaguzi huo, Trasias Kagenzi alisema jukumu la kuwapa mawakala madaftari ya orodha ya wapiga kura ni la vyama vyenyewe kwa vile tayari Tume ilikuwa imewasilisha madaftari hayo kwa vyama vyote.
Waandishi wa habari watano waliokuwa wakitoka katika Kata ya Ngarenanyuki kufuatilia upigaji wa kura, walipata ajali baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Ngarenanyuki kurejea Usa River kupinduka katika miteremko ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha.
Waandishi hao ambao walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Arumeru iliyopo Tengeru ambako walitibiwa majeraha yao ni Queen Lema wa Majira, Janeth Mushi wa Jambo Leo, Neema Kishebuka wa Tanzania Daima, Ashura Mohammed wa Redio Five na Grace Mbise wa Redio Sun Rise Arusha.
Wakati upigaji kura ukiendelea, Kagenzi alimuandikia barua Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe akiagiza chama hicho kuacha mara moja kutumia helikopta iliyotumika katika kampeni za chama hicho kupita katika vituo vya upigaji kura ili kuhakiki shughuli hiyo.
Kwa mujibu wa msimamizi huyo hatua hiyo ilihesabika kuwa ni ukiukwaji wa Sheria za Uchaguzi kutokana na sheria kutoruhusu vyama kufanya kampeni siku ya kupiga kura.
Kwa vile helikopta hiyo ndiyo iliyokuwa ikitumika katika mikutano ya kampeni ili kuwavuta wananchi, Kagenzi alisema ingeweza kuchukuliwa kama ilikuwa bado inafanya kampeni ya kuwashawishi wananchi kuichagua Chadema.
Hata hivyo, akizungumzia barua hiyo wakati upigaji kura ukiendelea pamoja na kukiri kuipokea, Mbowe alisema waliijibu mara moja barua hiyo wakimpinga Kagenzi kwamba wangeendelea kuitumia katika kuhakiki upigaji kura kwa vile sheria inaruhusu.
Mbowe alisema helikopta iliyokuwa inatumiwa na Chadema kwenye mikutano ya kampeni ilikuwa na maandishi yanayosomeka Chadema, lakini iliyokuwa inatumiwa jana kuangalia mwenendo wa upigaji kura katika vituo mbalimbali vya jimbo hilo, haikuwa na maandishi hayo wala alama yoyote ya Chadema.
Alisema kwa vile sheria inakiruhusu chama kutumia aina yoyote ya usafiri ikiwemo magari, pikipiki, miguu au baiskeli katika kuzunguka maeneo mbalimbali ya kupigia kura ili kuhakiki zoezi hilo, wao waliamua kutumia helikopta ili iwe rahisi kwao kufika katika maeneo yote ya jimbo kwa urahisi na kuhakiki upigaji huo wa kura.
Wakala wa Chadema atekwa Ilipofika saa 5.30 asubuhi vijana wasiofahamika wakiwa na gari ambalo halikufahamika mara moja namba zake za usajili walivamia kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Embaseni na kutoweka na mtu aliyetajwa na wafuasi wa Chadema kama wakala wa nje wa chama hicho.
Gazeti hili lilikuwepo katika eneo hilo katika Kitongoji cha Maji ya Chai ambapo wakala huyo aliyetajwa kwa jina moja la Maria au Mama Pendo mfanyabiashara wa Maji ya Chai alitekwa na watu hao wasiojulikana na kupakiwa ndani ya gari hilo na kupelekwa mahali kusikojulikana huku simu yake ikiita bila kupokelewa. Taarifa hizo zilipelekwa mara moja kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa aliyeahidi kulifuatilia.
Mwigulu azua tafrani Kulitokea utata baada ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa, Mwigulu Nchemba kuonekana katika kituo cha Polisi cha Usa River.
Wakati taarifa za awali zilisema Nchemba alikutwa akifanya kampeni katika Kanisa la AGT Kata ya Pori alikokwenda kuabudu kinyume na sheria, Nchemba akihojiwa katika Kituo cha Polisi cha Usa River alisema kilichotokea kanisani hapo ni kwa gari yake kuzingirwa na vijana wa Chadema waliotaka kumshambulia akapiga simu Polisi kuomba msaada.
Wakizungumza na waandishi wa habari mchana jana, Mkuu wa Kitengo cha Operesheni za Uchaguzi Arumeru Mashariki kwa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna Isaya Mngulu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye walithibitisha kwamba Nchemba ndiye aliyetoa taarifa Polisi akidai kuvamiwa.
Uchaguzi huo Mdogo umefanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari ambaye alifariki kwa ugonjwa wa saratani ya ubongo Januari 19, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment