Monday, April 23, 2012

Mbivu za Jairo, mawaziri leo

SERIKALI leo inaweka wazi bungeni ni namna gani imemwajibisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo ambaye alitiwa hatiani na Kamati Teule iliyomchunguza juu ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni.

Aidha, Mkutano wa Saba wa Bunge la 10 unaahirishwa leo huku macho na masikio yakiwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakitaka kufahamu hatima ya mawaziri wanaoshinikizwa kujiuzulu kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni ama kuhusika au kushindwa kudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma.

Kuhusu sakata la Jairo, taarifa ya Serikali juu ya utekelezaji wa maazimio ya Kamati Teule iliyotaka Jairo awajibishwe, itawasilishwa mezani kwa maana haitasomwa na wala kujadiliwa
na wabunge.

Hata hivyo, baada ya kuwasilishwa, itakuwa wazi kwa wabunge kufahamu yaliyomo hususan
hatua zilizochukuliwa.

Kamati Teule iliundwa kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni.

Katika Mkutano wa Tano wa Bunge, Serikali ilipokea mapendekezo ya kamati hiyo iliyomtia hatiani Jairo kuwa alichokifanya ni kinyume cha utaratibu wa Serikali. Ilipendekezwa awajibishwe.

Katika hatua nyingine, baada ya Kamati sita za Kudumu za Bunge kuwasilisha taarifa zake wiki iliyopita, leo itakuwa zamu ya kamati nyingine ikiwamo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Vile vile kesho Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango kujadili na kuishauri Serikali juu ya mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka
wa fedha 2012/2013.

Kuhusu shinikizo la kumwajibisha Waziri Mkuu, taarifa iliyotolewa jana kwa waandishi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), ilisema Mbunge wa Bariadi Mashariki,
John Cheyo (UDP) amegoma kusaini waraka wa kusudio la Azimio la kumpigia Waziri Mkuu kura ya kutokumwamini huku pia wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakitaka majina yao yasitajwe.

Kati ya saini 73 zilizopatikana, wamo wanaCCM watano na waliotaka watajwe ni Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe na Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola.

Watatu wametaka majina yawekwe hadharani leo baada ya taarifa rasmi ya kusudio husika
itakapowasilishwa kwa maandishi kwenye ofisi ya Spika.

“Mpaka leo (jana) orodha imetimiza idadi ya wabunge wazalendo wanaopigania uwajibikaji 75 kutoka vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni, isipokuwa chama cha UDPambacho
kina mbunge mmoja na hajatia saini waraka huo mpaka sasa,” alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni.

Zitto alisema leo wanawasilisha rasmi kwa Spika taarifa ya maandishi kwa mujibu wa Kanuni 133 (1) na (3) ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa kushindwa kusimamia
uwajibikaji wa Serikali Bungeni kwa mujibu wa Ibara ya 52 na hivyo kulinda mawaziri wenye kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na kulisababisha taifa hasara.

Kwa mujibu wa Zitto aliyeongozana na Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CUF, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya na wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR Mageuzi), wanatarajia kwamba siku 14 baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Bunge litakutana kwa haraka kuijadili ili kuwezesha uwajibikaji.

Wabunge hao wanaosema inapaswa uitwe Mkutano wa Dharura wa Bunge, wanasimamia Kifungu cha 4 cha Kanuni ya 133 inayosema, “hoja inayotolewa chini ya kanuni hii na iliyotimiza masharti ya Katiba, itawasilishwa bungeni mapema iwezekanavyo na itaamuliwa kwa kura za siri” ingawa kifungu hicho hakitaji ni siku ngapi zinapaswa zizingatiwe.

Kifungu hicho kinasema, ‘Endapo hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu itapitishwa na Bunge kwa kupigiwa kura na Wabunge walio wengi, Spika atawasilisha Azimio hilo kwa Rais mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile ndani ya siku mbili tangu Bunge lilipopitisha Azimio hilo, Waziri Mkuu atajiuzulu na Rais atamteua Mbunge mwingine kuwa Waziri
Mkuu.”

Katika hatua nyingine, Ikulu imekanusha taarifa ya gazeti la Tanzania Daima, toleo la jana lenye kichwa cha habari ‘JK alinda Mawaziri’ inayodai kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.

“Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Brazil, amerejea jana (juzi) Aprili 21, 2012 jioni. Hajaonana wala kufanya mazungumzo na Waziri
Mkuu, Mhe. Pinda.

“Hivi sasa Mhe. Rais anasubiri kupata taarifa rasmi kutoka Bungeni Dodoma,” ilieleza taarifa ya Ikulu. Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amewasili mjini Blantyre nchini Malawi jana jioni kuhudhuria maziko ya Profesa Bingu wa Mutharika, aliyekuwa Rais wa Malawi yanayofanyika leo. Alifariki Aprili 5, mwaka huu.

No comments: