Thursday, June 26, 2008

Mfululizo wa Semina za Jinsia na Maendeleo.

Jumatano wiki hii ya tarehe 25/06/2008 katika mfululizo wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) mada ilikuwa ni Juu ya Sherehe za Kitchen Party iliyowakilishwa na dada Agnes Mutayoba - Mratibu wa elimu wa Kata ya Mzizima na kuwezeshwa na dada Anna Kikwa. Lengo la Mada lilikuwa ni kujadili muundo wa sherehe za kitchen party zinazoendeshwa katika siku za hivi karibuni. Mtoa mada aliamua kutoa mada hii kutokana na utafiti alioufanya katika sherehe mbalimbali zilizofanyika katika jiji hili la Dar es salaam hivi karibuni.

Mtoa mada aliweza kuwachokoza washiriki wa semina kwa kuwauliza maana ya Kitchen Party ambao wengi walikubaliana kwamba ni mafunzo anayopewa Msichana/mwali kabla ya kuolewa ama pindi anapokuwa karibu ya kuolewa. Na karibia kila kabila lilikuwa na jina lake maalumu la mafunzo hayo. Kwa mfano, Wazaramo waliyaita Mkole. Pia mshirki kutoka USA alichangia na kusema kwao Kitchen party huwa ni sherehe ya kutoa zawadi kwa msichana anayekaribia kuolewa, na mara nyingi huandaliwa na wanawake wenye umri mkubwa kwa ajili ya binti yao.
Hivyo kitchen party tangu awali ilikuwa ni sherehe kwa ajili ya maandalizi ya Msichana anayekaribia kuolewa. Mtoa mada akatoa maswali saba ya uchokozi ya kutafakari kwa washiriki wa semina juu ya muundo wa sherehe za kitchen party za siku hizi. Washiriki walitakiwa kukaa katika makundi na kujadili maswali hayo saba, na mijadala iliyoibuka ni pamoja;
1. Je, Kitchen party ni sherehe inayoendana na mila na desturi za kabila husika?
Hapana, kwa sababu sherehe za siku hizi za kitchen party zipo kibiashara sana na hata wahusika hutumia lugha zisizostahili ili kuvutia biashara. Pia walimu wanaofundisha ni watu kutoka makabila mengine, hivyo haijali utamaduni na mila za kabila husika.

2. Sherehe za Kitchen Party zina mabadiliko yoyote?
Mabadiliko yapo wafundishaji hawana sifa, zipo kibiashara sana, mambo ya kufundishia ndani yanafanywa hadharani, na mafunzo yanafanyika kwa muda mfupi sana. Hivyo mafunzo haya yamepoteza dira.
3. Je umri Msichana anyepata mafunzo ya Kitchen party unalingana na elimu anayopewa?
Wasichana wanaweza kufika umri wa kutosha kufundishwa mafunzo hayo ama la, kwa sababu wapo wasichana wanaoozwa chini ya miaka 18, nao pia hupatiwa mafunzo hayo.

4. Kuna elimu nyingine ya ziada anayopewa msichana zaidi ya ile ya Kitchen party?
Ipo, wasichana wanapatiwa elimu mbalimbali za jinsi ya kwenda kuishi na waume zao, ukilingnisha na wanaume ambao ni mara chache sana kupatiwa elimu ya aina hiyo, kitu ambacho kinasababisha matatizo makubwa katika mahusiano yao.
5. Je kitchen party ni kitu cha kuiga au ni asilia?
Kitchen party ni kitu cha kuiga kutoka magharibi, ukilinganisha na sherehe za mafunzo ya zamani ya asili yalivyokuwa. Kuna mambo yameongezeka katika sherehe za siku hizi ikiwa pamoja na matumizi ya zisisokuwa na maadili, na umri wa washiriki katika sherehe hizo.
6. Iwapo msichana anapatiwa elimu ya kitchen party, mvulana anapatiwa elimu gani?
Mvulana hana elimu yoyote ya kuishi katika ndoa kutona na mabadailiko ya utandawazi, hivyo hupelekea kukosa maadili ndani ya ndoa yake. Zamani wavulana walipitia jando kabla ya kuoa na ilisaidia sana kuimarisha mahusiano ya ndoa.
7. Nini kifanyike badala ya Kitchen party?
Kitchen party inaweza ikawa na faida iwapo mambo kadhaa ya kisasa yakirekebishwa tofauti na hali iliyopo, ambapo imepoteza maana yake halisi.

Hitimisho.
Sherehe za kitchen party zinawadidimiza wanawake kwa sababu zinawachukulia muda mwingi katika maandalizi yake na kiasi kikubwa cha fedha. Pia inawadhalilisha wanawake kwa sababu mafunzo yanayotolewa hayazingatii maadili ya Mtanzania hasa katika uvaaji na mada zenyewe. Hivyo kuna haja ya kuangalia upya sherehe hizi ili ziweze kuleta manufaa katika zama hizi za utandawazi.

Picha za Wa-GDSS katika semina hiyo.


Mtoa Mada Bi. Agnes Mutayoba.


Sehemu ya Washiriki.

Washiriki wakiwa katika vikundi wakijadiliana.
Washiriki wakijadiliana.
Mshiriki akichangia mada.

Mshiriki akichangia mada.
Mshriki akichangia mada.

No comments: