Kikundi cha kufuatilia ukatili wa kijinsia na bajeti ya afya –hasa afya ya uzazi– katika Manispaa ya wilaya ya Kinondoni chakutana kwa kwa mara ya kwanza. Kikundi hicho kinachojumuisha asasi kumi na mbili zilizopo ndani ya Manispaa ya Kinondoni kiliundwa kutokana na semina juu ya Upimaji na Ufuatiliaji, ilifanyika tarehe 12 na 13 Juni, 2008. Semina hiyo iliyoandaliwa na TGNP na kuhudhuriwa na asasi za kijamii zipatazo 40 kutoka katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Dodoma, Pwani, Sumbawanga, Lindi, Manyara, Mtwara, Kilimanjaro, Unguja, Pemba na Morogoro. Lengo kuu la semina hiyo ilikuwa ni kuzipa asasi uwezo wa kutathimini na kufuatilia mambo mbalimbali katika maeneo yao. Pia malengo mengine ni pamoja na kuwajengea uwezo wa ushawishi na utetezi, kubadilishana uzoefu, kuimarisha mawasiliano, na kutengeza mitandao ya kufanya kazi kwa pamoja. Semina hiyo iliwezeshwa na Lilian Liundi (TGNP)-, Ananilea Nkya (TAMWA), na Salima Mauldi (Sahiba Sisters).
Baada ya semina hiyo washiriki waliweza kuunda mitandao ya kufanya kazi kwa pamoja kulingana na maeneo wanayotoka. Kila mtandao uliweza kupewa kazi maalumu ya kufuatilia na kutathimi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Ijumaa ya tarehe 20/06/2008 mtandao wa kutathimini utekelezaji wa bajeti ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia katika Manispaa ya Kinondoni uliweza kukutana kwa mara ya kwanza na kujadili jinsi ya kutekeleza jukumu lao. Asasi zinazounda mtandao huo ni; Precious Jewells Organization (PJO), Tanzania Women in Law and Advocacy (TAWLA), Tanzania Youth For Development (TAYOFODE), Makuburi Women Development Allowance (MWDA), Binti Leo, Kigogo Youth and Women Program (KYWP), Upendo Group, Victoria Agency Tanzania Trust (VTAT), Tanzania Policy Femele Network (TPENET). Mtandao huu unasimamiwa na TAWLA.
Mwenyekiti wa mtandao huu Harrieth Bandari kutoka MWDA na katibu wake Ms. Dorosta kutoka VTAT walifungua na kuongoza kikao. Baada ya kueleza kwa ufupi majukumu yao, wanamtandao walipata nafasi ya kujadiliana maswala mbalimbali muhimu. Wanamtandao walijadiliana juu ya shughuli muhimu ambazo walikubalina waanze nazo katika kukamilisha jukumu lao. Shughuli hizo muhimu ni pamoja na; Utafiti, Uelimishaji, Mafunzo, na Ushawishi na Utetezi. Walikubaliana wachague baadhi ya kata ndani ya Manispaa ya Kinodoni na kufanya utafiti juu ya hali ya ukatili wa kijinsia, hali ya upatikanji wa huduma za kiafya na uelewa wa jamii juu ya tatizo la ukatili wa kijinsia. Walikubaliana utafiti huo uanzie katika ngazi ya serikali ya mtaa na kufikia ngazi ya kikata. Pia walikubaliana waende katika vituo vya polisi, na mahakamani kuona na kupata maelezo na takwimu juu ya ukatili wa kijinsia ulivyo. Kuhusu uelimishaji walikubaliana waandae programu ya pamoja ya kuelimisha jamii juu ya tatizo la ukatili la kijinsia katika maeneo yatakayoonekana ni korofi zaidi baada ya kufanya utafiti. Pia walipendekeza watumie vyombo vya habari katika kuelimisha jamii.
Kuhusu Ushawishi na Utetezi hawakuweza kujadili mada hii kutokana na muda kwisha na hivyo kikao kuharishwa hadi tarehe 24/06/2008, ambapo walikubaliana itakuwa ni siku ya kumaliza ajenda zilizobaki na kugawana majukumu ya utekelezaji.
Kwa maoni yao wanamtandaoo wanaona changamoto zitakazo wakabili katika kutekeleza jukumu lao ni pamoja na ugumu wa kupata pesa za kutekeleza wajibu wao, kitu ambacho wanahisi kinaweza kukwamisha ari waliyonayo katika kufanikisha azima hii. Pia wanaona mtandao huu ni fursa ya pekee kwao katika kufanya kile ambacho wanahisi ni chenye manufaa kwa jamii na kwa muda mrefu walikuwa walihitaji nafasi ya kukitekeleza, na hivyo utaweza kutimiza ndoto zao katika kuleta usawa na huduma bora za afya kwa jamii.
Picha za Wanamtandao Kikaoni.
Wanamtandao wakijadiliana masuala mbalimbali katika kikao.
Kikao kinaendelea...
Picha ya pamoja ya wanamtandao.
1 comment:
Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wanamtandao wa kufuatilia Bajeti ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia kwa kuendeleza mapambano katika harakati za kuhakikisha bajeti ya afya inatumika ipasavyo. Tunawaomba wawe wantupa mrejesho katika kila hatua wanayochukua ili wanaGDSS tuweze kuiga mfano kutoka kwao na pia kuwapa mawazo wanapokumbana na changamoto.
Tunawatakia kila la heri katika harakati zenu.
Post a Comment