Thursday, June 19, 2008

SEMINA YA MJADALA WA MUSWADA WA BAJETI YA 08/09.

Utangulizi.
Mada juu ya tafakari na mapendekezo kuhusu bajeti ya 2008/09 je imekidhi matarajio yetu? Iliyowakilishwa katika semina za kila wiki za Jinsia na Maendeleo katika viwanja vya TGNP. Wiki hii ya tarehe 18/06/2008. Mjadala ulihudhuriwa na wanaharakati kutoka katika vikundi mbalimbali vya kijamii waliofikia 200 hivi na watoa mada wakuu walikuwa ni dada Gema Akilimali kutoka FemACT, mwakilishi kutoka UTU Mwanamke, na dada Mary kutoka Haki Elimu. Wawezeshaji waligusia mapungufu yaliyomo katika bajeti ya 08/09, ambapo watoa mada walitoa mapungufu ambayo wanaharakati waliyaona katika bajeti hiyo, na waligusia maswala ya msingi ambayo bajeti ya mwaka huu yalishindwa kutoa majibu ya kuridhisha na kuhitaji majibu ama marekebisho zaidi kabla ya mswada huo kupitishwa. Ripoti hii fupi inajaribu kuonyesha maeneo ambayo wawezeshaji waliyagusia na kuhitaji marekebishio ama ufafanuzi zaidi kutoka kwa serikali, na mwisho itaonyesha maoni na michango ya washiriki. Kwa ufupi semina hii iliweza kutoa fursa kwa wanaharakati kuwakilisha maoni na hisia zao juu ya mswada huu wa bajeti.

Kwanza, suala la utegemezi wa mapato kutoka nje, utegemezi huu umepungua kutoka asilimia 42% hadi 34% mwaka huu, lakini bado wanaharakati wanaona kuna haja ya serikali kucha kabisa utegemezi kutoka kwa wafadhili kwani kufanya hivyo ni chanzo cha mashinikizo mbalimbali kutoka kwa wafadhili hao katika utungaji wa sera hasa zile za masoko huria.

Pili, upande wa matumizi, mapendezo ya kutumia shlingi 7.1 trilioni ni kiasi kikubwa sana, wanaharakati walipendekeza serikali ipunguze wizara na mawaziri na kuhakikisha kila mtumishi wa umma anafanya kazi kwa ufanisi na kuthamini kazi yake, badala ya kuwa mzigo kwa mlipa kodi. Na rasilimali ziongezwe kwa wafanyakazi wa sekta nyeti kama walimu, madktari, wauguzi, na wataalamu wa kilimo hasa mabwana shamba. Na serikali bado haijaweaka mikakati madhubuti ya kudhibiti matumizi mabovu ya fedha za umma, kama ripoti ya mkaguzi mkuu wa serikali ilivyofichua ubadhirifu mkubwa katika halmashauri katika miaka iliyopita, hivyo wanaharakati wanahitaji mkakati ulio wazi wa kupambana na hali hii.

Tatu, mgawanyo wa kiasi cha 64% ya fedha ya bajeti katika sekta muhimu za elimu, miundombinu, maji, afya, kilimo, na nishati ni hatua ya kupongezwa, hata hivyo tungependa kujua ni kwa kiasi gani rasilimali hizi zitakwenda kwa kila sekta, nani atafaidika, na zitaweza vipi kuimalisha katika utoaji wa huduma kwa kila mwananchi? Na kuhusu swala la kilimo kupewa kipaumbele kwa kilimo cha mashamba makubwa ni kuwafanya wakulima wadogo dogo kukosa nafasi ya ushindani na hivyo kuwanyima ajira na kuwaongezea ugumu wa maisha, hivyo wito wetu kwa serikali ni kwamba waangalie upya suala la wakulima wadogodogo na ambao wengi ni wananchi wa vijijini.

Nne, maji safi na maji taka, serikali imepunguza kiasi cha 40% ya fedha katika bajeati ya maji ukilinganisha na mwaka jana. Wanaharakti wanatoa wito kwa serikali kusikia kilio cha watu wengi wa vijijini waliosahulika katika kupata huduma ya maji safi na salama maji ni kipaumbele kikubwa kwa wanawake/wasichana kwa sababu wao ndio wanajishughulisha kutafuta maji pamoja na kazi nyingine kedekede ikiwemo kutunza wagonjwa, kupika, usafi nk.

Tano, ajira na maisha bora. Bajeti hii haina mkakati wa jinsi ya kuwezesha ajira na uhakika wa maisha bora. Kwa majibu wa ripoti ya umasikini na maendeleo ya binadamu ya 2007 hali ya watu wasio na ajira ni mbaya sana hasa kwa wanawake na vijana, na takribani 40% ya wanawake katika jiji la Dar ers sdalaam hawana ajira ukilinganisha na 23% ya wanaume. Wanaharakti wanasisitiza serikali iweke mipango madhubuti katika kukuza ajira kwa vijana na wanawake na kuboresha maisha ya wananchi wa hali ya chini.

Sita, hotuba ya bajeti haijagusia katika sehemu yoyote kushirikisha sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya bajeti, hivyo wanaharakti wanaona kuna umuhimu mkubwa kwa serikali kutoa fursa kwa sekta binafsi hasa mashirika ya kijamii katika kutekeleza mipango ya bajeti ya mwaka 08/09.

Mapendekezo na maoni ya washiriki.

1. Elimu ya shule ya Msingi ipewe kipaumbele zaidi. Ubora uongezwe katika walimu, na vitabu, na sio majengo pekee kama ilivyo sasa.
2. Madini hayajapewa kipaumbele katika kuchangia pato la taifa, bado serikali inatakiwa kuongeza kipaumbele zaidi katika ukusanyaji wa kodi za madini na iachane na mikataba ya zamani ya madini ambayo ni ya kinyonyaji.
3. Serikali idhibiti mfumuko wa bei hasa hasa katika mazao ya kilimo kwani wananchi wa hali ya chini ndio wanaoumia zaidi na hali hiyo.

4. Kodi katika pembejeo za kilimo zitolowe kabisa tofauti na sasa ambapo mkulima bado anatozws kodi kubwa sana tofauti na faida anayopata kutokana na mazao.

5. Kodi inayopatikana kutoka kwa wananchi inaweza kuendesha nchi hii hivyo kinachotakiwa wananchi waongeze ufuatiliaji wa mapato na matumizi ya serikali kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa hadi wilayani ili kupunguza mianya ya ubadhirifu unaofanywa na maofisa ambao sio waaminifu.

6. Mchango wa vifaa vya uzazi ufutwe kabisa kama sera ya serikali inavyosema, na tofauti na sasa ilivyo kwani katika hospitali nyingi za serikali bado wananchi wanatakiwa kuchangia vifaa hivyo na ni chanzo cha vifo vya akina mama wengi hasa wale wa kipato cha chini.

7. Serikali itafute vyanzo vingine vya mapato na sio kuongeza kodi katika sigara na bia kila mwaka. Bado kuna vyanzo vingi vya kodi ambavyo havijaguswa.


Baadhi ya Picha za washiriki wa Semina hiyo.

Mtoa Mada wa Kwanza Mama Gema Akilimali (FemAct) akiwakilisha

Mtoa Mada wa Pili Dada Sarah Kutoka Utu Mwanamke akiwakilisha.


Baadhi ya washiriki wakifuatilia semina.

Baadhi ya Washiriki wakifuatilia semina

Dada Subira Kibigi akichangia hoja juu ya mada zilizowakilishwa.

1 comment:

Author said...

Bajeti hii haijamtendea haki mwananchi wa kawaida hasa walivyopunguza kodi kwenye mafuta mazito ya moto poa, idadi kubwa ya watumiaji wa majiko ya moto poa wako mijini, vijijini mafuta haya hata hayapatikani na hata yakipatikana hakuna atakayeweza kumudu kuyanunua, hapa cha msingi wangeondoa kodi ya mafuta ya taa kabisa isiwepo kwani ndio hutumiwa na wengi na pia ingewekwa mikakati madhubuti ya mpango wa kata mti panda miti na sio mti! Nishati mbadala ya kuni ndio kipimbilio la wengi wenye hali ngumu kimaisha hivyo kwa kupanda miti mingi tungeweza kuzitumia kuni pasipo kuharibu mazingira.

Upande mwingine mbovu ni walipopunguza kodi ya leseni za barabarani (road license, magari yaliyopunguziwa gharama kubwa ni mashangingi (4X4) ambayo htumiwa na mawaziri na wabunge wenyewe,hii haimsaidii mwananchi wa kawaida!! Wangeondoa kabisa kodi hiyo kwenye matrekta na magari makubwa ya kubebea mazao kutoka vijijini na mashambani na ingeleta nafuu kubwa kwa mwananchi.