Tuesday, June 24, 2008

FEMACT YAUNGA MKONO WABUNGE KUPAMBANA NA UFISADI

Sisi Mtandao wa wanaharakati wanaotetea usawa wa jinsia, haki za binadamu, ukombozi wa wanawake na maendeleo (FemAct) tunaungana na wabunge wote ambao wameamua kusimama kidete kupambana na ufisadi hapa nchini ili rasilimali za taifa ziweze kunufaisha wananchi wanaoteseka na umaskini mijini na vijijini.

Tunaona hatua ya wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi , kuamua kutumia sauti na fursa zao kupigania maslahi ya wananchi walio wengi ni muhimu kuungwa mkono na kila mtu anayeitakia nchi yetu amani na maendeleo endelevu bila kujali ni mwana siasa au la.

Kitendo cha wabunge kutaka serikali ihakikishe kuwa watu walioiba fedha kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) wazirudishe na kuchukuliwa hatua na kisha Umma ufahamishwe ni kina nani hao waliohusika na uovu huo, kinapaswa kupongezwa kama hatua sahihi katika kuleta mapinduzi ya kweli ya kukomesha ufisadi dhidi ya mali na rasilimali za taifa.

Wabunge hao pia wanastahili pongezi kwa kuibana serikali kuhakikisha kwamba shilingi bilioni 216 ambazo na watu wachache walikopa toka Benki Kuu takribani miaka 16 iliyopita ziwe zimerundishwa na wabunge kupewa vithibitisho halisi vya kuonesha kuwa fedha hizo zimerudi serikalini . Kwetu rasilimali hizi ni muhimu sana katika kutekeleza miradi ya wananchi inayolenga kuondoa tofauti za kimkoa,mijini na vijijini na hususan kuboresha huduma za kupunguza vifo vya wanawake katika uzazi, kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia, huduma za maji na nishati ili kupunguza mzigo wa kazi za kulea na kuendeleza familia unaofanywa hususan na wanawake na watoto

Kadhalika wabunge wanastahili kuungwa mkono pale wanapoidai serikali isimamie uwajibikaji wa wale wote waliohusika na kashfa kwenye mkataba wa uzalishaji wa umeme wa dharura ambao ulitolewa kwa kampuni hewa ya Richmond.

Hadi sasa serikali inaendelea kulipa mabilioni mengi ya fedha za Watanzania kuhusiana na mkataba huo mchafu wakati maelefu ya wananchi wanaendelea kuteseka kutokana na ugumu wa maisha.

Sisi FemAct tunafarijika sana wabunge wanapofanya kazi zao kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa na wananchi walio wengi badala ya tabia iliyozoeleka hapo awali ya kuweka mbele maslahi ya watu binafsi au vyama vya siasa.

Hakika sisi tunaona wakati umefika kwa kila mbunge, kila kiongozi na kila mwananchi kuwa jasiri kutetea haki na maslahi ya umma na nchi yetu kwa ujumla hata kama kwa kufanya hivyo kutaudhi wale ambao kwa ujasiri huo watakuwa wamehatarisha maslahi yao binafsi au vyama vyao vya siasa. Wabunge kuonesha ujasiri katika kutaka hatua sahihi zichukuliwe dhidi ya ufisadi na mafisadi ni muhimu kwa sababu mwisho wa siku kilicho muhimu kuliko vyote ni umma wa Watanzania na taifa letu na si maslahi ya mtu mmoja mmoja au chama cha siasa.

Ndiyo sababu sisi FemAct tumeona tuweke wazi msimamo wetu kuwa tunaunga mkono kwa dhati hatua ya baadhi ya wabunge kujitoa mhanga kwa ajili ya kudai haki za wapiga kura wao kitendo ambacho tunaona kinaashiria dhamira ya wabunge hao ya kupambana na rushwa na vitendo vyote vya ufisadi ambavyo ni chanzo cha umaskini na ufukara wa watanzania walio wengi.

FemAct tunatarajia kuona kwamba serikali inatekeleza yale yote ambao wabunge wamedai serikali yetu iyatekeleze kwa wakati kuhusiana na kashfa ya Richmond, EPA na fedha hizo nyingine lukuki ambazo zilikopwa BOT ambazo hazijarudishwa.


FemAct ni mtandao unaojumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 50 yakiwepo Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),chama cha waandishi Wanawake Tanzania TAMWA, Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu -LHRC, Kituo cha Msaaada wa Sheria kwa Wanawake -WLAC, Fordia, Shirika la Wanasheria wanawake nchini-TAWLA.

2 comments:

Anonymous said...

mimi nachakua nafasi hii kuwaunga mkono FemAct kwanza kwa kutambua mchango wa wabunge wanaopambana na vitendo vya ufisadi katika nchi yetu. Natumaini sisi sote tunaona ugumu uliopo katika mapambano haya na mimi kwa mtazamo wangu itikadi ndio nguzo ya mafisadi wanayoitegemea iwalinde na iliyobaki katika mapambano haya, hivyo tukifanikiwa kuwaelimisha wabunge wetu kuweka mbele maslahi ya taifa nahisi vita hii tutashinda. aluta continua!

Anonymous said...

NASHANGAA SANANA NA SELEKALI AICHUKUI MAMUZI YAKINA KUUSU MAFISADI JE MAHAKAMA INAWACHUKULIAJE WAMELIZIKA NA VITENDO VA MAFISADI VYA KUCHEZEA PESA ZA WANANCHI TUMECHOKA MIMI ALLY NGWALE MABIBO DSM