Tuesday, June 24, 2008

BUNGE LETU LINAELEKEA WAPI ?!!

KUMETOKEA vioja ndani ya Bunge, nalo limeingiliwa na ndumba! Ndiyo, imani za kishirikina zimeingia bungeni. Wakati huu wa Bunge kujadili Bajeti tumeshuhudia Bunge likitumia sehemu ya muda, nguvu na rasilimali zetu katika kufuatilia uvumi wa kishirikina.

Tumekwenda mbali, tunaambiwa Bunge letu tukufu linachunguza uvumi huo! Hiki ni kioja kwa namna yake, maana kama jambo ni la uvumi iweje lichunguzwe. Kwamba tumefika mahali tunatumia muda na fedha zetu kuchunguza uvumi! Hivi ushahidi na vielelezo vya uvumi vinapatikanajamani?

Kama jambo ni la uvumi, basi kawaida ya anayehusishwa na uvumi ni kuukanusha vikali uvumi huo. Tulitaraji Bunge, mara baada ya kuanza kuenea kwa uvumi huo lingekanusha vikali baada ya kujiridhisha kuwa ni uvumi tu. Tena ni uvumi wenye kuhusiana na imani za kishirikina. Imani za kishirikina zimechangia sana kurudisha nyuma maendeleo yetu. Tuna mifano ya mauaji ya akina mama wazee na malbino yanayochangiwa na imani hizo. Bunge liwe mfano wa kupiga vita imani hizo.

Ni ajabu, na pengine ni mambo ya aibu hata mbele ya wahisani wanaochangia Bajeti yetu wanaposikia, kuwa katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia, Bunge la nchi linatumia muda wake na rasilimali zake kufuatilia na hata kuchunguza masuala ya imani za kishirikina.

Ili kulinda heshima ya Bunge letu na nchi yetu, jambo hili lingeangaliwa kisayansi na kiteknolojia zaidi ili nasi twende na wakati. Kama inadaiwa kuna mbunge ameingia bungeni usiku na kuweka vitu kwenye viti vya wabunge, basi kuna ya msingi ya kuangalia, kujiuliza na kuyapatia majibu kabla ya kuchukua hatua nyingine.

Haya yafuatayo tunaweza kabisa kuanza nayo kuyaangalia kabla ya kulifanya jambo hili kuwa ni kitu kikubwa kinachotuchukulia muda na fedha zetu; Sote tunaelewa, kuwa Jengo la Bunge ni mahali pa kazi kama ilivyo mahali pengine. Walipa kodi wa nchi hii wamechangia jengo la Bunge lijengwe na liwe ni mahali pa kazi zenye lengo la kumsaidia Mtanzania na kulinda maslahi ya umma wa Watanzania. Kila sehemu ya kazi ina taratibu zake.

Tuna imani kuna waliopewa dhamana ya kuruhusu na kuzuia wageni kuingia ndani ya jengo hilo katika wakati wa kazi na baada ya kazi. Lakini kikubwa, huwezi kuingia ndani ya jengo la Bunge bila kufunguliwa mlango na mwenye dhamana ya kushika funguo za mlango huo. Na kwa nini mbunge aliyeingia humo aingie usiku badala ya wakati wa kazi? Tunaambiwa hakuingia peke yake, je aliingia na nani?

Kilichotokea hapa ni ukiukwaji wa taratibu za kazi. Tuaambiwa aliyehusika anajulikana lakini jina halitajwi. Huku hakusaidii kupunguza uvumi, kunaongeza uvumi na kutupotezea wakati wa kujadili mambo ya kimsingi ya taifa letu. Jengo la Bunge ni la kisasa na la gharama kubwa. Tunaambiwa kamera za kurekodi matukio ndani ya jengo hilo hazikufanya kazi isipokuwa moja tu. Je, ni nani anayehusika na kuhakikisha kamera hizo zinafanya kazi?

Maswali yanayoulizwa hapa na mengineyo yana wahusika wa kuyajibu. Bunge litusaidie kupata majibu ya maswali haya ya msingi ili tupunguze hofu ya kutokea kwa madhara makubwa huko twendako. Maana, tunachokiona hapa ni uzembe wa baadhi ya watendaji katika Jengo hilo la Bunge. Leo kaingizwa Mheshimiwa Mbunge usiku, hatujui kesho ataingizwa nani. Inahusu usalama wa Jengo la Bunge kwa maana ya usalama wa Wabunge wetu. Tuko katika karne ambayo, mbali ya mambo mengine, tunapambana na ugaidi. Kamera za ndani na nje ya ukumbi wa Bunge si za mapambo. Zimewekwa ili kuchangia katika shughuli za usalama. Wahusika wanafanya nini?

Naam. Ni wakati sasa wa Bunge kukemea vikali imani za kishirikina na hasa zinapofika na kuingia ndani ya Bunge. Huko nyuma tumesikia habari za popobawa na kadhalika. Haya ni mambo ya abrakadabra, kama ninavyoyaita siku zote. Hayana maana yoyote. Ni kama vile mbinu ya wajanja fulani kututaka tutoke kwenye mstari wa kujadili mambo ya msingi yenye kuhusu hali yetu ya sasa na mustakabali wa nchi. Tusikubali kutoka kirahisi kwenye mstari wa kujadili ya maana na ya msingi kwa taifa. Na hapa nitarudi kwenye kujadili yenye kumhusu Mtanzania wa kawaida kuhusiana na Bajeti ya mwaka huu.

Jumatatu ya juma hili nilisimama kituo kimoja cha mafuta mjini Iringa. Usiku ulikuwa unakaribia. Mbele yangu nilimwona mama aliyeshika galoni ndogo. Ni galoni tupu ya ujazo wa lita tano. Alisimama sehemu ya kuuzia mafuta ya taa. Nilisogea, nilimsalimia. Akaniambia anamsubiri kijana wa kumpimia mafuta ya taa. Anaitwa Mama Mwajuma.

Mara akatokea kijana anayehusika. Anaitwa Bakari. Mama Mwajuma alinunua mafuta ya taa ya shilingi 200! Bei ya lita moja ya mafuta ya taa kwa siku hiyo ilikuwa ni shilingi 1450. Kwa shilingi 200 hupati hata robo lita. Mama yule alipimiwa nukta kadhaa za mafuta. Ndiyo, alipimiwa matone kadhaa ya mafuta ya taa.

Na kama ilivyo jina lenyewe la mafuta, Mama Mwajuma alikwenda kununua mafuta ya kuwashia koroboi. Hakuwa na uwezo wa kununua lita moja ya mafuta ya taa, ni bei ya juu sana. Bakari, kijana mwuza mafuta aliniambia; kuwa zamani kipimo cha kuanzia ilikuwa ni mafuta ya shilingi 500. Kwamba mpaka mwaka jana lita moja ilikuwa ni shilingi 900. Bakari alizidi kunielimisha, kuwa kutokana na kuelewa unyonge na hali ngumu za watu wengi, wameamua kuwasaidia hata wenye kutaka mafuta ya taa ya shilingi 200.

” Tutafanye kaka, si unaona mama huyu hali yake.Nikimkatalia mafuta ya shilingi 200 atakwenda kulala giza. Ni bora nimpe hayo matone ya mafuta akajaze kibatari chake”.

Naam. Tunachoongelea hapa si uvumi. Ni hali halisi. Bei za mafuta zimepanda sana, hivyo ugumu wa maisha umezidi kwa Watanzania wengi zaidi. Bei ya nishati ya umeme nayo ni ya juu sana. Leo kwenye miji yetu kuna Watanzania wanaotumia vibatari. Hawamudu tena kulipia gharama za umeme.

Tufahamu, kuwa kwenye hospitali na zahanati zetu kuna wagonjwa wanaolala chini kwa kukosa vitanda. Kuna wagonjwa wanaokosa dawa. Katika nchi yetu hii, achilia mbali vijijini, mijini kuna barabara za mitaa zenye mashimo kama mahandaki. Tuna shule vijijini na mijini ambako wanafunzi wanakaa chini na wengine kukosa walimu. Haya yanatokea katika nchi yetu hii.

Kwa nini wagonjwa wetu walale chini na wakose dawa? Kwa nini watoto wetu wakae chini madarasani na kukosa walimu? Fedha zinakwenda wapi? Haya na mengineyo ndio maswali tunayopaswa kujiuliza na kujiumiza vichwa. Haya si mambo ya uvumi. Haya si mambo ya abrakadabla. Ni hali halisi. Hatuhitaji tume kuchunguza. Tunahitaji kuchukua hatua. Sasa.


Chanzo: Gazeti la Raia Mwema
Na Maggid Mjengwa (Blogger).

4 comments:

Author said...

Bunge la Bajeti la mwaka huu 2008, linaashiria kwamba hapatakuwa na ya maana ya kuzungumzwa. Bunge limeanza na mguu wa mkosi. Mambo mawili yanaweza kutajwa kuwa ambayo yamelitia Bunge la Bajeti nuksi. Waache kujadili masuala ya kijinga na walenge ya muhimu yenye maslahi kwa taifa zima na si kwa maslahi yao kisiasa!!!

Edwin

Anonymous said...

nilishangazwa na kilicho tokea siku za karibu kuona bunge kama taasisi muhimu kuacha majukumu yake ya msingi, na kugeuza ukumbi wa bunge kuwa kijiwe cha kujadili masula ya hovyo kama wenyewe wanavyo yaita ya uvumi na uzushi mtupu kuhusiana na suala la ushirikina.sipendi kuamini lakini yamekwisha tokea wananchi tuliweka tumaini letu mikononi mwa bunge kupata afueni ya matatizo yanayo likabili taifa kinyume chake bunge limejipa kazi mpya kujadili uvumi na kuya acha masuala mengi ya msingi ambayo ayajapatiwa majibu yakiendelea kupigwa danadana misili ya mchezo huo wa watoto na kuacha masuala kama vile epa,richmond,meremeta,kiwila na mfumuko wa bei ulio pelekea kupanda kwa bei ya nishati na nafaka na kufanya hali kuwa mbaya zaidi kwa wananchi maskini walio wengi.taifa limefikishwa hapo na kundi dogo la viongozi walafi kukosa uzalendo na kuwajibika. nilicho jifunza kutokana na hili sisi kama jamii tufanye mabadiliko kwani hawa wenzetu tulio watuma wametuthibitishia kuwa tume wapa kazi wasio iweza wao vichwa vyao vimejawa na kujadili uvumi kuliko hali halisi inalo likabili taifa tuna haja ya kuwapa nafasi kizazi kipya kisicho kuwa na hata chembe ya ufisadi wala kuliingiza taifa katika mikataba ya kinyonyaji kwa maslai ya wachache huu ni wakati wa kizazi kipya chenye fikra chanya za kulikomboa taifa lililo mezwa na umaskini wa kutupwa.kisicho kuwa muumini wa uvumi.SOLOMON ASKOFU

Anonymous said...

si situshwi hata kidogo na kinacho tokea ktk bunge letu tukufu, hili ni tokeo la kizazi legelege kinacho zaa viongozi legelege, walio choka mapema kabla hata hakujapambazuka,ukiona hivi ni ishara ya makuzi,malezi na hata aina ya elimu wanayo pata watanzania, kwa muda mrefu isiyo na muono mpana usio weza kunyambulisha masuala gani ni msingi wa maendeleo,hivyo basi tunahitaji mjadala wa kitaifa wa kupata aina ya elimu inayo weza kutufikirisha na kutunyambulisha fikra endelevu.bila hivyo tutaendelea kuwa na bunge butu na wabunge butu na kunajisi mahali patukufu panapo paswa kujadiliwa masuala ya msingi na endelevu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu hivyo shime shime tusiingie ktk mtego wa kujadili uvumi na uzushi wa kikundi cha watu wa chache wanao itafuna nchi hii kama mchwa wasio na huruma na kuacha kujadili mabadiliko ya viongozi wabovu ndani ya serikali na chama tawala toka ngazi ya chini hadi juu mabadiliko huletwa na watu wachache wanao tambua utaifa wao na rasilimali zao huu mfano wa kujadili usirikina ni sawa na kuipeleka timu yetu ya taifa ktk ukumbi wa bunge wakati wa vikao vya bajeti mwaka jana kwa nini wa kati wa bajeti??? mwanaharakati ALBERT KILLANGO GDSS

Anonymous said...

Mimi nakubaliana na anony wote hapo juu. Eti wabunge wanajadili uvumi wa ulozi! kumbe wanaogopa uchawi. kwanini hiyo spirit ya kuogopa uchawi hawaiamishii kuogopa machozi ya Watanzania walalahoi? mie nadhani hofu yao kubwa ingekuwa kwa kilio cha Mlalahoi. Mlalahoi ana matatizo mengi kiasi kwamba hata huo Ulozi anaona ni kitu kidogo sana.
Hebu Wabunge oneni AIBU!
Amkeni kutetea haki za Wanyonge.
Nikashangaa hata wengine wakathubutu Kumbwatukia Mh Anna Kilango! Hee kwanini asilie na wananchi WAKE?
Hizo Pesa Za EPA Tunataka kujua zimelejeshwa kiasi gani?? Na zinapangiwa kazi gani.
Mchanga wa macho mmeshatupiga nao sana, lakini sasa MACHO YETU yamekuwa sugu. Hatuwezi kuvumilia tena kudanganywa tena.INATOSHA