Wednesday, October 1, 2014

WANAHARAKATI WA NGAZI YA JAMII NA WASHIRIKI WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KUHUSU RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA INAYOPENDEKEZWA NA BUNGE MAALUM LA KATIBATAMKO LA WANAHARAKATI WA NGAZI YA JAMII NA WASHIRIKI WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KUHUSU RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA INAYOPENDEKEZWA NA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Wanaharakati wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (Gender Development Seminar SeriesGDSS) linaloratibiwa na TGNP Mtandao tunatoa tamko hili baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa Rasimu inayopendekezwa na kutolewa na Bunge maalum la Katiba tarehe 24/9/2014 mjini Dodoma. Tamko hili tunalitoa kwa kuhusianisha rasimu ya Katiba inayopendekezwa na  madai ya wanaharakati wa Masuala ya Jinsia.

Wanaharakati masuala ya jinsia na haki za binadamu waliainisha madai 12 ya kikatiba yanayowahusu Wanawake na makundi mengine ya walio pembezoni. Madai hayo ni pamoja na Haki za wanawake zibainishwe kwenye Katiba, Sheria Kandamizi zibatilishwe, Haki ya kufikia, kutumia, kunufaika na kumiliki rasilimali ya nchi, Utu wa mwanamke ulindwe, Utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu haki za Wanawake, Haki sawa katika nafasi za uongozi, Haki za wanawake wenye ulemavu, Haki ya uzazi salama, Haki za watoto wa kike, Haki ya kufikia na kufaidi huduma za Msingi, Wajibu wa wazazi katika matunzo ya watoto na Katiba iunde chombo maaalum kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi.

Tunapongeza kamati ya uandishi wa katiba na Bunge maalum la katiba kwa kuzingatia na kutambua umuhimu wa baadhi ya masuala ya Jinsia yakiwemo haki za wanawake, haki za watoto hususan umri wa motto, haki za wenye ulemavu, haki za wazee na kuyaingiza katika rasimu ya Katiba lakini tumeshangazwa kuona suala la maji halijatambuliwa kama haki ya msingi ya kikatiba wakati ambapo asilimia 65% ya watu wa mijini ndio wanapata maji safi na salama huku asilimia 42% ya wakazi wa vijijini ndio wanaopata maji safi na salama. Tunadai haki ya kupata maji safi na salama iwe ni haki ya kikatiba ili kuweza kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutembea umbali mrefu wa kutafuta maji.

Rasimu ya katiba imeipa uwezo bunge la jamhuri ya muungano kumuwajibisha Rais pindi akishindwa kutekeleza majukumu yake na akienda kinyume na sheria na taratibu za nchi. Lakini rasimu hii imewanyima wananchi  haki yao ya msingi ya kumuwajibisha kiongozi (Mbunge/diwani) waliemchagua kwa kura zao halali pindi anaposhindwa kutekeleza majukumu na ahadi alizozitoa wakati wa kampeni kwa wananchi. Tunadai rasimu hii ya katiba iweke ukomo wa vipindi kwa wabunge kukaa madarakani na iweke mfumo mzuri wa wananchi  kuwawajibisha viongozi wasiotimiza majukumu yao kama ilivyo kwa bunge ilivyopewa dhamana na haki ya kumuwajibisha Rais anaposhindwa kutimiza wajibu wake.

Tunapongeza bunge maalum la katiba kwa kupunguza umri wa kugombea Urais kutoka miaka 45 ya zamani hadi miaka 40 kwa sasa (Ibara 85) na kuweka utaratibu wa kuhoji matokeo ya urais katika mahakama kuu. Hali hii itasaidia kutoa haki  kwa vijana na wanawake kushiriki katika kuwania nafasi za uongozi na pia itawezesha wananchi wenye malalamiko dhidi  ya matokeo ya Urais kupata haki ya kukata rufaa na kupinga matokeo.

Rasimu hii ibara ya 79 na 80  imeendeleza kumlimbikizia Rais madaraka ya kuteua viongozi na watendaji  mbalimbali wa serikali bila ya kufuata na kuzingatia ushauri atakaopewa na  mtu au mamlaka yoyote.  Hali hii bado inaendeleza mfumo mbaya wa mgawanyo wa madaraka kikatiba na inaendeleza mfumo kandamizi katika utoaji wa fursa za kiuongozi. Tunashauri rasimu hii ya Katiba iweke ukomo wa uteuzi kwa rais ili kutoa fursa kwa mamlaka nyingine kufanya uteuzi wenye tija. Mfano katiba ya Kenya imetoa fursa ya wananchi kuhoji uteuzi unaofanywa katika ngazi mbali mbali.

Ibara ya 135 (b) imeeleza sifa ya mbunge awe anajua kusoma na kuandika Kiswahili au kingereza. Sifa hii ya kuchaguliwa kuwa mbunge inadidimiza maendeleo ya taifa kwani bunge linatakiwa kupitia na kuchambua kwa kina mikataba mbali mbali ambayo kwa sehemu kubwa ipo kwenye lugha ya kingereza.  Je kigezo hiki cha kujua kusoma na kuandika kwa mbunge kutaweza kumfanya aweze kuisimamia, kufanya uchambuzi wa kina na kuiwajibisha serikali kikamilifu? Na je kwa kigezo na sifa hizi za mbunge je itaondoa tatizo la nchi kuingia mikataba mibovu? Tunadai rasimu hii ya katiba ibadilishe sifa ya kiwango cha elimu ya mbunge kuwa kidato cha nne.

Tunapongeza bunge maalumu la Katiba kwa kutambua haki ya  upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa watu wote ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi salama (Ibara ya 14 kifungu cha (2) (f) ), lakini rasimu hii bado haijaonesha ni namna gani makundi ya walio pembezoni kama wanawake, wazee na walemavu wataweza kufikia huduma bora za afya bila vikwazo kutoka kwa watoa huduma hizo. Kwa mfano rasimu hii haijaonesha namna gani wanawake wajawazito, walemavu na wazee wataweza kupata misamaha ya kuchangia gharama za  upatikanaji wa huduma za afya. Tunadai rasimu iweke mfumo mzuri wa kuwasaidia makundi ya walio pembezoni kuweza kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo.

Ibara ya 111kifungu cha (1) (d) imetaja sifa ya kuwa waziri au naibu waziri kuwa ni lazima awe ni mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kifungu hiki kinaendeleza mgongano wa madaraka kati mihili mikuu miwili ya dola (Bunge na Serikali) kwa kumpa madaraka mbunge kuwa waziri au naibu waziri. Tunadai mawaziri wasiwe miongoni mwa wabunge ili kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa mihimili yote mitatu kwa kila mhimili kujitegemea

Katika ibara 22 kifungu cha(2) (d) imeanisha haki ya wanawake kupata, kumiliki, kutumia, kuendeleza na kusimamia ardhi kama ilivyo kwa mwanaume lakini tumeshangaa kuona katika ibara ya 22(2) (b) rasimu hii ikitoa fursa ya bila ya ukomo kwa wawekezaji kuweza kutumia ardhi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na makaazi. Tunashauri kipengele hiki kiweke ukomo kwa wawekezaji kutumia ardhi ili kuweza kuepusha migongano na migogoro ya kimaslahi na ya kikatiba kati ya wananchi na wawekezaji katika suala zima la umiliki wa ardhi.

Tunapongeza bunge maalum la katiba kwa kutambua haki za wanawake na usawa wa kijinsia katika ushiriki na upatikanaji wa fursa sawa za ajira, ushiriki katika  ngazi za maamuzi, kumiliki mali na kupata ujira sawa na mwanaume katika kazi zenye sifa zinazofanana (Ibara ya 54 kifungu A hadi G). Lakini rasimu hii bado haijatamka wazi uwiano wa asilimia 50 kwa 50 katika ngazi na nafasi mbali mbali za maamuzi. Tunadai katiba itamke uwiano wa 50/50 katika nafasi na ngazi zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Ibara ya 14 (2)(e) imeeleza katiba itaweka utaratibu  unaofaa kwa ajili ya kila mtu kupata elimu,  lakini ibara 49(1) imeeleza haki ya kupata elimu ya msingi inayomtayarisha kikamilifu kuendelea na elimu ya ngazi inayofuatia au kuweka msingi wa kuanza kujitegemea. Tunadai rasimu ya katiba itambue haki ya kupata elimu kutoka elimu ya awali hadi  kidato cha nne ili kuweza kuondoa matabaka katika jamii na sio kuweka utaratibu tu wa upatikanaji wa elimu.

Ibara ya 257 kifungu cha (3) kimetoa uhuru kwa Benki kuu ya Tanzania (BOT) kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa, kudhibitiwa au kupewa maelekezo na mtu au mamlaka yoyote. Kifungu hiki kinakinzana na dhana bora ya uwajibikaji na utawala bora na kinatoa mwanya wa ubadhirifu na matumizi ya mabaya ya fedha za umma kwa kigezo cha watendaji wa benki kuu kutowajibishwa kutokana na makosa yao kiutendaji pindi wanapokua madarakani. Kifungu hiki kinachochea na kutoa fursa ya ulimbikizaji kiporaji wa rasilimali na fedha za umma. Tunadai ibara hii irekebishwe.
Kutokana na hayo tulio yaeleza hapo juu tunadai yafuatayo;
i.                          Tunadai katiba itamke uwiano wa 50/50 katika nafasi na ngazi zote za maamuzi kati ya wanawake na wanaume kuanzia ngazi za chini kabisa hadi taifa, katika ngazi za kisiasa, kiuchumi na kijamii
ii.                       Tunadai haki ya kupata maji safi na salama iwe ni haki ya kikatiba ili kuweza kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutembea umbali mrefu wa kutafuta maji.
iii.                     Tunadai rasimu hii ya katiba ibadilishe sifa ya kiwango cha elimu ya mbunge kuwa kidato cha nne.
iv.                      Tunadai mawaziri wasiwe miongoni mwa wabunge ili kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa mihimili yote mitatu kwa kila mhimili kujitegemea.
v.                       Tunadai katiba iweke ukomo wa vipindi kwa wabunge kukaa madakani na iweke mfumo mzuri wa kuwawajibisha viongozi wasiotimiza majukumu yao kwa wananchi.
vi.                      Tunadai rasimu iweke mfumo mzuri wa kuwasaidia makundi ya walio pembezoni kuweza kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo.
vii.                   Tunadai kipengele cha ukomo kwa wawekezaji kutumia ardhi ili kuweza kuepusha migongano na migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika suala zima la umiliki wa ardhi.
viii.             Tunadai katiba iunde chombo maaalum kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi
ix.                     Tunadai rasimu ya katiba itambue haki ya kupata elimu kutoka elimu ya awali hadi  kidato cha nne ili kuweza kuondoa matabaka katika jamii na sio kuweka utaratibu tu wa upatikanaji wa elimu.
x.                        Tunadai rasimu hii ya katiba ifute kipengele cha Benki kuu ya Tanzania (BOT) kutowajibishwa na kudhibitiwa na  mtu au mamlaka yoyote ya kiutendaji ili kuimarisha mfumo wa uwajibikaji.
Tamko hili limesainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao kwa niaba ya washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) na wanaharakati  wa ngazi ya jamii leo tarehe 27/9/2014.
 

Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji- TGNP Mtandao
KNY Washiriki wote wa semina za Jinsia na Maendeleo GDSS
                           
Kamati ya uchambuzi wa rasimu inayopendekezwa  na wananchi wanaoshiriki GDSS ni hawa wafuatao;
i.                    Badi Darusi                       Mwenyekiti
ii.                  Esther William                  Katibu
iii.                Hamadi Masudi                 Mjumbe
iv.                Rehema Mayuya               Mjumbe
v.                  Heriet Kabende                 Mjumbe
vi.                Lena Jackson                     Mjumbe
vii.              Selemani Bishagazi           Mjumbe


No comments: