Wednesday, October 1, 2014

“ JE AJENDA YA USAWA WA KIJINSIA NI AJENDA YA VYAMA VYA SIASA?”



 “ JE AJENDA YA USAWA WA KIJINSIA NI AJENDA YA VYAMA VYA SIASA?”


Makala hii Imeandaliwa na Usu Mallya & Ruth Meena
Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania

Dhana ya usawa wa jinsia  inatumika pale ambapo jamii imeweza kuondoa tabaka lililojengeka katika kufikia, kumiliki na kufaidi rasilimali zinazoshikika na zisizoshikika katika jamii husika. Kimantiki usawa wa jinsia ni hali ya maisha isiyojengeka katika kubagua mwanamke au mwanaume kutokana na jinsi yake. Kimaumbile binadamu huzaliwa na jinsi ya kike au kiume, lakini jamii hutafsiri ni nini maana ya kuwa mwanamke au mwanaume, kwa kutoa haki tofauti, stahili tofauti , wajibu na hata thamani ya utu wao. Katika jamii nyingi tofauti hizi huashiria kujenga tabaka kati ya mwanaume na mwanamke kwa njia ya kuhalalisha ubaguzi wa jinsia ambao huashiria kunyima mwanamke haki sawa katika kufikia na kumiliki rasilimali, na  katika kupata heshima, ya utu wake.  Mfumo huu unaposhamiri katika jamii, huwa
unadhoofisha kujengeka na kuimarika kwa demokrasia, utawala bora na uwajibikaji.

Dhana ya demokrasia ni mfumo wa maisha uliojengeka katika  msingi inayowezesha wanajamii kusikiliza na kusikilizwa, kutafakari kwa makini kutambua, kuheshimu  na kuelewa fikra za wengine na kujenga mahusiano yenye kuheshimiana, kuvumiliana tofauti za kifikra, pamoja na kugawiana madaraka ya kuongoza jamii husika. Katika Nyanja ya siasa demokrasia ni mfumo wa siasa unaoruhusu ushiriki wa wengi katika maamuzi ya msingi kuhusu maisha wahusika.

Kimantiki huwezi kujenga mfumo wa demokrasia usiozingatia usawa wa jinsia. Hapa kwetu Tanzania tabaka la jinsia linazidi kuongezeka na hivyo kudhoofisha demokrasia na kuathiri maendeleo yetu hususani vita dhidi ya umaskini.   Uchambuzi yakinifu uliyofanywa na shirika moja la kimataifa lijulikanalo kama Global Economic Forum mwaka 2013 ulikiri kwamba  tabaka  kati ya wanawake na wanaume  katika nyanja zote hususani elimu, afya na uongozi linaongezeka. Pengo la jinsia kati ya wanawake na wanaume,   imezidi kupanuka na Tanzania imeshuka sana katika nyanja zote za elimu, afya, uchumi na uongozi. Mwaka 2006 Tanzania ilikuwa ya 26 kati nchi zilizofanyiwa utafiti, hali hii ilishuka hadi kufikia 52 mwaka 2009, ikaendelea kushuka hadi  kufikia 57  mwaka 2010, ikafika ya 63 mwaka 2012.  Mwaka jana 2013 imeshuka kufikia ya 70. 

Athari za kuongezeka kwa pengo au tabaka la jinsia katika uimarishwaji wa demokrasia ni nini?? Ni nani awajibike katika kuondoa tabaka hili?? Makala hii itajikita katika kuchambua wajibu wa vyama vya siasa katika kujenga demokrasia kwa mrengo wa jinsia.

Vyama Vya Siasa Vina Jukumu Gani Katika Kufikia Usawa wa Kijinsia Kwa 50/50 Katika Uongozi?

 Vyama vya siasa katika mfumo wa Demokrasia ya vyama vingi ni taasisi muhimu ya kujenga, kulea na kuimarisha kada la viongozi wa kisiasa. Vilevile vyama vya siasa ni nguzo kuu  ya utawala bora kwa mantiki ya kuwajibisha serikali iliyoko madarakani kuzingatia utawala wa sheria, haki  na uwazi. Utawala wa sheria unajengeka tu pale ambapo kila raia ke kwa me, wa makundi na tabaka zote wanapewa fursa sawa  mbele ya sheria. Vyama vya siasa vinapopewa dhamana ya kuingia  katika vyombo vya uwakilishi vinahusika katika utunzi wa sheria na sera za nchi. Hii inamaanisha kwamba vyama hivi vina nguvu ya kuleta mabadiliko katika mifumo kandamizi kwa kutunga sheria zitakazobatilisha sheria kandamizi ikiwa ni pamoja na sheria zinazohalalisha ukandamizaji wa kijinsia.

Mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa umejengwa katika utambuzi huu. Vyama vya siasa kote duniani ni taasisi muhimu katika kuwakilisha sauti na matakwa ya makundi ya wananchi wanawake kwa wanaume wenye fikra na mawazo yanayoshabihiana hususan kuhusu itikadi inayoongoza dira ya aina ya jamii wanayoitamani. Kwa kuongozwa na itikadi zao vyama vimeweza kujenga ushawishi mkubwa kwa wanachama wenyewe na wananchi wengine katika kuunga mkono sera zao na mikakati ya maendeleo hata kuweza kupewa nafasi za uongozi wa kisiasa katika ngazi ya serikali za mitaa, majimbo na nafasi ya uraisi.

Ili vyama vya siasa viweze kutekeleza wajibu na majukumu ya kuimarisha demokrasia, utawala bora, na haki sawa, sharti vyama hivi vijenge misingi  hii na utamaduni ndani ya vyama vyao kwa matendo. Vyama vinavyotetea haki na demokrasia haviwezi kubagua wanawake katika ngazi za maamuzi ndani ya vyama.

Swali la kujiuliza ni kwa kiwango gani vyama vyetu vya siasa nchini Tanzania vimejengwa katika misingi ya demokrasia yenye mrengo wa jinsia  au viko tayari kuendeleza mabadiliko ndani ya vyama kuelekea kwenye misingi imara ya demokrasia? Je ni vyama vipi hapa kwetu Tanzania vinavyoweza kusimama na kukiri kwamba vinatenda kama vinavyonena? (walk the talk).  Je ni vyama vipi ambavyo havipatwi na kigugumizi wanawake wanapodai ushiriki katika ngazi zote za maamuzi?? Je ni vyama vipi viko tayari kuona na kuleta mabadiliko ya kimapinduzi katika mifumo inayoendelea kuwaweka pembezoni takribani nusu ya watanzania katika mifumo rasmi ya uchumi na siasa?  Miaka hamsini baada ya Uhuru inakuwaje baadhi ya viongozi wa ngazi za juu katika vyama wanendelea kutilia shaka uwezekano wa kuwa na usawa katika maamuzi ya msingi yanayogusa watanzania wote Wanawake kwa wanaume?

Ajenda ya usawa wa kijinsia kufikia 50/50 nchini Tanzania imepata msukumo mkubwa katika majadiliano yanayoendelea hivi sasa ndani ya Bunge Maalum la Katiba, miongoni mwa wanaharakati wa usawa wa kijinsia na haki za wanawake na katika vyombo vya habari. Ajenda hii si ngeni, nchi ya Tanzania imeridhia Maazimio mbalimbali ya kimataifa na kikanda katika kufikia azma ya usawa wa kijinsia katika uongozi. Azimio la Umoja  wa Afrika kupitia Mkataba wa Nyongeza wa Maputo (20053) uliagiza nchi wanachama  kufanya marekebisho ya Katiba ili kuwezesha kufikia  50/50 usawa wa kijinsia katika Uongozi ifikapo mwaka 2015.

Nchini Tanzania, juhudi hizi zimekuwa ni sehemu ya utetezi wa haki za wanawake miongoni mwa wanaharakati wa Usawa wa Jinsia, Demokrasia na Maendeleo kwa muda mrefu. Hususan katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, mojawapo ya madai ya wanaharakati katika uchaguzi mkuu wa 2005 ilikuwa ni kuitaka serikali itakayochukua madaraka kuanza mchakato wa kutekeleza agizo hilo la Umoja wa Afrika. Mchakato wa kuelekea uwiano wa Jinsia katika Uongozi kwa 50/50 ulianza mwaka 2005 kwa Uongozi wa Wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Chambuzi zilifanyika hususan kujifunza kutoka nchi nyingine kuhusu muundo unaofaa kufikia usawa wa 50/50 na Kampeni mbalimbali zimekuwa zinaendeshwa kuanzia kipindi hicho.

Rasimu ya Katiba iliweka bayana Msingi wa Usawa wa 50/50 katika uongozi Ibara 113 (a) kwa kupitia Uchaguzi wa Majimbo. Wanaharakati walipongeza hatua hii na kujenga hoja ya umuhimu wa kuweka msingi wa usawa katika nyanja zote za uongozi na si katika uchaguzi wa Majimbo ya Kisiasa peke yake. Katika majadiliano yanayoendelea hivi sasa katika Bunge Maalum la Katiba hoja hii imekubalika kimsingi kutokana na mapendekezo kutoka kamati nyingi. Matarajio yetu ni kuwa Mapendekezo ya Katiba Mpya yatazingatia matakwa ya wananchi walio wengi na hoja za Kamati za Bunge Maalum la Katiba. Pia tunatarajia kuwa Muundo utakaopendekezwa hautaendelea kujenga madaraja kati ya wanawake na wanaume katika Uongozi wa Kisiasa.

Katika kuzingatia dhana ya ushiriki kivitendo, ni matarajio ya walio wengi kuwa utekelezaji wa msingi wa usawa wa kijinsia kufikia 50/50 katika uongozi utaleta mabadiliko ya taswira na sura za Uongozi katika vyama vyote vya Siasa. Vyama hivi, vinapojiandaa kuteua safu mpya ya uongozi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, tunataka tuamini kwamba vitaleta mabadiliko ya twasira ya sasa ambapo uongozi wa ngazi za juu umehodhiwa na jinsi moja tu, yaani wanaume.

Licha ya ukweli kuwa wanawake wamekuwa nguzo kuu  ya kujenga vyama, ushiriki wao katika Uongozi wa  vyama vyao  umekuwa  ni kwa kupitia mfumo wa Matawi ya Vyama “Women Wings” , wakati kuna fursa finyu za ushiriki wa moja katika mfumo mkuu wa maamuzi ndani ya vyama kama wenye viti kitaifa, kimkoa na wilaya, wajumbe wa halmashauri kuu, kamati kuu, makatibu wakuu,na nafasi nyingine za utendaji ndani ya vyama husika. Msingi wa usawa wa jinsia ndani ya vyama ingaliashiria dhamira za vyama husika kuweka ajenda za kuwajibika katika kubomoa matabaka  mifumo inayowanyima haki wanawake.

Hata hivyo wakati matarajio ya wanawake na wanaharakati wa kutetea haki za usawa wa jinsia nchini yakiwa makubwa, uchaguzi uliofanywa hivi karibuni na Chama cha Chadema, umetupa wasiwasi kiasi cha kujiuliza ni kwa kiwango gani vyama vya siasa vimetafakari ajenda ya usawa wa kijinsia kama sehemu ya itikadi zao? Je usawa wa kijinsia ni sehemu ya majadiliano ya mustakabali wa taifa na dira ya vyama? Katika uchaguzi huo safu ya viongozi wa juu ni kama ifuatavyo:






Safu Mpya  Uongozi wa Juu CHADEMA.
NGAZI YA UONGOZI
WANAWAKE
WANAUME
Mwenyekiti
0
1
Makamu Mwenyekiti Bara
0
1
Makamu Mwenyekiti Zanzibar
0
1
Katibu wa Chama
0
1
Naibu Katibu wa Chama
0
1
Mwenyekiti Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)
0
1
Makamu wa BAVICHA Bara
0
1
Makamu wa BAVICHA Zanzibar
0
1
Mwenyekiti
Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA)
1
0
Makamu Mwenyekiti (BAWACHA) Bara
1
0
Makamu (BAWACHA) Zanzibar
1
0


Hitimisho

Kufikia usawa wa jinsia ni nguzo kubwa katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi, siasa na jamii katika taifa. Vyaama vya siasa vina jukumu kubwa la kuhakikisha msingi wa usawa wa jinsia unaongoza itikadi,mikakati na mfumo wa uongozi katika ngazi zote za maamuzi ndani ya vyama.. Kutambuliwa kwa msingi huu katika Rasimu ya Katiba uende sambamba na kuweka msingi wa kuwajibisha vyama vyote vya siasa katika kutekeleza na kulinda msingi huu. 

No comments: