Wednesday, October 1, 2014

NINI KIFANYIKE BAADA YA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUMALIZA KAZI YAKENINI KIFANYIKE BAADA YA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUMALIZA KAZI YAKE 04.10.2014
Endapo Bunge Maalum la Katiba Litapitisha  Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kwa wingi wa kura za ndiyo za Wajumbe wa Bunge hilo,  Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete atakabidhiwa rasimu hiyo na Kuwa Katiba Inayopendekezwa.  Hatua inayofuata kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni  utoaji wa elimu na uhamasishaji kwa Umma juu ya maudhui yaliyomo kwenye Katiba Inayopendekezwa na Kampeni ya Upigaji wa Kura ya maoni.

Elimu kwa Umma
 Ratiba kamili ya muda wa kutoa elimu kwa umma kuhusu   maudhui yaliyomo  katika Katiba inayopendekezwa  itatolewa kupitia Tanagazo la Gazeti la Serikali (Government Notice).
Kwa madhumuni ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kuipigia kura ya maoni Katiba inayopendekezwa, Tume italazimika, na vyama vya siasa na vyama vya kijamii vinaweza kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku thelathini kuanzia siku ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.

Kipindi hicho ni muhimu sana  ili wananchi  wote kuelewa kilichomo katika Katiba inayopendekezwa ili waweze kuona kama masuala yao ya muhimu yameingizwa katika katiba hiyo.  Tunatoa wito hasa kwa wanawake na makundi ya pembezoni kutumias kipindi hicho kuisoma na kuielewa Katiba inayopendekezwa kwani ndiyo sheria mama na itakuwepo kwa muda mrefu  ni kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.  Ni muhimu kutambua kuwa katiba hii ni  ya wananchi wote kwa ujumla na si ya vyama vya siasa wala  kundi kulani katika Jamii.

TGNP Mtandao wa wanawake na katiba pamoja na mashirika mengine yanayotetea haki za binadamu tutaendelea kutumia fursa hiyo kuendelea kuelimisha  na kuraghbisha wananchi kuhusu  Katiba inayopendezwa. Hii itasaidia  sana wakati wa  kuipigia kura ya maoni juu ya Katiba inayopendekezwa wananchi wawe wana uelewa wa kutosha kuhusu  yaliyomo katika katiba hiyo na hatimaye wapige kura wakiwa na maamuzi sahihi.

Zoezi la kupigia kura Katiba inayopendekezwa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ndani ya siku kumi na nne baada ya kuchapishwa kwa maswali katika Gazeti la Serikali itaainisha:
(a) siku ambayo kura ya maoni itafanyika;
(b)muda wa upigaji kura ya maoni; na
(c)muda wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupiga kura ya maoni juu ya Katiba inayopendekezwa  
Kila mwananch mwenye umri wa miaka  18  na kuendelea  kwa wale waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura atahusika kupigia kura  Katiba inayopendekezwa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi Itasimamia mchakato wa Upigaji wa kura ya maoni.  Wapigaji kura watatumia  kadi au vitambulisho vya mpiga kura swali la kujiuliza ni kwa wale ambao hawana vitambulisho hivyo itakuwaje? Kwa mujibu wa Sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 kura hiyo itakuwa ni ya  siri na wapiga kura wataipigia kura ya NDIYO au HAPANA Katiba Inayopendekezwa na itatakiwa kupata wingi wa kura za Ndiyo za zaidi ya asilimia hamsini ili iweze kupita kwa pande zote mbili za Muungano na endapo haitapita Katiba ya Sasa itaendelea kutumika.


Zoezi la kufanya mabadiliko katika katiba ya 1977

Kutokana na taarifa zilizotolewa kupitia vyombo vya habari baada ya kikao cha Mheshimiwa Rais na wajumbe wanaounda Taasisi ya Kidemokrasia Tanzania (TCD), Katiba inayopendekezwa  haitakuwa tayari  hadi hapo baada ya uchaguzi Mkuu wa  2015. Kutokana na hilo  maazimio yaliyofikiwa ni kufanya baadhi ya mabadiliko muhimu kwenye  katiba ya mwaka 1977   ili iweze kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Pamoja na kwamba  serikali haijatoa tamko rasmi au mwongozo wa jinsi ya kuendesha zoezi hilo,  baadhi ya vyama vya siasa vimesha pendekeza mabadiliko wanayotaka yafanyiwe kazi. Sisi  Mtandao wa wanawake na  Katiba  tunadai  taarifa  rasmi kutoka katika mamlaka husika za serikali kuhusu suala hili zito na nyeti kuhusu mabadiliko ya katiba ya 1977 kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi ujao. Tunadai pia Serikali itoe mwongozo wa namna wananchi watakavyoshirika katika mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba kwani  tunaamini kuwa hili ni suala la wananchi wote na sio la wanasiasa peke yao.

Pamoja na mapungufu hayo ya taarifa rasmi, sisi  Mtandao wa Wanawake na Katiba tunatoa mapendekezo yetu ya awali kuhusu  mabadiliko katiba ya 1977 endapo yatalazimika kufanyika.

i)                Hamsini kwa  hamsini katika  nafasi zote za uongozi
ii)             Ajenda hii si ngeni, nchi ya Tanzania imeridhia Maazimio mbalimbali ya kimataifa na kikanda katika kufikia azma ya usawa wa kijinsia katika uongozi. Azimio la Umoja  wa Afrika (AU Convention 1963)na  Mkataba wa Nyongeza wa SADC (Maputo Protocol 2003) uliagiza nchi wanachama  kufanya kuweka mikakati makusudi (affirmative action) ili kuwezesha kufikia  50/50 usawa wa kijinsia katika ngazi za maamuzi  ifikapo mwaka 2015.
. Huu ni muda muafaka kwa Tanzania  kutimiza  ahadi hiyo. Tunatarajia  katika marekebisho ya Katiba ya 1977 suala hili la 50/50 katika ngazi za maamuzi  litapewa kipau mbele.
Kwanini tunadai 50/50?

a.     Mfumo huu utaweka msingi madhubuti utakaoimarisha msingi wa usawa.
b.    Utalazimisha vyama vya siasa kusimamisha wagombea wenye sifa, na kuwawezesha wagombea wao wanawake na wanaume kushinda.
c.      Vile vile mfumo huu hautawabebesha wawakilishi mzigo wote wa gharama za uchaguzi kwani sehemu kubwa ya gharama za uchaguzi zitabebwa na vyama husika, au kwa wagombea binafsi mzigo utabebwa na kundi litakalokuwa linawaunga mkono.
d.    Wawakilishi watakaochaguliwa kwa mfumo huu, watawajibika zaidi kwa wapiga kura wao, ambao hawakulazimika kununua kura zao, bali waliwachagua kwa imani ya ueledi wao katika jimbo husika.
e.      Kwa njia hii, rasilimali za uchaguzi zitatumika kwa kuzingatia usawa, tutapunguza rushwa kwenye kuwania uchaguzi, na hatimae taifa litanufaika zaidi kwa kupata wawakilishi waliyo bora na imara.  Pamoja na ubora wa mfumo huu, kuna wanaoona changamoto zake.
iii)         Tume huru ya uchaguzi inayozingatia uswa wa jinsia
Kuwa na tume huru ya uchaguzi ni kilio cha muda mrefu  cha wananchi. Sisi Mtandao wa wanawake na katiba tunadai tume huru ya uchaguzi  ambayo ina uwakilishi sawa kati ya wanawake na wanaume. Hii itasaidia masula ya wanawake na makundi ya pembezoni kupata nafasi na kuzingatiwa katika maamuzi yote ya Tume ya Uchaguzi

iv)           Mgombea Huru
Tunadai pia katika mabadiliko ya Katiba ya 1977  sula la mgombea huru lipewe kipaumbele kwani ni wananchi wengi hususan wanawake wenye uwezo mkubwa lakini si wanachama wa chama chochote na hawana utashi wa kujiunga na chama chochote. Iwapo suala la mgombea huru litapitishwa wanawake na wanaume wengi watapata fursa ya kugombea nafasi mbali mbali bila kufungwa na chama cha siasa. Hii itapanua demokrasia na ushiriki katika  masuala ya uongozi bila vikwazo na ubaguzi.
v)                   Usawa wa Kijinsia ndani ya vyama vya siasa kama kigezo cha usajili na chama kuingia kwenye uchaguzi.
Vyama vinatakiwa kuwandaa wagombea kutoka makundi yote ya vijana na watu wanaoishi na ulemevu.

Imeandaliwa na:
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji (TGNP)
No comments: