Wednesday, October 1, 2014

Kwa nini tunahitaji Chombo cha Uwajibikaji Cha Kusimamia Utekelezaji wa Misingi Ya Usawa Wa Jinsia



Mtandao wa Wanawake na Katiba
Kwa nini tunahitaji Chombo cha Uwajibikaji  Cha Kusimamia Utekelezaji wa Misingi Ya Usawa Wa Jinsia
Ruth Meena na Usu Mallya

Tume ya kusimamia haki za wanawake na usawa wa jinsia ni moja ya vyombo vya uwajibikaji vinavyowekwa kisheria vya kusimamia utekelezaji wa misingi hizi kama ilivyobainishwa katika sheria za nchi.   Kama vilivyo vyombo vingine vya uwajibikaji vinavyobainishwa kikatiba  kazi kuu ya tume kama hii  ni  kusikiliza, kusimamia na kuthibiti ulinzi wa haki za wanawake. Tume ya kusimamia usawa wa jinsia huwezesha kusimamia demokrasia na kujenga utamaduni wa ulinzi wa haki za binadamu hususan  haki za wanawake.

Kwa nchi zilizo na tume ya usawa, chombo hiki hufanya shughuli hizi:
v Kutathmini sera na sheria ili kubaini zile zinazokinzana na misingi ya haki na usawa kama zilivyobainishwa katika katiba
v Kutoa mapendekezo ya kubadilisha au kutunga sheria zinazoendana na misingi ya haki na usawa wa jinsia.
v Kushauri na kuelekeza serikali mbinu za  kutafsri mikataba ya kimataifa kuhusu haki za wanawake ziwe sheria na sera za nchi
v Kubuni na kuelekeza serikali na vyombo vyake   mikakati ya kupunguza tabaka la jinsia na kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
v Kusimamia vyombo vingine ndani ja jamii ili kuthibiti utekelezaji wa misingi ya usawa wa jinsia
v Kusikiliza mamalamiko kuhusu ukiukwaji wa haki za msingi ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa jinsia na ukatili wa kijinsia.
v Kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za msingi za wanawake na watoto
v Kutengeneza vigezo na viashiria  vya kupima utekelezaji wa sera, sheria na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za wanawake
Mwelekeo wa nchi nyingi sasa huvi hasa zenye dhamira  ya dhati ya kupunguza na hatimaye kuondoa tabaka au pengo la jinsia zimeingiza ndani ya katiba Chombo kitakachowajibika kusimamia dhamira ya nchi ya kutokomeza ubaguzi wa jinsia. Jirani zetu Malawi na Rwanda na Afrika ya Kusini wana vyombo vya uwajibakaji na masuala ya jinsia ndani ya katiba zao. Kwa upande wa Kenya wameamua kuongezea hadidu rejea  kwenye Tume ya Haki za Binadamu na kuipa wajibu wa kusimamia misingi ya usawa wa jinsiaasuala ya Jinsia.   Tume hii kwa sasa inaitwa Tume  ya Haki za Binadamu na Usawa. Kati ya hadidu rejea za tume hii, ni  kusimamia utekelezaji wa haki za wanawake  ndani ya jamii   na kusimamia uzingatiaji wa masharti ya haki hizo (Compliance); kuwajibisha  serikali kuhusu kutekeleza sera, na mikataba ya kikanda na kimataifa. Kusimamia ulinzi wa haki za wanawake na kujenga utamaduni wa kuheshimu haki hizo katika taasisi za umma na binafsi.
Kwanini tutake kuhimiza kundwa kwa chombo cha uwajibikaji wa masuala ya jinsia ndani ya katiba mpya ya Tanzania?

Kwanza kabisa mapendekezo ya rasimu ya Katiba Mpya yameingiza dhamira, malengo na misingi ya kujenga jamii iliyojikita katika usawa wa jinsia. Dhamira hizi siyo ngeni katika historia ya nchi yetu. Katiba ya sasa na  baadhi ya sheria na  sera za nchi zimekiri dhamira ya kujenga usawa wa jinsia. Vilevile tuna wizara ya Maendeleo ya Jamii na Jinsia na vitengo katika wizara zote pamoja na Taasisi mbalimbali vinavyoshughulikia masuala ya jinsia na ubaguzi wa wanawake. Hata hivyo vyombo hivi havina mamlaka ya kisheria ya  kuwajibisha   wizara nyingine au taasisi za umma na zile za sekta binafsi   vyombo vingine kutekeleza dhamira na malengo ya kikatiba. Wizara na taasisi hizi havina mamlaka ya kisheria ya kuamuru uchunguzi wa uvunjwaji wa misingi ya usawa wa Jinsia katika taasisi za umma au zile za binafsi.   Matokeo yake ni ukiukwaji wa misingi ya usawa wa kijinsia  unaendelea kutokana na muktadha wa ukosefu wa chombo cha kikatiba cha kuwajibisha uzingatiaji wa dhamira na misingi.
Athari za kukosekana kwa chombo cha uwajibishaji chenye mamlaka ya kikatiba ni ukiukwaji wa misingi ya usawa inayoashiria kuongezeka kwa pengo//tabaka la jinsia. Kama tulivyobainisha katika madai ya kutetea hoja ya kuingiza misingi ya usawa wa kijinsia katika katiba, pengo la jinsia hapa Tanzania limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka badala ya kupungua.

Utafiti uliyofanywa na Global Economic Forum mwaka 2013 ulibaini kwamba pengo la jinsia limezidi kupanuka na Tanzania imeshuka sana katika nyanja zote za elimu, afya, uchumi na uongozi. Mwaka 2006 Tanzania ilikuwa ya 26 kati nchi zilizofanyiwa utafiti wa ujenga usawa wa jinsia. Hali hii  ilishuka hadi kuwa nchi ya  52 mwaka 2009, ikaendelea kushuka hadi  kufikia 57  mwaka 2010, ikafika ya 63 mwaka 2012, na kufikai 60 mwaka 2013. Mwaka jana 2013 imeshuka kufikia ya 70. Maeneo yaliyosababisha zaidi ni elimu ilikuwa ya 118, afya 112, na siasa 32. Mambo  muhimu ya kujiuliza ni : kwa nini pengo la jinsia linaongezeka?  ni nani anasimamia utekelezaji wa mikakati ya haki na usawa wa jinsia? Nani anawajibika?
Katika nyanja ya elimu tunaambiwa kwamba pamoja na jitihada za serikali kuwekeza katika kupanua elimu watoto wa kike wanaoingia shule za msingi hawamalizi, na wale wanaomaliza hawafanyi vizuri hivya ni wachache sana wanendeleza vipaji vyao hadi elimu ya juu. Kwa nini hali hii inazidi kuwa mbaya?? Pamoja na kuwa na tume ya haki za binadamu, kwa nini ukatili dhidi ya wanawake na watoto unazidi kuongezeka? Ni chombo gani chenye mamlaka ya sheria ya kuchunguza na kusikiliza mamalamiko dhidi ya ukiukwaji wa haki za msingi za wanawake na watoto wa kike??  Ni dhahiri kuwa kukosekana kwa chombo cha kikatiba cha kufuatilia na kutathmini masuala ya kijinsia ni pungufu kubwa ambalo linafanya juhudi zinazofanyika na taasisi mbalimbali zisiwe na matokeo tarajiwa. Kwa mantiki hii, kuwepo kwa chambo hiki kutaashiria dhamira na nia ya dhati ya kushughulikia na badaye kutokomeza pengo la jinsia katika nyanja zote za kijamii.
isi tunaelewa kabisa kwamba kuwepo kwa chombo siyo suluhu ya matatizo yote yanayoashiria ukiukwaji wa haki za wanawake na watoto wa kike. Lakini  tunaamini chombo chenye mamlaka ya kisheria kitakuwa na nguvu ya kusimamia na kuzuia hali isiendelee kuwa mbaya.

Hitimisho
 Kimantiki, chombo kilichopewa mamlaka ya kikatiba kufanya kazi  hizo zilizoainishwa katika makala hii  kitakuwa na nguvu ya kisheria ya kufuatilia utekelezaji wa  dhamira, malengo na misingi iliyobainishwa ndani ya katiba kuhusu masuala ya jinsia. Chombo hiki pia kitakuwa na jukumu la kushirikiana na vyombo vingine vya uwajibikaji ili kujenga misingi imara ya demokrasia, uwajibikaji na utawala bora kwa mrengo wa jinsia.


No comments: