Friday, October 10, 2014

Wanaharakati Wakamatwa na Polisi kwa Kuandamana



Wanaharakati Wakamatwa na  Polisi kwa Kuandamana
  • Mashirika ya kimataifa yaingilia kati

Angalizo la Mhariri: Hili ni Tamko la FemAct lililotolewa kwa umma baada ya Jeshi la Polisi kuwashikilia wanaharakati kwa kuandamana ili kushinikiza serikali kusitisha mgomo wa madaktari uliofanyika Januari na Februari 2012 . .”
Sisi, wanachama wa Muungano wa Wanaharakati tunaotetea usawa wa kijinsia, haki za binadamu na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) nchini Tanzania  tunaojumuisha zaidi ya asasi za kiraia zipatazo 40 tumechukizwa na tendo la kukamatwa kwa wanaharakati 16 tarehe 9 Februari 2012 jijini Dar es Salaam na kufunguliwa kwao mashtaka eti kwa kosa la kufanya mkusanyiko haramu.

Miongoni mwa waliokamatwa ni wafanyakazi  wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Helen Kijo-Bisimba, Anna Migila, Marcus Albany na Godfrey Mpandikizi; Ananilea Nkya, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi Habari Wanawake Tanzania (TAMWA); Irenei Kiria, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la SIKIKA; wafanyakazi na wanachama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wakiwemo Dk. Diana Mwiru, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia, Anna Kikwa, Mkuu wa Idara, Utawala na Fedha na Dorothy Mbilinyi, Afisa Mwandamizi wa Programu, Ukuzaji wa Mitaala na Mafunzo, Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia(GTI); wajumbe kutoka vikundi na mitandao ya kijamii, wakiwemo: Specioza Mwankina, kutoka Mtandao wa Watu wenye Ulemavu washio na VVU (NEDPHA); Esther Tibaigana kutoka Kikundi cha Wanawake cha Tushikamane; Janeth Mawinza wa Kikundi cha Wanawake cha Jipange na Mwanaidi Mkwanda kutoka kikundi cha Community Care.


Wanaharakati hawa walikamatwa wakiwa wanaelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kusubiri hatma ya mazungumzo kati ya Waziri Mkuu na madaktari kutoka hospitali za umma ambao kwa majuma kadhaa walikuwa katika mgomo wa kushinikiza madai yao ya muda mrefu. Siku moja tu kabla ya kukamatwa zaidi ya wanaharakati 200 wakiwemo waliokamatwa waliandamana kwa amani kupinga ukimya mrefu wa serikali ambapo mamia ya Watanzania wakipoteza maisha kwa kukosa haki yao ya kupata huduma za afya stahili kwa vile serikali imekosa kuingilia kati na kutatua madai ya madaktari.

Maandamano hayo yaliyoitishwa kwa ushirikiano wa  FemAct, Jukwaa la Katiba, Policy Forum, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na asasi nyinginezo yalimulikwa vyema na vyombo vya habari kwa vile yalifanyika kwenye barabara inayotumiwa na wanasiasa wengi pamoja na viongozi wa serikali na kusababisha msongamano wa takriban masaa mawili.

Hakika mashtaka dhidi ya wanaharakati ni haramu na ya kukemewa hasa ukizingatia kuwa wanaharakati hao walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya kujieleza (Ibara ya 18); na pia wakilinda haki ya kuishi ya Watanzania wenzao (Ibara ya 14) ambao walinyimwa huduma za dharura na za kuokoa maisha yao.

Sisi, tulioweka sahihi yetu hapo chini, kwa pamoja tunaeleza kutofurahishwa kwetu na vitendo na hatua za Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla kwa namna walivyolishughulikia suala hili.


No comments: