TGNP WASHIRIKIANA NA WAJIKI KUPIGA VITA UKATILI
WA KIJINSIA MWANANYAMALA
JAMII imetakiwa kuunaganisha nguvu kupiga vita vitendo vya
Ukatili wa Kijinsia majumbani na katika mazingira ya kazi na kushirikiana na
jeshi la polisi ili watuhumiwa wanaofanya ukatili waweze kufikishwea kwenye
vyombo vya sheria.
Maandamano yakiwa yamekaribia |
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya siku ya rangi ya
chungwa duniani, iliyoadhimishwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Taasisi na
Wanawake katika Jitihada za Maendeleo (WAJIKI) katika viwanja vya Minazini Mwananyamala Kinondoni Jijini Dar es salaam,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi alisema kuwa Jamii ya Tanzania
inatakiwa kujiuliza ni kwanini kuna ongezeko kubwa la matukio ya ubakajai,
vipigo, udhalilishwaji wa wanawake na wasichana
wakati huu zaidi.
Alisema kuwa wanaharakati wa masuala ya Ukatili
wa Kijinsia wanafanya maadhimisho hayo katika ngazi ya Jamii kushiriki kupiga
vita aina yoyote ya ukatili wa kijinsia, wakivaa mavazi ya rangi ya chungwa
kuonesha kuwa wanapinga kikamilifu bila uoga kila aina ya ukatili wa kijinsia
wanaofanyiwa wanawake na wasichana.
“Pamoja na juhudi zinazofanyika za kuwapeleka
watoto wa kike shule bado kuna tatizo la udhalilishwaji na ukatili mkubwa
wanaofanyiwa, ubakaji unaenda hadi kwa vitoto
vichanga, tunajiuliza kama watoto waodogo
wanaobakwa wanakosa gani? Hawa wabakaji
wanatoka wapi? Kwanini hawaishi pamoja na kwamba kuna wanaokamatwa na
kuchukuliwa hatua kali?”alisema Liundi
Washiriki wa GDSS wakiwa na Mabango kwenye maandamano yaliyofanyika Mwananyamala kupinga Ukatili wa Kijinsia |
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji (TGNP) Lilian Liundi akiwaongoza wananchi katika maandamano ya kupinga ukatili wa kijinsia |
Alisema kuwa Mimba za utotoni ni tatizo kubwa
ambalo linakwamisha na kufifisha kabisa ndoto ya motto wa kike ya kupata elimu
na kufikia ndoto nzuri.
Aliongeza kuwa Utafiti uliofanywa na TGNP
Mtandao katika mikoa ya Mbeya, Shinyanga, Morogoro na Dar es salaam, umebaini
kwamba kuna tatizo kubwa la kimfumo ambalo limesbabisha maelfu ya wasichana
kukosa masomo kutokana na ukatili wa kijinsia.
Liundi alisema kuwa hatuwezi kuondoakana na
umasikini wakati idadi kubwa ya wasichana hawaendi shule au wamekatishwa masomo
kwasababu taifa linatakiwa kuwa na watu waliosoma na wanaoweza kupambana na
changamoto za kiuchumi wakiwa na uelewa wa kuchambua na kupambanua masuala
yanayowazunguka. Lazima kupambana na biashara haramu ya watoto wa kike ili
kuwapa fursa ya kusoma na kujenga uchumi pale walipo wakifanya kazi zenye
staha.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa WAJIKI, Janeth Mawinza alisema kuwa hakuna mtu mmoja mmoja au kikundi au taasisi
moja inayoweza kupambana na kumaliza kabisa tatizo la Ukatili wa Kijinsia bila
kuunganisha nguvu.
Alisema kuwa WAJIKI chini ya Kituo cha Taarifa na Maarifa
Mwananyamala wamafanikiwa kupambana na kesi nyingi za Ukatili wa Kijinsia na
hadi kuzifikisha mhakamani kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya
wananchi, viongozi wa serikali ya mtaa, kata, Jeshi la Polisi Kinondoni na
Idara ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Kinondoni.
“Ukatili mkubwa unaendelea katika Jamii, yetu,
matukio tuliyoyaibua ni machache, tunahitaji ushirkiano wa kutosha kutoka kwa
Jamii ili kukomesha kabisa matukio haya na jeshi la polisi liendelee kutusaidia
kuchukua hatua pale tunapowapa taarifa.
Zaidi ya wasichana 100 sasa wameshafanyiwa ukatili katika eneo hili na bado
hatujaweza kupata taarifa zote”alisema mawinza
Kwa upande wake Mkuu wa dawati la Jinsia Mkoa
wa Polisi Kinondoni, Prisca Komba alisema kuwa
askari polisi atakayejaribu kupuuza kesi ya ukatili wa kijinsia
atachukuliwa hatua za kinidhamu na kuwataka mawakili au waendesha mashtaka wa
serikali kutumia muda kusoma kwa umakini taarifa za maelezo na vielelezo
vilivyoko kwenye majalada ya kesi za ukatili wa Jinsia zilizofunguliwa ili haki iweze kupatikana mahakamani.
“ Ninawataka askari Polisi wote kuwa makini, na
kutokuwasumbua wahanga wa ukatili wa kijinsia, na waendesha mashtaka au mawakili wa serikali
kuchukua muda kuyasoma majalada ya kesi hizi za ukatili ili kutokuhitimisha
kesi hizi kiholela na kuwapa washtakiwa uhalali wa kuwa huru wakati wametenda
kosa. Wewe polisi jiulize kama aliyefanyiwa ukatili angekuwa mwanao, mama yako,
Binti yako ungefanya nini? “alihoji Komba.
Pamoja na kutoa tena namba zake za simu kwa
umma ambazo ni 0655664979 ili apigiwe
kupewa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake, aliwataka
madaktari wa vituo vya afya na hospitali za umma wanaowafanya wahanga wa
Ukatili wa Kijinsia vipimo kukubali kujitokeza mhakamani kutoa uahshaidi pindi
wanapohitajika.
Katika juhudi za kutokomeza ukatili wa
kijinsia, Julai 2012 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kupitia kampeni yake
ya UNiTE (Tushikamane kutokomeza Ukatili kwa Wanawake) alitunuku kila tarehe 25
ya kila mwezi iwe siku ya Orange (Orange Day au siku ya rangi ya Chungwa).
Katika siku hii watu huvaa nguo za rangi ya chungwa na kupinga ukatili dhidi ya
Wanawake aidha kwa kuelimisha ama kuhamasisha jamii kuungana katika vita dhidi
ya ukatili wa Wanawake. Mada ya mwezi huu ni ‘Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Mtoto
wa Kike’
No comments:
Post a Comment