Monday, December 10, 2012

Tujivunie nini miaka 51 ya uhuru?

JANA tulipoadhimisha miaka 51 ya uhuru wa Tanganyika, Watanzania wa kada mbalimbali wanakitazama kipindi hicho kwa namna tofauti, kama wanavyoeleza katika mahojiano haya yaliyofanywa na  Elias Msuya. Endelea…

Frank Moyo
NDANI ya miaka 51 ya uhuru, kuna mambo mengi ya maendeleo yamefanyika. Kwa mfano, kuna ajira nyingi, rasmi na zisizokuwa rasmi, zimejitokeza. Wakati huu vijana wengi tumejiajiri kwenye usafiri wa bajaj, hii inasaidia kujikimu kimaisha.
 

Siyo kwamba tunapata fedha nyingi, lakini tunaweza kujikimu tu kimaisha.
Hata hivyo naweza kusema kuwa bado nchi yetu haijaendelea kama zilivyo nchi za wenzetu. Wenzetu wana treni zinazopita chini ya ardhi, wana barabara za angani (flyovers). Sisi bado reli na barabara ni zile zile tu.
 

Nashauri Serikali iwaangalie na wananchi walio katika ajira zisizo rasmi kwa kuwa ndiyo wengi kuliko watumishi wa umma na wafanyakazi walio katika sekta rasmi.
Serikali pia iimarishe miundombinu kama reli na barabara ili kuongeza maendeleo.


Japhet Kanyika
SAWA tumepata uhuru, lakini ni wa maneno tu. Hakuna uwajibikaji wa kweli wa kuleta maendeleo.
 

Kwa mfano elimu yetu tangu tumepata uhuru bado haijazaa matunda katika jamii. Watanzania wengi hawana elimu ya kuwawezesha kueleza kero zao, ukilinganisha na raia wa Kenya ambao wanajua haki zao kwetu bado.
 

Utakuta mtu hajui hata haki zake au anashindwa kueleza shida yake, mwisho anabaki na umasikini wake.
 

Kwa upande mwingine, ukiangalia maeneo ya vijijini, vijana wengi wamejiajiri kwenye biashara ya bodaboda, lakini hawana mafunzo ya kutosha ya biashara hiyo.
Isitoshe Serikali inaweka ukiritimba kwa vijana, mfano kijana akihitaji leseni ambayo gharama yake ni Sh40, 000 tu, atazungushwa hadi anajikuta ametoa Sh200, 000.

Kwa upande wa kilimo, mimi ni mkulima natoka wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Wakulima wengi hawana elimu ya kilimo, matokeo yake wanalima mashamba makubwa bila utaalamu, hivyo kuishia kupata mazao kiduchu. Wanatumia nguvu na fedha nyingi lakini hakuna cha zaidi wanachopata.
Nashauri Serikali iwekeze kwenye elimu ili wananchi wajikwamue kiuchumi.


David William
MIAKA 51 ya uhuru, bado hatuna la kujivunia kwa sababu vijana wengi hatuna ajira. Ukiacha vijana waliosoma hadi vyuo vikuu, lakini wengi wetu hatuna cha kufanya, tumebaki na umasikini mtupu.
 

Mimi ni mwanamichezo na nimechezea timu za Kombaini ya Makuburi na Simba ‘B’, lakini nimeshindwa kuendelea kwa sababu ya mazingira magumu. Sina uwezo wa kujikimu kimaisha wala kujikita kikamilifu kwenye michezo.
 

Hilo ndio tatizo linalotukumba sisi vijana. Naamini kabisa kwa kipaji changu hiki cha michezo ningefika mbali, lakini kwa umasikini huu nimeshindwa.

Serikali haina mkakati wowote wa kutukwamua vijana, ndiyo maana sioni faida za kusheherekea uhuru.
Kwa sasa najishughulisha na biashara ya taxi ili kujikimu kimaisha hata kama ndoto yangu ya kuwa mwanamichezo imepotea.

Naishauri Serikali iwekeze kwenye michezo kwa kutambua vipaji vya vijana na kuviendeleza. Waanzishe shule za soka na michezo mingine.
Huko ndiko tutakapotokea, siyo lazima vijana wote tukae ofisini, hata huku mitaani tunaweza kujikwamua. Kwa nchi za wenzetu wanamichezo wanalipwa vizuri kuliko hata maofisa wa Serikali.


Saleh Mpiga
NI kweli katika miaka hii 51 ya uhuru kuna mafanikio mengi yaliyopatikana. Uchumi umekua, kilimo kimeimarika, barabara zimejengwa na miundombinu mingine, ukilinganisha na miaka ya nyuma.
 

Lakini bado kuna tatizo la ajira kwa vijana. Wengi hatuna ajira tunaishi maisha ya kubahatisha. Kibaya zaidi hata vijana waliosoma vyuo vikuu hawana ajira.
 

Chanzo cha tatizo hili ni utandawazi ambapo raia wa mataifa mengine wanakuja na kuchukua ajira zetu. Ukifuatilia utaona elimu zao ziko juu, sisi tunaishi kwa ujanja tu.
Tatizo jingine liko kwa viongozi wetu ambao wamekalia kujilimbikizia mali kuliko kujali maslahi ya umma. Wananchi wengi wanataabika kwa umasikini lakini wao wanafaidi kwa maisha ya anasa.


Ally Juma
KWA kweli mimi bado sijaona matunda ya uhuru, ikiwa hadi leo, wakulima vijijini wanakosa hata matreka ya kulimia.

Serikali imeshindwa kupeleka matrekta ili kuwasaidia wakulima, matokeo yake wanalima kwa kubahatisha tu na bei za vyakula zinakuwa juu kwa sababu kilimo hakijaboreshwa.
 

Mimi nimetokea Mzumbe, Morogoro ambako nilikuwa mkulima. Kule matrekta yanamilikiwa na watu wachache. Mbunge wetu alikuwa na matrekta yake ambayo hayakuwa yakitumia na wananchi wote.
 

Tunashindwa kuelewa kwa nini Serikali isipeleke matrekta hayo kwa Serikali za vijiji ili wananchi wachangie tu gharama za mafuta. Lakini kwa hali ya sasa mkulima atapata wapi fedha za kukodi trekta ili alime?
 

Hiyo ndiyo sababu ya vijana wengi kukimbilia mijini kutafuta vibarua. Ni tatizo la kitaifa.
Mimi sasa nimejiajiri kama dereva wa taxi. Tumeunda umoja na tuna mfuko wetu tunaokusanya fedha kwa ajili ya kukopeshana. Ila bado tunatafuta mfadhili wa kutuongeza mtaji, ili tupate mikopo ya maendeleo. Huo ndiyo ukombozi kwa vijana wasio na mitaji.
Naishauri Serikali iwekeze kwa vijana ili kuleta maendeleo ya kweli.


Zainab Kapoma
MAFANIKIO yaliyopatikana kwa miaka 51 ya uhuru kwa kweli yananichanganya. Hakuna kitu kinachoniuma kama vijana wetu wanaosoma hadi vyuo vikuu kukosa ajira, eti kwa sababu tu hawana uzoefu. Atapataje uzoefu wakati ndiyo katokea shule?

Wazee wanang’ang’ania madarakani huku vijana wakisotea ajira kwa muda mrefu. Watu wamekuwa madarakani tangu tupate uhuru lakini wamo tu. Sana sana wanawaachia watoto wao, huku vijana wengi wenye sifa wakisota tu.

Ndiyo maana nasema sioni mafanikio ya uhuru. Labda hilo treni waliloleta hapo juzi, kwa sababu tumekuwa wa kwanza kwa Afrika Mashariki na kati kuwa na treni la abira jijini Dar es Salaam.
 

Lakini nashauri kuwepo kwa utaratibu kwa vijana wenye elimu kupewa ajira haraka, siyo kwa watoto wa vigogo peke yao.



Friday, December 7, 2012

Jaji Mark Bomani awashukia polisi

KUJIRUDIA kwa matukio ya polisi kutumia silaha za moto dhidi ya raia, kumepokewa kwa hisia tofauti, huku Mwanasheria Mkuu wa Kwanza wa Serikali, Jaji Mark Bomani akilitaka jeshi hilo kuacha kutumia nguvu wanapokuwa katika operesheni zao.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kuhusu tukio la hivi karibuni la kupigwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, watu wa kada mbalimbali walisema, kitendo cha polisi kutumia nguvu sio busara.
Jaji Bomani kitendo cha polisi kutumia nguvu badala ya busara katika operesheni zao kinaweza kuleta uhasama kati ya wananchi na jeshi hilo.
“Kwa ujumla matumizi ya nguvu kwa polisi si mazuri  na nadhani tunatakiwa kubadilika katika hilo.” alisema Jaji Bomani.
Bomani alieleza kuwa  kwa ujumla polisi wanatumia vibaya silaha zao ingawa bado hajapata uhakika wa jinsi  tukio la kujeruhiwa kwa Matutu lilivyokuwa .
Alisema tukio la Mwangosi lilikuwa baya zaidi lakini picha anayoiona na kuihusisha na tukio la juzi, ni kuwa kuna matumizi mabaya ya mashambulizi ya polisi kwa raia.
Hata hivyo wakati Jaji Bomani akieleza hayo Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Amiri Ramadhan Manento  alisema kila tukio linalofanywa na polisi linatakiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kuanza kulizungumzia.
Jaji Manento alisema akiwa ni mwanasheria hawezi kutoa hitimisho ya tukio la kujeruhiwa kwa Matutu kabla ya uchunguzi wa kisheria kufanyika.
“Tunahitaji kujua mambo mengi, ya michakato ya makosa ya jinai, (criminal procedure) kwa mfano polisi walipoingia walifanya nini, walipotoka, ni maneno gani walimuuliza mtu wa kwanza waliyekutana naye.
Tunahitaji kujua iwapo walitumia kizuizi cha usalama(safe cage) katika silaha zao au la” alisema Jaji Manento
Alisema kulingana na taarifa zilizopo katika magazeti bado unahitajika uchunguzi wa kujua  ni namna gani polisi waliingia ndani ya nyumba hiyo.
Aidha Jaji huyo mstaafu alisema hawezi kuwahukumu polisi moja kwa moja kwani hakuna ushahidi kuwa walikuwa wakimwinda mwandishi, bali inawezekana waligundua kuwa ni mwandishi baada ya kumjeruhi.

Thursday, December 6, 2012

HII NI WODI YA WAZAZI YA HOSPITALI YA TEMEKE

Kwa hali hii ni kweli Serikali yetu inawajibika kwa Wananchi/ wapiga kura wake????

Wednesday, December 5, 2012

Semina: KATIBA NA HAKI ZA WATOTO YATIMA NCHINI



SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

UNAKARIBISHWA KATIKA JUKWAA LA WAZI LA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII MTOA MADA NI Daniel Samson/ UDSM

MADA: KATIBA NA HAKI ZA WATOTO YATIMA NCHINI 

Lini: Jumatano Tarehe 5/12/2012

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  


WOTE MNAKARIBISHWA

Wakili: Korti ilikosea kumvua Lema ubunge

WAKILI wa Serikali Mkuu Timon amedai kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilikosea kutengua ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, kwa madai ya kutumia lugha za matusi kwa kuwa Bunge limeruhusu wanasiasa kutukanana kwenye kampeni.

Wakili Vitalis alitoa madai hayo jana, wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Lema, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),katika Mahakama ya Rufani jijini  Dar es Salaam.
Wakati wakili huyo wa serikali akitoa madai hayo, Wakili wa wajibu rufaa, ambao walishinda katika kesi ya msingi, Alute Mughway, naye alidai kuwa Mahakama Kuu, Arusha ilikosea katika uamuzi wake, pamoja na mambo mengine, kwa kukataa baadhi ya madai yao.
Lema alivuliwa ubunge April 5, 2012, katika hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalia, kufuatia kesi iliuyofunguliwa makada watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Lema kupitia kwa Wakili wake Method Kimomogoro alikata rufaa Mahakama ya Rufani, lakini Novemba 8, 2012 mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kuini kuwepo kwa dosari za kisheria, kutokana na pingamizi lililowekwa na upande  wa wajibu rufaa.
Hata hivyo mahakama hiyo ilimpa nafasi nyingine ya  kukata rufaa tena baada ya kumpa siku 14 kufanya marekebisho ya dosari hizo za kisheria na kuiwasilisha mahakamani ndani ya muda huo, amri ambayo aliitekeleaza.
Wakati Lema akikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kumvua ubunge, wajibu rufaa nao walikata rufaa (Cross Appeal) kupinga uamuzi wa mahakama hiyo, huku wakibainisha hoja nne.
Katika hoja ya kwanza hadi ya tatu walidai kuwa Jaji alikosea katika hukumu yake kwa kuchanganya vituo vilivyotolewa ushahidi na mashahidi wanne na hatimaye akakataa ushahidi wapo, pamoja na tarehe za ratiba ya kampeni ya CCM nay a Chadema.
Hoja ya nne walidai kuwa Jaji alikosea kwa kuamua kuwa hata kama Lema kwenye kampeni zake alidai kuwa Dk. Buriani ni mkazi wa Zanzibar hatafaa, wakidai kuwa ukazi si sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge.
Hatimaye rufaa hizo zilisikilizwa jana na jopo la   Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lililoundwa na Jaji Salum Massati, Jaji Bernard Luanda, chini ya uongozi wa  Jaji Nathalia Kimaro.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mawakili wawili ambao ni ndugu, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu na kaka yake Mghway, walipambana vikali kwa hoja za kisheria.
Lisu, Kada wa Chadema ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alikuwa akimtetea Lema mrufani (Lema), akisaidiana na Wakili  Method Kimomogolo, huku Mughway akiwatetea wajibu rufani ambao ni makada wa CCM.

Udasa: Maslahi ya taifa kwanza

JUMUIYA ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), kimewataka wananchi kuweka siasa kando pale unapofika wakati wa kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa taifa.Pia, Udasa imesema iwapo raslimali za taifa zitasimamiwa na kutumika vizuri kwa mapato yanayopatikana, wananchi wake wataondokana na ugumu wa maisha.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Udasa, Dk Francis Michael alipokuwa akizungumzia Kongamano la kujadili Mstakabali wa Taifa kwa miaka 50 ijayo ya uhuru, litakalofanyika chuoni hapo Desemba 9, mwaka huu.

Dk Michael alisema kongamano hilo halilengi kukuza mitazamo ya kisiasa, bali litakuwa na nia ya kulijenga taifa kwa vizazi vijavyo.

Alisema mada kuu ‘Uhuru Wetu na Mustakabali wa Taifa kwa Miaka 50 ijayo’, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala kufungwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Tuesday, December 4, 2012

TGNP: Madawati ya Kutetea Jinsia Yasimamiwe

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umetoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa madawati yaliyowekwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini, ambayo yanatetea haki za jinsia yanasimamiwa kikamilifu ili kupunguza unyonyaji na unyanyasaji nchini.

Wito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya, jijini Dar es Salaam katika mjadala wa kupinga ukatili wa kijinsia, kauli mbiu ya mtandao huo ni ‘Tokomeza Ukatili wa Kijinsia, Jitokeze kutoa maoni ya Katiba Mpya’.

“Madawati haya yawe ni ya kusaidia na kukomesha ukatili wa kijinsia, hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba kesi zote ambazo zinafunguliwa zinasimamiwa kikamilifu,” allisema Mallya.

  Usu alisema Mikoa ya Singida na Mara inaongoza kwa kiasi kikubwa kwa ukatili wa kijinsia hususani katika suala la ukeketaji na sababu nyingine ambayo inachangia ni ukosefu wa mgawanyo sawa wa matumizi ya rasilimali za taifa.

Alisema ukatili wa kijinsia una sura tofauti na kwamba hali hiyo inaongezeka kila uchao kutokana na kutokuwepo kwa sera makini za kiuchumi zinazowalinda wanawake katika kumiliki mali.

Monday, December 3, 2012

Kumekucha Mabilioni Ya Uswisi

  • WEREMA ASEMA USALAMA WA TAIFA,INTERPOL KUSHIRIKI UCHUNGUZI NDANI, NJE YA NCHI
Na: Claud Mshana
SERIKALI imeamua kuunda kikosikazi kitakachohusisha Idara ya Usalama wa Taifa,  Polisi wa Kimataifa (Interpol) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuanza uchunguzi kuhusu  Watanzania wanaotuhumiwa kuficha kiasi cha Sh314 bilioni nchini Uswisi.
 
Hatua hiyo ya uchunguzi inatokana na Bunge kutoa maazimio ya kuitaka Serikali kufuatilia sakata hilo katika kikao chake kilichopita mjini Dodoma na kutoa majibu katika kikao cha Bunge cha Aprili mwakani.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema, “Tuhuma hizo siyo jambo dogo na Serikali haiwezi kuzipuuza, sasa tunachukua hatua madhubuti.”
Jaji Werema alisema kuwa Serikali imeshapiga hatua katika kufanya uchunguzi huo.

“Tumepiga hatua katika suala hili, ila ukianza kusema sana utakuwa unaharibu. Tumeamua kuwa na kikosi maalumu cha upelelezi kitakachoshirikisha Idara ya Usalama wa Taifa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Wizara ya Fedha na wachunguzi binafsi wakiwamo Polisi wa Kimataifa (Interpol) pamoja na Benki ya Dunia (WB).
 
“Serikali inaweza kuwashirikisha watu wengine kama Benki ya Dunia (WB) na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kwa ajili ya kusaidia uchunguzi huo.”
 
Aliongeza kuwa katika timu hiyo, wameamua kumshirikisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutaka ukweli wa sakata hilo.
“Tumeamua kulifuatilia jambo hili, kama tutafanikiwa litakuwa jambo jema. Kama hatutafanikiwa tutakuwa tumejaribu,” alisema.

Hata hivyo, Werema alisema kuwa, bado hawajamwita Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kwa ajili ya ushauriano zaidi.
“Unajua kuwa mwanasheria mkuu siyo kujua kila kitu, Zitto pia anaweza akawa na mbinu, ambazo zitasaidia katika jambo hili,” alisema Werema.
 
Uchunguzi
Hivi karibuni akiwa jijini Mwanza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika alisema kuwa Serikali ya Uswisi imeitaka Tanzania kuwasilisha kwake majina ya watu wanaotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo, kama sharti la kusaidia uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.
 
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la Kiingereza nchini, maofisa wa Uswisi walitaka ushahidi zaidi wa majina kama sharti la kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo.
 
Kwa mujibu wa habari hizo, maofisa hao waliwataka wenzao wa Tanzania kupeleka majina ya wahusika, pia kutoa ushahidi usio shaka unaoonyesha nani alimpa nani rushwa, kuonyesha mazingira ya rushwa yaliyosababisha kupatikana kwa fedha hizo.

Maofisa hao pia walitaka Serikali ya Tanzania kuonyesha jinsi fedha hizo zilivyohamishwa hadi kwenye benki zao.
 
Kauli ya Zitto
Akizungumzia masharti hayo, Zitto alisema uchunguzi utakaofanywa utafuata mfumo wa uchunguzi binafsi na kubainisha kuwa, kufuata mfumo wa kiserikali kunaweza kuwa na vikwazo vingi.
“Sisi hatufuati mfumo wa kiserikali, mfumo wa kiserikali ndiyo una masharti hayo. Sisi tunafuata mfumo wa uchunguzi binafsi,” alisema Zitto.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa