MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kutaka isitishe utekelezaji wa malipo ya Sh96
bilioni kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya Dowans kutokana na kuvunja mkataba
wa kibiashara kinyume na sheria.
Kufuatia
uamuzi huo, Tanesco sasa inatakiwa kuilipa Dowans kiasi hicho cha fedha
ambacho kwa ujumla kinaliongezea shirika hilo mzigo wa madeni.
Tanesco
kupitia mawakili wake Rex Attorneys iliwasilisha mahakamani hapo maombi
mawili; kibali cha kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama hiyo
iliyotolewa Septemba 28, 2011 na kuomba kusimamishwa kwa utekelezwaji wa
hukumu hiyo.
Katika
hukumu ya awali iliyotolewa na Jaji Emilian Mushi, mahakama hiyo
ilikubali maombi ya Tuzo kwa Dowans iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa
ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), Novemba 15, 2010.
ICC
iliamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia ya Dola za Marekani billion
65,812,630.03, kutokana na kuvunja mkataba wa kibiashara kinyume cha
sheria. Mahakama Kuu Tanzania ilikubaliana na tuzo hiyo na kuipa kampuni
hiyo nguvu ya kisheria.
Hata
hivyo, Tanesco haikuridhika na hukumu hiyo, badala yake ikawasilisha
mahakamani hapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa kuipinga.
Jana,
kwa mara nyingine mahakama hiyo iliendelea kubariki Dowans kupewa tuzo
hiyo na kutupilia mbali maombi ya Tanesco, ikiwamo pingamizi la
utekelezaji wake.
Katika
uamuzi wake aliousoma jana asubuhi, Jaji Dk Fauz Twaib alikubaliana na
hoja za Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama kwamba mahakama hiyo haina
mamlaka kisheria kusimamisha utekelezaji wa malipo hayo baada ya hukumu
ya ICC.
Awali,
wakili Fungamtama katika hoja zake, alidai kuwa maombi hayo
yamefunguliwa chini ya Kanuni ya 11 (2) na ya 47 ya Mahakama ya Rufani
ya Tanzania ya mwaka 2009.
Alidai
kuwa kanuni hiyo ya 47 inatumika kwa maombi ambayo Mahakama ya Rufani
na Mahakama Kuu nchini zina mamlaka ya kisheria lakini, katika maombi
hayo ya Tanesco kusimamisha utekelezaji wa malipo hayo, mahakama kuu
haina mamlaka hayo.
Kwa
mujibu wa Fungamtama, kanuni ya 11(2) (b) ya kanuni za Mahakama ya
Rufani za 2009, zinaihusu Mahakama ya Rufani tu na kwa maana hiyo, ni
Mahakama ya Rufaa pekee ndiyo inaweza kusimamisha utekelezwaji wa
malipo.
Hata
hivyo, wakili wa Tanesco aliyejitambulisha kwa jina la Mwandambo
akijibu hoja za Wakili Fungamtama alidai kuwa, kanuni hizo zinaipa
nguvu mahakama hiyo kusimamisha utekelezaji wa malipo iliyotolewa katika
mahakama hiyo ambazo zinakatikwa rufaa katika Mahakama ya Rufaa.
Lakini,
Jaji Dk Twaib alikubaliana na hoja za wakili Fungamtama kwamba kifungu
cha kanuni ambacho Tanesco ilikitumia katika maombi hayo, hakiipi
mamlaka Mahakama Kuu kusimamisha utekelezaji wa hukumu zake.
Jaji
Dk Twaib alisema kuwa, namna na masharti ya kusimamisha utekelezaji wa
hukumu yalivyoainishwa katika kifungu (d) cha kanuni hizo za Mahakama ya
Rufani.
Alisema
kama Wakili Fungamtama alivyoeleza kwa usahihi, kanuni hizo zinaihusu
Mahakama ya Rufaa tu kama ilivyoainishwa vizuri katika Kanuni ya 3 ya
Kanuni za Mahakama ya Rufaa za mwaka 2009.
“Mheshimiwa
Jaji Mkuu anatambua msimamo wa kisheria uliowekwa katika maamuzi
mbalimbali kwa misingi kwamba, mchakato wa rufaa unapokuwa umeanza kwa
kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa, mahakama hii inakoma
kuwa na mamlaka ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu,”, alisema Jaji.
Jaji Dk Twaib alisema mahakama hiyo inaweza kuwa na mamlaka hayo kabla kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
“Mara
tu taarifa ya kusudio la kukata rufaa inapokuwa imewasilishwa (kama
ilivyo katika kesi hii), Mahakama Kuu inakoma kuwa mamlaka,” alisisitiza
Jaji Dk Twaib na kuongeza:
“Kwa
misingi iliyoelezwa mahakama hii haina mamlaka ya kisheria
kushughulikia maombi ya kusimamisha utekelezaji yaliyowasilishwa na
muombaji (Tanesco)”, alihitimisha uamuzi wake Jaji Dk. Twaib.
Sakata
lenyewe Mwaka juzi jopo la majaji watatu wa ICC lilitoa uamuzi wa
kuitaka Tanesco kuilipa Dowans Tuzo ya Sh96 bilioni, kutokana na madai
ya kuvunja mkataba wa kibiashara kinyume cha sharia. Hata hivyo, uamuzi
huo umekuwa ukipingwa na baadhi ya watu wakisema Dowans ilirithi
mkataba haramu wa Richmond hivyo, mkataba huo haukuwa halali.
Tanesco
nayo kwa upande wake, katika maombi yake ilidai kuwa kama mchakato wa
utekelezaji wa hukumu hiyo utaendelea, itaathiri uwezo wake wa kuzalisha
na kusambaza umeme nchini na hivyo kusababisha tatizo kubwa la ukosefu
wa umeme nchini na hivyo kuathiri uchumi wa nchi kwa jumla.
Pia
lilidai kuwa iwapo maombi yao hayatakubaliwa itapata hasara kubwa na
hivyo kuathiri kwa kiwango kikubwa utendaji wake na hata kuleta
wasiwasi wa kusimama kwa shughuli zake za kila siku. Mawakili hao
walisihi mahakama hiyo kuzingatia maombi hayo kwa madai kuwa hasara
itakayotokana na tatizo la ukosefu wa umeme itakuwa ni kubwa na
isiyoweza kufidiwa kwa namna yoyote ile.
Walidai
kuwa ingawa taarifa ya kusudio la kukata rufaa siyo kigezo cha kuzuia
utekelezaji huo, lakini kwa hoja za kesi yake ni nzito kiasi cha kutosha
kuifanya mahakama kutumia uwezo wake wa kisheria kuzingatia maombi yao.
“Mahakama ina uwezo wa kuamuru kusimama kwa utekelezaji huo kwa namna
itakavyoona inafaa.”, walisisitiza mawakili hao wa Tanesco katika
maombi hayo.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari
No comments:
Post a Comment