AL I Y E K U W A mgombea wa kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya CCM katika uchaguzi wa urais wa Zanzibar na Waziri Kiongozi mstaafu, Dk. Gharib Bilal, ameteuliwa
na Rais Jakaya Kikwete kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu ujao.
Kabla ya kutamkwa kwa jina la Dk. Bilal jana saa tatu usiku, kura za ndiyo zilipigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, kumthibitisha Kikwete kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Akitangaza matokeo ya kura hizo jana jioni, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar,
Rais Amani Abeid Karume, alisema asilimia 99.16 ya wa jumbe walipiga kura za Ndiyo
kumthibitisha Rais Kikwete kuwa mgombea wa urais wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa Karume, idadi ya wajumbe wote ni 1,968, waliopiga kura walikuwa 1,909, hakuna hata kura moja iliyoharibika, kura za Ndiyo zilikuwa 1,893 sawa na asilimia 99.16 na kura za Hapana zilikuwa 16 sawa na asilimia 0.84.
Mapema ilipofika wakati wa kupitisha jina la mgombea huyo, Rais Kikwete alilazimika kuondoka katika kiti chake cha uenyekiti na kumkabidhi Rais Karume ili kuongoza mkutano.
Alikwenda kukaa katika sehemu maalumu iliyotengwa kwa viongozi wa juu wa serikali,
wastaafu, wake wao pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu.
Baada ya kupitishwa kwa kura hizo, Karume alimpisha Kikwete kurejea katika kiti chake na baadaye kidogo walikwenda katika kikao cha Kamati Kuu kumpitisha mgombea mwenza.
Juzi baada ya mgombea wa urais wa Zanzibar kutangazwa kuwa ni Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Shein, Rais Kikwete aliwashukuru na kuelezea umuhimu wa kila mgombea
katika kuleta maendeleo ya Tanzania.
Rais Kikwete alimwambia Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha kuwa yeye ni kijana mdogo, ana umri mdogo na Tanzania na Zanzibar bado wanamuhitaji.
Pia alimwambia Dk. Bilal kuwa kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi na kuwa yeye ni kiongozi makini, mzoefu, mwenye uwezo na Tanzania na Zanzibar wanamuhitaji.
Ulifuata wasaa wa kusoma wasifu wa mgombea ambao ulisomwa na Katibu wa Oganaizesheni, Kidawa Himid Saleh, kabla ya kazi ya kupiga kura kuanza.
Katika wasifu, Saleh alisema Rais Kikwete alijitokeza peke yake katika kuchukua fomu na kurudisha na kwamba alipata wadhamini 14,069 katika mikoa yote ya Tanzania.
Alisema Kamati Kuu pamoja na NEC ziliridhika kwamba Rais Kikwete anazo sifa za kuendelea kuwa Rais wa Tanzania na hivyo kuwaomba wajumbe wote wa Mkutano Mkuu kumpa kura za Ndiyo.
“Chini ya uongozi wake, Serikali imetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa mafanikio makubwa. Takribani asilimia 80 ya malengo na shabaha za Ilani zimetekelezwa
na mengine yanaendelea kutekelezwa,” alisema Saleh katikawasifu huo.
“Tumefanikiwa hivyo kwa sababu Ndugu Kikwete alihakikisha kwamba bajeti na mipango ya Serikali ya kila mwaka inazingatia malengo ya Ilani ambayo tulimkabidhi mwaka 2005.
“Katika miaka mitano iliyopita, Ndugu Kikwete ameifanya kazi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa bidii kubwa, kwa uadilifu mkubwa, kwa busara kubwa na umakini mkubwa,”
aliongeza Saleh.
Baada ya kusomwa kwa wasifu huo, waasisi wa chama wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, walipata wasaa wa kuongeza maelezo ya ziada kuhusu mgombea huyo.
Balozi Job Lusinde kwa niaba ya waasisi wa Bara, alisema Rais Kikwete ameongoza kwa staili yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya na mafanikio makubwa yamepatikana.
Alisema wakati serikali ikijivunia kuanzisha chuo kikuu cha aina ya kecha Dodoma, wakazi wa mji huo wana furaha kubwa kwa sababu uchumi wa mji umeimarika.
Kwa upande wake, maelezo ya waasisi wa Zanzibar yaliyotolewa na Hassan Nassoro Moyo, yalieleza kuwa sifa zaidi ya sita zinamfanya Kikwete astahili kupewa muhula mwingine wa
kuongoza Tanzania.
Alizitaja kuwa ni mpendwa wa watu; kiongozi shupavu, mkweli, mtekelezaji na mwadilifu; mtetezi wa Muungano na msimamizi na mtetezi wa Mapinduzi; mpenda maendeleo na
ametekeleza Ilani kwa mafanikio.
Awali, mkutano wa jana ulianza kwa burudani kama ilivyo kawaida, lakini alikuwa wanamuziki wa kizazi kipya, Marima Lawrence maarufu kama ‘Marlow’ aliyekonga nyoyo za
wajumbe akiongozwa na Rais Kikwete.
Alishambulia jukwaa na kuufanya ukumbi mzima kusimama na kucheza baada ya kuimba wimbo wake wenye mahadhi sawa na ule wa ‘Missing my baby’.
Marlow katika wimbo huo alikuwa na mashairi ya kuisifu CCM na Rais Kikwete na haya yalikuwa baadhi ya maneno ya wimbo huo: “Tumeanza kupiga honi now, pipiiii… hawaelewani, hatukuja kupoteza…tunarudi kwa kishindo, na Jakaya ni Rais, Kwa Pamoja tusonge mbele, na CCM ni zaidi.”
No comments:
Post a Comment