Tuesday, July 13, 2010

Shahidi adai kampuni aliyoleta Basil Mramba ilikuwa feki

Shahidi wa 11 katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi ya umma na kuisababishia hasara serikali, inayowakabili waliokuwa mawaziri, Basil Mramba, na Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja, ameiambia mahakama kuwa Kampuni ya Alex Sterwart (Assayers) Government Business, ilisaini mkataba na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) miezi miwili kabla haijaruhusiwa na serikali kisheria kufanya biashara zake hapa nchini.

Shahidi huyo, Frank Kanyus, ambaye ni Msajili Msaidizi wa Makampuni wa Wakala wa Serikali wa Biashara na Leseni (Brela), alidai mahakamani hapo jana kuwa kampuni, ambayo imesajiliwa nje ya nchi, ikifanya kazi nchini bila ya kuruhusiwa na serikali kisheria, ni kosa la jinai. Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Frederick Manyanda Frank (37), alidai Kampuni ya Alex Sterwart (Assayers) Government Business, ilisajiliwa nchini Marekani Desemba 13, 2002.

Alidai Juni 14, 2003, kampuni hiyo ilisaini mkataba na BoT na kwamba, iliruhusiwa rasmi na serikali kufanya biashara zake nchini kwa kupatiwa cheti cha usajili (certificate of compliance) Agosti 18, 2003, baada ya kutimiza masharti yote ya sheria za nchi.

Frank, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alidai kisheria, kampuni iliyosajiliwa nje ya nchi, ikisajiliwa nchini, husajiliwa kama tawi.

Shahidi huyo alidai anaifahamu vyema kampuni hiyo kwa vile alikuwa ni mmoja wa maofisa wa Brela waliohusika katika kuisajili.

Alidai aliajiriwa na Brela mwaka 2001 kama afisa usajili wa makampuni na mwaka 2007 aliteuliwa kuwa msajili msaidizi wa wakala huo anayeshughulikia maombi ya usajili wa makampuni, majina na alama za biashara.

Frank alidai baada ya kuhakiki maombi na vitu hivyo na kujiridhisha kama vimekidhi matakwa ya sheria, huvipeleka kwa viongozi wake wa juu.

“Tulifikia hatua ya kupokea nyaraka za Alex Sterwart (Assayers) Government Business, kuzikagua, kufungua jalada, kuhakiki na kui-foward kwa viongozi wangu wa juu. Jina la hilo jalada nililifungua mwenyewe, ndani yake niliandika kuwa nilipitia nyaraka na kuzihakiki,” alidai Frank kabla ya kulitoa jalada hilo mahakamani kama kielelezo.

Baadaye, shahidi huyo alihojiwa na wakili wa upande wa utetezi, Herbert Nyange na kuieleza mahakama kuwa anuani ya kampuni hiyo iliyomo kwenye mkataba huo inaonyesha kuwa ofisi zake zinapatikana Kitalu namba 1129, Barabara ya Chole, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam. Shahidi huyo alidai kutumika anuani kunatakiwa kufanyika, kuanzia hati ya usajili inapoanza kutolewa na kwamba, ingekuwa ni makosa kampuni hiyo kuanza kutumia anuani ya Tanzania kabla ya kusajiliwa nchini.

Nyange pia, alimhoji shahidi huyo kama hapa nchini zabuni inaweza kutolewa kwa makampuni ya nje na ya ndani na kujibu kuwa anajua. Pia, alimhoji shahidi huyo kama kampuni ya nje inaweza kushiriki kwenye zabuni bila ya kuwa na hati ya usajili na kujibu kuwa hajui.

Shahidi huyo pia alidai kuwa kampuni hiyo ilipoingia mkataba na BoT, ilikuwa inatumia anuani iliyoko Washington DC, Marekani na siyo kampuni iliyosajiliwa Tanzania na kuongeza kuwa kwa kuingia mkataba tu bila kuanza kazi hakuna matatizo.Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la mahakimu watatu wakiongozwa na Mwenyekiti, John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika, itaendelea leo.

Katika kesi hiyo, Mramba, Yona na Mgonja, wanadaiwa waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia kampuni hiyo kutolipa kodi tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na uliisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11,7.


CHANZO: NIPASHE

No comments: