Monday, November 3, 2008

Tunataka haki, si kafara za kisiasa

WIKI na miezi imepita, na sasa umepita ule muda ambao Rais Jakaya Kikwete aliwapa mafisadi waliokwiba fedha za umma za EPA, kuzirejesha.

Wakati akilihutubia Bunge, mjini Dodoma, Agosti 21, 2008, Rais Kikwete aliiongezea muda kamati yake maalumu inayochunguza wizi huo na kuipa hadi Oktoba 31 kuikamilisha kazi hiyo; hatua iliyolenga kuwapa mafisadi hao fursa nyingine ya kurejesha fedha hizo na mpaka hivi juzi wakati akilihutubia taifa katika utaratibu wake wa wa kila mwezi aliueleza umma wa watanzania kuwa muda aliowapa wanaotuhumiwa kuiba fedha hizo wazirudishe baadadhi yao hawajafanya hivyo na kusema ambao hawajarejesha watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.

Tulipata kusema huko nyuma, na hatuoni haya kurudia kusema tena na tena; kwamba haki haipo katika kurejeshwa kwa fedha hizo; bali ipo katika kuwachukulia hatua za kisheria wezi hao.

Tulisema huko nyuma na tunasisitiza kusema tena kwamba Serikali itakuwa haisimamii haki kama itaacha kuwafikisha mafisadi hao mahakamani; eti kwavile tu wamerejesha pesa walizoiba.

Na kama ndivyo itakavyotokea hiyo Novemba mosi; yaani mafisadi waliorejesha fedha hizo kutoshitakiwa, basi, ingekuwa vyema pia kwa Serikali kuwatangazia msamaha wezi wote wa pesa za umma walioko vifungoni kama nao watarejesha fedha walizokwiba.

Maana; hatuwezi kukubali kuiachia nchi yetu kuwa na sheria mbili – moja kwa wanyonge na nyingine kwa vigogo na mafisadi. Kwa usalama na amani yetu sote na ya wanetu, ni lazima tuendelee kujenga nchi ambayo raia wote ni sawa mbele ya sheria.

Aidha, wananchi walitarajia kwamba mafisadi walioghushi na kuiba fedha za EPA watakaofikishwa mahakamani, ni vigogo hasa wa wizi huo wa pesa za umma, na si watu waliotafutwa kutolewa kafara za kisiasa; ilhali vigogo wenyewe wa ufisadi wa EPA wamefichwa nyuma ya pazia.

Labda tumkumbushe tena Rais wetu, Jakaya Kikwete kwamba wizi huo wa kihistoria wa pesa za EPA, umemweka yeye binafsi katika majaribu makubwa.

Wizi huo wa EPA ni mtihani mkubwa ambao Rais anapaswa kuuvuka kwa kutenda haki, na hiyo ni kama hataki wananchi waendelee kupoteza imani na namna anavyoiendesha vita dhidi ya ufisadi nchini.

Yeye mwenyewe Rais ni shuhuda, wakati wa ziara zake mikoani, jinsi wananchi wanavyoilalamikia kero hiyo ya kushamiri kwa ufisadi nchini. Wasiwasi wetu ni kwamba kama atashindwa kuchukua hatua za kuridhisha dhidi ya wahusika, atapoteza imani ya wananchi wake, na wakati mwingine itadhaniwa kuwa kuna kundi la mafisadi nchini ambalo “halishikiki”.

Na ili hilo lisitokee, ni vyema basi, kwa Rais Kikwete kujipa ujasiri wa hali ya juu na kuwafikisha mafisadi wote wa EPA mahakamani; bila kujali walirejesha fedha walizoiba au la, na bila kujali ni wafadhili au si wafadhili wa chama chake CCM.

3 comments:

Anonymous said...

serikali iache kuongopea wananchi wake, wao wanadhani kila siku wananchi watavumilia huo uwongo wao wanoufanya? itafika kipindi watachoka na kudai haki zao. bila kufanya jambo la maana hapa wananchi wataisusa hii serikali mwaka 2010. natamani wananchi wote wangejiunga na kupambana na unyonyaji huu wa viongozi wa serikali.
mdau

Anonymous said...

wananchi wote waungane ili kukomesha aina hii ya unyonyaji wa waziwazi unaoendeshwa na serikali yetu kila kukicha. kwani bila kufanya hivyo kiazi kijacho cha watanzania kitaishi kwa taabu nyingi kwa uzembe wa watu wachache wanaopenda kujilimbikizia mimali bila kutosheka..

Anonymous said...

Serikali itambue kwamba sasa si muda wa wakuburuzana tena, wananchi wanataka mambo yaende kwa haki na si kuangalia nani ni nani! Si muda wa serikali kuwalinda viongozi wake na kuwakandamiza wananchi bali inatakiwaq kuwawajibisha viongozi halisi waliohusika na EPA.
Serikali isiweke vivuli vya wezi bali wezi wenyewe.
Wananchi wameamka hawataki tena kugandamizwa hivyo serikali itende haki vinginevyo wananchi hawatakuwa na IMANI na Serikali yao. Wananchi tusikubali kuburuzwa hata kidogo tudai haki itendeke.
By Eva