Monday, November 24, 2008

AJIRA KWA VIJANA MUHIMU BARANI AFRIKA- JK

Jakaya Mrisho Kikwete amesema Mahitaji ya ajira kwa vijana ni makubwa zaidi katika nchi za Afrika , hivyo suala la kutengeneza ajira kwa vijana hao ni changamoto kubwa ya maendeleo inayolikabili Bara hilo na dunia kwa ujumla hivi sasa.

Rais kikwete ameyasema hayo katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Afrika uliofanyika kwa siku moja tarehe 20 Novemba, 2008 Addis Ababa nchini Ethiopia ambao Mwenyekiti wake alikuwa Bwana Anders Fogh Rasmussen ambaye ni waziri Mkuu wa Denmark.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha Rose-Migiro.

Akifungua rasmi Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Sheraton Addis, Bwana Rasmussen amesema ajira ndiyo injini muhimu kwa maendeleo ya Bara la afrika na kwamba ongezeko la idadi ya vijana linawakilisha fursa pekee kwa Bara hilo ambayo inatakiwa kutumiwa kikamilifu katika harakati za kuleta maendeleo.

Amesema hatua madhubuti zinatakiwa kuchukuliwa ili kutoa msukumo katika kutekeleza Maendeleo ya Milenia (MDGs).Aidha amesema ukuaji wa uchumi hauna budi kuwanufaisha raia wote na ndiyo maana jitihada za Tume zimelenga, pamoja na mambo mengine, katika masuala ya ajira.
Kwa upande wake, Rais Kikwete amesema kwa zaidi ya asilimia 89 ya vijana duniani wanaishi katika nchi zinazoendelea na kwamba idadi ya vijana wanaoishi katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 13 ya vijana wote duniani.

Amesema ajira kwa vijana zinahitaji ongezeko kubwa la uzalishaji na utengenezaji wa fursa zaidi za ajira kwa kuongeza kiwango cha uwekezaji wenye tija zaidi.

Ameainisha mambo muhimu katika kukabiliana na tatizo la ajira kuwa ni pamoja na utekelezaji wa dhana ya ushindani, ukuaji wa uchumi, ujasiriamali, maendeleo katika biashara pamoja na maendeleo ya elimu, mafunzo na ujuzi.

Mambo mengine ni uwezeshaji na kuwepo kwa fursa za kupata mikopo na kutumia vema fursa za sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Amesema ujasiriamali unatoa fursa kubwa zaidi za ajira kwa vijana na wanawake na hivyo kupunguza kiwango cha umaskini.

Hata hivyo amesema changamoto zilizopo ni namna ya kuwawezesha vijana kuwa wajasiriamali kati ya mamilioni ya vijana waliopo ambao kwa sasa hawana ajira, namna ya kuwasaidia wale ambao tayari wameanzisha biashara zao na namna ya kuwafanya wajasiriamali wadogo kukua hadi kufikia ngazi ya kati ya ujasiriamali.

Amevitaja vikwazo viwili vikubwa vya ujasiriamali kuwa ni kukosekana kwa ujuzi wa ujasiriamali na uhaba wa fursa za kupata mitaji.

No comments: