Thursday, November 27, 2008

KILA KITUO CHA POLISI KUWA NA DAWATI LA KUHUDUMIA WAHANGA WA UKATILI WA KIJINSIA

Jeshi la Polisi nchini limejiandaa kikamirifu kuanzisha dawati (chumba) maalum la kushughulikia makosa ya ukatili wa kijinsia nchini. Kwa majaribio, kuanzia mwezi ujao (Desemba, 2008) kila kituo cha polisi kanda maalum ya Dar es Salaam kutakuwa na dawati hilo, na baadae mwakani kwa vituo vyote nchini. Hayo yalisemwa na Katibu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania, Kamishna wa Polisi Elice Mapunda, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Maafisa wa Polisi Kurasini Dar es Salaam, wakati akitoa tamko la Jeshi la Polisi kuhusu ukatili wa kijinsia kwenye tamasha la kuadhimisha siku 16 za Uanaharakati wa kupambana na ukatili wa kijinsia. Tamasha hilo liliandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kufanyika katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Mabibo, Dar es Salaam.

Aliwataka wananchi na hasa wanawake wasiwe na wasiwasi na wawe na imani na polisi. “Najua wanawake wamekata tamaa na jinsi askari walivyokuwa wanawa-treat (wanawahudumia) wakifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia. Awali tulikuwa hatujui nini maana ya ukatili wa kijinsia, lakini kwa jitihada za Mtandao wa Wanawake Polisi na Mashirika ya Wanaharakati mbali mbali, Polisi karibu wote wamepata mafunzo ya kupambana na ukatili wa kijinsia, kwa sasa tunaongea lugha moja. Tutumieni, tushirikiane tuweza kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa vitendo hivi”, alisema Kamishna Mapunda.

Aliwakumbusha wanaharakati kuwa ni haki ya kila mmoja kuhudumiwa na polisi pale anapofanyiwa ukatili wa kijinsia, na kuwataka kuakikisha kuwa watumia fursa hiyo ipasavyo. Pia alikariri tamko la mgeni rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora, Mheshmiwa Sophia Simba kuwa mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ni jukumu la jamii nzima. “Ukatili wa kijinsia ni suala la jamii nzima, si la mtu mmoja mmoja. Hivyo ili tuweze kutokemeza vitendo hivyo lazima jamii nzima tushirikiane. Polisi hawatoshi, jeshi lina takiribani polisi elfu thelathini na idadi ya watanzania ni takribani milioni arobaini kwa sasa; ambayo ni uwiano wa askari mmoja kwa watu mia nne hamsini!. Jamii nzima lazima ipambane” alisisitiza kikamanda.

Kamishna Mapunda alimalizia kwa kutoa changamoto kuwa kuwepo na dawati la kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia katika kila kituo cha polisi sio dawa, bali jamii bado inatakiwa kuelimishwa na kuamasishwa ili iweze kuona kuwa suala la ukatili wa kijinsia halifai na halina nafasi katika jamii yetu.

Tamko hilo lilipokelewa kwa furaha na mamia ya wanaharakati walioudhuria maadhimisho hayo kutoka mikoa yote ya Tanzania.

1 comment:

Anonymous said...

Labda hii itasidia kupunguza adha kubwa iliyokuwa inawasumbua akinamama wetu pindi waendapo kushitaki matatizo yanayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia. kwa kweli kwa hili polisi wameonyesha njia.
Mdau, Arusha.