Monday, November 10, 2008

Mrejesho wa Semina ya GDSS ya Tarehe 05/11/2008.

Mrejesho wa Semina ya GDSS ya Tarehe 05/11/2008.

Mada katika semina ya Jumatano ya tarehe 05/11/2006 ilikuwa ni, Mrejesho wa Wanaharakati kutoka katika vikundi mbalimbali ambao walikwenda kufuatilia kero zilizopo katika maeneo yao. Vikundi ambavyo vilifanikiwa kutoa mrejesho ni pamoja na; Kigamboni clusters, Kigogo, Makuburi, Mwananyamala, Kinondoni, na Kawe.

Baadhi ya Kero ambazo zilitajwa na wanaharakati wengi ni pamoja na;

- Haki ya kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi hasa ngazi ya Kata na Serikali ya mtaa. Katika Maeneo mengi bado wananchi hawapati fursa ya kushiriki katika vikao vya serikali za mitaa, hivyo kushindwa kufuatilia ama kutoa maamuzi ya mambo mbalimbali ya maendeleo katika maeneo hayo.

- Haki ya kupata maji safi na salama. Bado katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam maji safi na salama limekuwa ni tatizo sugu, wakazi wengi bado hawapati maji safi na salama ya kunywa na ya matumizi ya kawaida, hivyo wanawake wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji maeneo ya mbali hivyo kuwazidishia mzigo wa kazi wanawake.

- Haki ya kuendelea na masomo kwa watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni. Bado watoto wanaopata mimba wakiwa mashuleni hawaruhusuwi kuendelea na masomo, kitu ambacho kinawanyima haki watoto wa kike kuendela na masomo. Pia wahalifu wanaowapa mimba watoto wa kike hawachukuliwi hatua kali za kisheria kitu ambacho kinaongeza wigo wa tatizo hili.

- Rushwa katika vituo vya polisi na ukatili wa kijinsia. Katika baadhi ya vituo vya polisi hapa nchini vimekuwa vikituhumiwa kwa vitendo vya rushwa; ambapo askari wanawadai rushwa watuhumiwa wa kesi mbalimbali na kusababisha kupindishwa kwa haki za wadai. Pia askari wa wanaume wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuwatendea watuhumiwa wanawake vitendo vya unyanyasaji wakijinisa kwa kuwadai rushwa ya ngono.

- Ajira kwa watoto wa kike hasa wale wanaoachishwa shule ili waende kutumika katika kazi za ndani, katika mabaa, ama katika madanguro.

Changamoto.
Harakati hizi za kutatua kero za wananchi zinakabiliwa na changamoto zifuatazo;

- Changamoto kubwa iliyopo ni kuweza kuunganisha nguvu ya pamoja ya wanaharakati katika ufuatiliaji kero mbalimbali, kwa mfano wanaharakati wameshindwa kuunganisha nguvu za pamoja katika kudai maswala mbalimbali ya kijamii, jambo ambalo limesababisha nguvu nyingi kupotea inapotokea vikundi viwili ama zaidi kupigania swala moja na kuacha sekta zingine bila utetezi.

- Kukosekana kwa mbinu shirikishi katika ufuatiliaji wa mambo mbalimbali katika ngazi ya mtaa, jambo amblo limesababisha wanaharakati kufanya kazi pekee yao badala ya kuwatumia wanajamii hivyo kuweza kuongeza ushiriki mkubwa zaidi katika kufuatilia mambo. Pia hii itasaidia jamii kudai mambo ambayo wanahisi wanayahitaji zaidi kuliko wanaharakati kupambana pekee yao.

- Changamoto nyingine kwa wanaharakati ni katika kutambua kiini cha tatizo ambacho kinasababisha kuwepo kwa kero nyingi katika jamii. Kwa mfano badala ya wanaharakati kupambana na huduma mbovu za afya hasa katika swala la afya ya uzazi kwa kuwatupia mpira waauguzi wa afya pekee na kuacha mfumo mzima ambao unasababisha huduma ziwe mbaya, kwa mfano kuna hospitali zina waaguzi wawili wa afya na wanahudumia zaidi ya wazazi 50 kwa siku, kwa hali hiyo lazima huduma itakuwa si nzuri. Hivyo changamoto kwa wanaharakti ni kuongeza wigo wa mapambano na kuungalia kiini halisi cha tatizo.

Mwanaharakati unafanya nini cha ziada kuhakikisha kwamba serikali inatatua kero hizi? Kwa maoni yako, Serikali imefanya vya kutosha katika kutatua kero hizi?

5 comments:

Anonymous said...

wanaharakati bado tunasafari ndefu kuelekea katika maendeleo ya kweli ambayo kwa hayo sisi wote tunamatumini nayo. Changamto ya mawasiliano bado ni kubwa sana na tunaihitaji kuifanyia kazi wote kwa
pamoja kwa kubdilishana na kupeana taarifa tunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Nawatakieni wote kila la kheri katika mapambano hayo ya luleta mabadiliko hapa nchini.

Anonymous said...

jamai hawa serikali lini wataleta majisafi kwa kila raia wake? waache kutunyanyasa

Anonymous said...

serikali iwasaidie raia wake sio kuendeleza maeneo wanayokaa viongozi pekee yake kwani hiyo sio kuwajali wananchi, tunataka na sisi watu wa chini tukumbukwe.

Anonymous said...

Watoto wa kike waliopata ujauzito shuleni wasifukuzwe shule bali wapewe mapumziko ya miezi mitatu baada ya kujifungua waweze kuendelea na masomo
Serikali iwe na sheria ambayo itawabana watu wanaoajiri watoto wenye umri wa kuwa shuleni kuwafanya wafanyakazi wa ndani. hii itasaidia kulinda haki za msingi za watoto hasa kupata elimu
Pia nashauri Rais awe anatembelea katika magereza mbalimbali ili kujua matatizo yakijinsia yanayowakabili wafungwa.

Anonymous said...

WAtoto wa kike wanaopata ujauzito wasifukuzwe bali wapewe mapumziko ya miezi mitatu baada ya kujifungua waweze kuendelea na masomo.Hilo linawezekana kama wanaharakati tutasimama imara katika kutetea haki kwa mwanamke.
Serekali iwe na sheria ambayo itawabana watu wanaoajiri watoto wenye umri wa kuwa shuleni kufanywa wafanyakazi wa ndani.
Pia wanaharakati tuwe msitari wa mbele kuwafichua wale wote wanaoajiri watoto.
Pia nashauri Rais awe anatembelea katika magereza mbalimbali ili kujua matatizo ya kijinsia yanayowakabili wafungwa.
BY EVA