Wednesday, November 19, 2008

EPA: Kama vile mchezo wa kuigiza

Baadhi ya watuhumiwa walalamika wanasiasa kuwatosa

WAKATI baadhi ya watuhumiwa wakiwa wamekwisha kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani yaBenki Kuu (BoT), mbinu chafu zilizotumika na vigogo katika kuchota mabilioni ya fedha katika akaunti hiyo sasa zimebainika.

Mbinu hizo ni pamoja na kughushi nyaraka mbalimbali na kutumia kivuli cha siasa katika kupitisha nyaraka husika bila kufanyika kwa uhakiki wa kina wa uhalali wa nyaraka hizo, kazi iliyofanyika kwa kasi iliyowashangaza hata wakaguzi wazalendo na wale wa kimataifa waliopitia hesabu za BoT.

Mfano wa dhahiri uliotolewa tokea mwanzo ni ule wa kampuni ya Kagoda Agricultural Limited, ambayo ilithibishwa tokea mwanzo jinsi vigogo walivyoghushi nyaraka za kampuni 12 za kigeni kuweza kujichotea kiasi cha Sh bilioni 40.

Katika mchakato huo, Kagoda ilighushi nyaraka mbalimbali kuweza kujichotea kiasi cha Dola za Marekani 30,732,658.82 (takriban Sh bilioni 40), ikiwa ni pamoja na nyaraka hizo kupitishwa na maofisa wa BoT bila kufanyiwa uhakiki.

Waliowasha moto wa wizi huo walikuwa ni wakaguzi wa kimataifa wa kampuni ya Deloitte & Touche, ambao walitimuliwa na serikali baada ya kutokea kutokuelewana katika ukaguzi wa akaunti hiyo ambayo sasa inazidi kuisakama Serikali.

Deloitte & Touche, ambayo ilipewa kazi ya kukagua akaunti za BoT, ilikumbana na utata mkubwa katika akaunti ya EPA namba 99915091 01, na hivyo kuwa kiashirio cha kwanza cha utata mkubwa katika akaunti hiyo.

Maelezo yaliyoibua utata huo yanaonyesha kwamba aliyekuwa Gavana wa BoT, Marehemu Dk. Daudi Ballali, alianza kujulishwa mapema kuhusiana na wizi huo akipewa mfano wa dhahiri jinsi Kagoda Agriculture Limited ilivyoghushi nyaraka.

Mfano uliotolewa kudhihirisha uhalifu huo ni jinsi ambavyo mikataba ya ununuzi wa madeni kwa kampuni 12 ilivyosainiwa katika kipindi kifupi cha kati ya Septemba 10, 2005 na Novemba 5, 2005, kipindi ambacho kilielezwa kuwa ni vigumu kwa wahusika kutembelea mbalimbali duniani kutiliana saini.

Aidha, imefahamika kwamba nyaraka zote zilisainiwa na wakili mmoja tu B.M. Sanze, na kati ya hizo mikataba minne ilisainiwa Oktoba 18, 2005 na mitano ilisainiwa siku moja baadaye Oktoba 19, 2005, jambo ambalo lilitia shaka jinsi wawakilishi wa kampuni hizo za kigeni walivyoweza kusafiri kwa wakati mmoja wakitofautiana kwa saa chache, jambo ambalo lilishindwa kuthibitishwa kwa kutumia kumbukumbu za Uhamiaji.

Katika nyaraka hizo, mikataba miwili iliyosainiwa Oktoba 18, 2005 kuhusiana na kampuni mbili za Ujerumani, Lindeteves J Export BV na Hoechst ikionyesha kwamba kulikuwa na deni la Euro 1,164,402.76 badala ya fedha za Ujerumani (Deutsche Marks.)

Wachunguzi na wakaguzi wameshitushwa na kasi ya ajabu ya jinsi marekebisho ya makosa hayo yalivyofanyika kwa kipindi kifupi baada ya BoT kuifahamisha Kagoda Agriculture Limited; huku barua ya kutaka marekebisho yafanyike ikiwa na maelekezo ya kuidhinisha malipo ya Sh 8,196,673,600.53 kwenda kwenye akaunti ya Kagoda. Kampuni hiyo iliwasilisha mkataba uliorekebishwa siku mbili tu baada ya kujulishwa.

"Haiwezekani hata kidogo kwa kampuni ya kigeni inayodai kuandika fedha zisizo sahihi huku BoT ikiendelea kuidhinisha malipo bila kuhakiki mikataba yote 12 ambayo imeonekana kufanana kwa kila kitu ikiwa ni pamoja na maneno," inaeleza sehemu ya waraka wa wakaguzi.

Pamoja na kubainika kuwa mikataba na nyaraka zote hazikuwa na nembo ya kampuni huusika, nyaraka zote zilisainiwa katika ukurasa mmoja pekee wa mwisho tofauti na nyaraka za kisheria zinavyopasa kuwa.

Uchunguzi wa kina umebaini kufanana kwa mihuri ya kampuni zote zilizopitishwa ikiwa inalandana kabisa na muhuri wa kampuni za Kitanzania, tofauti ikiwa ni majina na anuani ya kampuni husika.

Mfano uliotolewa ni wa kampuni za Kitaliano za Fiat Veicoli Industriali na Adriano Gardella S.P.A pamoja na kampuni ya Kimarekani ya Valmet ambazo zote zimeonekana kuwa na mihuri na lugha zilizofanana katika nyaraka zote.

Utata mwingine uliodhihirika kughushi ni katika mkataba wa kampuni ya Valmet ya Marekani uliohusu Dola za Marekani 2,398,439.96 kusainiwa na Patrick Kevin, aliyetajwa kuwa Mhasibu wa kampuni hiyo, jambo ambalo limeelezwa kwamba ingekuwa vigumu kwa mhasibu kuachiwa kufanya kazi hiyo.

Utata mwingine uliobainika ni katika mkataba wa kampuni ya Daimler Benz AG ambao ulionyesha kusainiwa na Mkurugenzi aliyetajwa kwa jina la Christopher Williams, huku sahihi yake ikisomeka 'W Christopher'.

Uchunguzi wa ziada ulithibitisha kwamba baadhi ya kampuni zilikwishakufa wakati mikataba hiyo ikisainiwa na kampuni za Kitanzania, jambo ambalo linaendelea kuthibitisha wizi mkubwa wa kutumia maandishi uliofanywa katika akaunti ya EPA.

Mifano hai ni kampuni za Hoechst AG iliyobadilika na kuwa Aventis mwaka 1999, Daimler Benz AG iliyobadilika na kuwa Daimler Chrysler AG mwaka 1998 na Fiat Veicoli Industriali iliyobadilishwa na kuwa Industrial Vehicle Corporation (IVECO) tokea Januar1 1, 1975.

Kampuni nyingine zilizobadilika ni Mirrlees Blackstone kuwa MAN B&W Diesel Limited mwaka 2002/03 na Valmet iliyobadilishwa na kuwa Metso Paper kuanzia Mei 10, 2000. Utata huo uliwafanya wachunguzi na wakaguzi kujiuliza ilikuwaje kampuni zote hizo kuingia mikataba mwaka 2005 kwa kutumia majina ya zamani.

Pamoja na kuingiwa kwa mikataba hiyo na kampuni zilizokwisha badilishwa majina na umiliki wake, kampuni za sasa zenye uhusiano na kampuni zilizoingia mkataba zimekanusha kufahamu watu waliotajwa kuziwakilisha katika mikataba hiyo.

Kagoda ambayo ilisajiliwa Septemba 29, 2005, na kujichotea Sh bilioni 40 katika kipindi cha mwezi mmoja tu, jambo ambalo limewashangaza wengi kuona kampuni ngeni isiyofahamika inawezaje kuaminiwa kiasi kikubwa cha fedha bila kuhakikiwa.

"Inashangaza jinsi BoT ilivyoweza kuamini kampuni mpya kuwasilisha nyaraka za mabilioni ya fedha kwa kuingia makubaliano na kampuni za kigeni katika nchi za Ujerumani, Italia, Yugoslavia, Uingereza, Marekani na Japan kwa muda mfupi kiasi hicho bila kutilia shaka," wamehoji wakaguzi waliokagua hesabu za BoT.

Tayari kampuni ya Kagoda Agricultural Limited imekuwa gumzo katika sakata zima la EPA. Inafahamika kwamba kati ya shilingi bilioni 90 zilizoibwa katika akaunti ya EPA, sehemu kubwa ilichukuliwa na kampuni ya Kagoda Agricultural Limited ambayo hadi sasa wahusika wake hawajaguswa pamoja na kujitokeza kwa vigogo wawili kurejesha fedha zilizoibwa na kampuni hiyo.

Vyanzo vya uhakika vinaeleza kwamba sehemu kubwa ya Shilingi bilioni 90 zilizothibitika kuchukuliwa kihalifu zilichukuliwa na makundi mawili tu, kundi la kwanza likiwa chini ya Jeetu Patel na lingine likiwa chini ya usimamizi wa vigogo wawili waliotumia kampuni ya Kagoda.

Imefahamika kwamba kwa sasa kuna hekaheka kubwa za kutaka kuzuia kushitakiwa kwa wahusika wa Kagoda, lakini vyanzo vya ndani ya Serikali vimeeleza kwamba kwa sasa Serikali haitabiriki na lolote linaweza kutokea wakati wowote kabla ya mwisho wa mwaka.

Kumekuwa na utata kuhusiana na ilipo na umiliki wa Kagoda Agricultural Limited. Hakuna anayeweza kubainisha hasa zilipo ofisi na wahusika wa kampuni hiyo tata.

Kumbukumbu za BRELA zinaonyesha kwamba ofisi zake zipo Kipawa Industrial Area Plot namba 87, Temeke, Dar es Salaam lakini eneo hilo lina makampuni tofauti jirani lakini namba iliyotajwa haionekani na badala yake eneo lenye ofisi na kampuni viwanja vyenye namba 77, 86 na 88 katika eneo hilo la viwanda.

Katika ukaguzi wake wa awali wa mkaguzi wa nje Samuel Sithole kutoka kampuni ya Kimataifa ya Deloitte & Touche yenye makao yake Afrika Kusini alionya kuhusu matendo ya kihalifu ndani ya Kagoda kabla ya kuandikiwa barua na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji kwamba fedha hizo zilienda katika mambo "nyeti" ya kiusalama.

Hata hivyo siku nne baada ya kuandika barua hiyo, Meghji alifuta barua hiyo akielezea kupotoshwa na aliyekua Gavana, Dk. Daudi Ballali, uamuzi ambao ulimgharimu kwa kiasi kikubwa mwanamama huyo makini ambaye alijikuta akiachwa nje ya Baraza la Mawaziri.

Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema serikali yake haitomuingilia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), watuhumiwa wengi walikamatwa na kufikishwa mahakamani walikuwa wamejiaminisha kuwa wamekwishapona na sasa waliobaki "hawalali" kuhofia kushitukizwa na kupandishwa kizimbani.

Tayari watu 20 wamekwisha kufikishwa mahakamani baada ya wafanyabiashara watatu kufikishwa mahakamani Jumatatu wiki hii wakitanguliwa na watuhumiwa wengine wakiwamo watumishi wa BoT waliohusika katika mchakato wa wizi huo.

Waliopandishwa kizimbani ni Ajay Somani na Jai Somani wanaodaiwa kula njama ya wizi wakiwa na watu wengine ambao hawajafahamika kuiibia BoT na kwamba Septemba 2, 2005 waliiba Sh. bilioni 5.9 mali ya benki hiyo.

Mtuhumiwa mwingine aliyefikishwa mahamani ni mfanyabiashara Mwesiga Lukaza, aliyepandishwa kizimbani akiunganishwa na mshtakiwa mwingine Johnson Lukaza, ambaye alishapandishwa kizimbani mapema wiki hii.

Watuhumiwa wengine ambao tayari wamefikishwa mahakamani ni Farijala Hussein, Rajab Maranda, Japhet Lema, Bahati Mahenge, Davis Kamungu, Godfrey Mosha, Manase Mwakale na Eddah Mwakale, Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nandy, Ketan Chohan, Jayantkumar Chandubahi Patel na Johnson Lukaza.

Wengine ni wafanyakazi wa BoT ambao ni Mkuu wa Idara ya Madeni ya Biashara, Iman David Mwakyosa, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Madeni, Ester Mary Komu na makaimu Katibu wa benki wawili ambao ni Bosco Ndimbo Kimela na Sofia Joseph Lakila.

Raia Mwema
November 19, 2008

3 comments:

Anonymous said...

Kwa ukweli hapa mimi naona serikali ya Kikwete inatuchezea kiini macho, haiwekani watu wote wameiba eti wanaambiwa watakaorudisha hawatashitakiwa. Mimi sikubaliani na hili.

Pilly Saidi

Anonymous said...

Hii ni Bongo Dar es Salaam! Haiwezekani watu wenye taaluma zao wafanye kazi kwa kubahatisha! Huu ni wizi ulioboreshwa! Waliohusika na wizi huu warudishe pesa ama wafilisiwe na kutumikia kifungo EVA

Anonymous said...

Kutokana na mchakato mzima wa EPA unawaweka wananchi katika utata mkubwa sana mbona unahusisha wafanya biashara watupu wakati hata watumishi wengi hasa wa BOT wamo tena wale wakubwa wanaendelea kutesa kwa raha zao na wanasiasa. Tunaomba swala hili lisifanywe kisiasa bali sheria ifuate mkondo wake bila kuzuiliwa ili tuwaone wale ambao ni walaji EPA.